1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana na wamualika Guterres

23 Machi 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamemualika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano wao mjini Brussels, ambapo wamejadili usalama wa chakula duniani na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4P8G2
Belgien Brüssel | EU Gipfeltreffen
Picha: Olivier Matthys/AP/dpa/picture alliance

Kushiriki kwa Guterres katika mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Ulaya  kunajiri siku chache baada ya kuanzishwa upya kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki juu ya usafirishaji salama wa nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi ambayo ni muhimu katika kukabiliana na mzozo wa chakula duniani.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy anatarajiwa pia kutoa hotuba katika mkutano huo kwa njia ya video, ili kuwapa ripoti kamili viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya juu ya vita vinavyoendelea nchini humo.

Belgien Brüssel | EU Gipfeltreffen - Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/dpa/picture alliance

Akiwasili katika mkutano huo wa siku mbili, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kuwa wanahitaji kuhakikisha kuwa nafaka za Ukraine zinaendelea kusafirishwa nje ya nchi, huku Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas akisema kuwa anapinga hatua yoyote itakayolenga kuilegezea Urusi vikwazo chini ya mpango huo wa usafirishaji nafaka.

Soma pia: Viongozi wa Ulaya kuharakisha kuipatia Ukraine silaha

Mwezi Mei mwaka jana, Marekani ilitupilia mbali ombi la Urusi la kutaka kulegezewa vikwazo na nchi za Magharibi kabla ya kuruhusu usafirishaji wa nafaka za Ukraine, ikidai kuwa hakukuwepo vikwazo vyovyote kwa nafaka na mbolea za Urusi. Suala hilo la usafirishaji nafaka na mbolea limekuwa likizua mtafaruku ndani ya Umoja huo.

Msaada zaidi kwa Ukraine wajadiliwa

Belgien EU-Verteidigungsaußenminister
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Viongozi hao wanatarajiwa kuidhinisha mpango wa dola bilioni 1.1 ulioidhinishwa na mawaziri wa mambo ya nje siku ya Jumatatu wa kuipatia Ukraine jumla ya makombora milioni 1 hapo mwakani. Kyiv imesema inahitaji silaha hizo kwa haraka mno ili kukabiliana na uvamizi wa majeshi ya Urusi.

Alipokuwa akiwasili katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema:

"Jambo muhimu ni kuhakikisha amani thabiti na ya kudumu. Hiyo inamaanisha kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kuheshimu mipaka ya nchi nyingine, jambo linalokiukwa na Urusi huko Ukraine. Na bila shaka ni Waukraine wenyewe watakao weka masharti ya kuanza kwa mazungumzo ya amani na ambayo kwa kawaida yatalazimika kudumu kwa muda kadhaa."

Soma pia: Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya waanza Brussels

Yaliyoshuhudiwa pia katika mkutano huo ni mizozo kati ya Ufaransa na Ujerumani kuhusu nafasi inayostahili kwa nishati ya nyuklia katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na marufuku ya matumizi ya gari zinazotumia mafuta ifikapo mwaka 2035.

Mkutano kati ya Ufaransa na Ujerumani umepangwa kufanyika kesho asubuhi huku uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa barani Ulaya ukiwa umedorora kwa miezi kadhaa. Hadi kesho Ijumaa, viongozi hao wa Umoja wa Ulaya watajadili pia mifumo ya kuimarisha ushindani wa kiuchumi wa bara hilo.