IDHAA YA KISWAHILI | DW
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari

Habari za Ulimwengu | 19.04.2019 | 03:00

Trump alijaribu kuudhibiti uchunguzi wa Mueller

Sehemu ya ripoti ya Mchunguzi Maalum Robert Mueller nchini Marekani juu ya kujihusisha kwa Urusi kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 inaonesha kuwa Rais Donald Trump alitaka kuudhibiti uchunguzi huo na kulazimisha kuondolewa kwa Mueller mwaka 2017. Ripoti hiyo iliyotolewa jana inachambua matukio 10 yanayoashiria uzuwiaji wa haki kutendeka, ikiwemo hatua ya Trump kumfuta kazi mkurugenzi wa shirika la ujasusi, James Comey. Hata hivyo, mchunguzi huyo maalum anasema hakuweza kuthibitisha moja kwa moja endapo Trump alitenda uhalifu wa kuzuwia haki kutendeka. Mawakili wa Trump wameiita ripoti hiyo kuwa ushindi wa wazi kwa rais huyo. Hata hivyo, mkuu wa chama cha Democrat kwenye kamati ya sheria ya bunge, Jerrold Nadler, amesema kuwa Mueller amewasafishia njia kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kibunge dhidi ya Trump. Tayari bunge hilo limewaita kwa mahojiano mwanasheria mkuu na Mueller mnamo mwezi ujao.

Mahakama ya juu ya Uganda yamsafishia njia Museveni

Mahakama ya Juu nchini Uganda imekubaliana na uamuzi wa kuondosha ukomo wa umri wa mgombea urais, na hivyo kumsafishia njia Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 74 kuwania kwa muhula mwengine wa sita. Mahakama hiyo ilitupilia mbali zuio la wapinzani, ambao waliukatia rufaa uamuzi wa mahakama ya katiba ulioridhia mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na bunge. Katika uamuzi wake hapo jana, Jaji Mkuu Bart Katureebe alitangaza kwamba rufaa hiyo imeshindwa, baada ya majaji wanne kuitupilia mbali dhidi ya watatu walioiunga mkono. Mwezi Disemba 2017, Rais Museveni - ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 - aliusaini muswaada wa sheria kuondosha ukomo wa umri kwa wagombea urais, na hivyo kuashiria kuwa angeliwania tena mwaka 2021. Uamuzi huo ulizusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa wapinzani, ambao wanamtuhumu kiongozi huyo kutaka kuwa rais wa maisha.

Serikali ya Mali yajiuzulu

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali amekubali ombi la kujiuzulu kwa waziri mkuu na baraza lake zima la mawaziri. Soumeylou Boubeye Maiga alichukuwa hatua hiyo hapo jana, kufuatia wiki mbili za maandamano ya umma dhidi ya mauaji ya kiholela katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Maandamano hayo yalichochewa na mauaji ya wachungaji 160 wa jamii ya Fulani, ambayo yanashukiwa kufanywa na watu wa jamii ya Dogon, wanaoishi kwa kilimo na uwindaji. Mauaji hayo yaliitikisa Mali, ambayo katika miezi ya karibuni imeshuhudia mauaji mengine kadhaa, yakiwemo yale ya wanajeshi 23 walioshambuliwa kwenye kituo chao. Juzi Jumatano, bunge lilijadili uwezakano wa kura ya kutokuwa na imani na serikali kutokana na mauaji hayo na pia kushindwa kuwanyang'anya silaha na kuwazuwia wanamgambo wa itikadi kali. Umoja wa Mataifa una zaidi ya wanajeshi 16,000 nchini Mali, vikiwemo vikosi kutoka Ufaransa na Ujerumani.

Ufaransa yakanusha tuhuma za Libya

Ufaransa imekanusha tuhuma kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Libya kwamba imekuwa ikimuunga mkono mbabe wa kivita, Jenerali Khalifa Haftar, ambaye jeshi lake limeanzisha operesheni ya kuutwaa mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli. Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana inasema imesitisha mahusiano yote kati yake na upande wa Ufaransa kutokana na msimamo wa serikali ya Ufaransa kumuunga mkono inayemuita kuwa ni mhalifu Haftar. Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imeziita tuhuma hizo kuwa za kuudhi na za uzushi. Taarifa ya ikulu ya Ufaransa imesema kuwa nchi hiyo inaiunga mkono serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa chini ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj na pia "juhudi za upatanishi za Umoja wa Mataifa kuelekea suluhisho la kisiasa linalojumuisha pande zote." Ufaransa imesaidia kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Libya vilivyo chini ya serikali mjini Tripoli, wakiwemo polisi na walinzi wa Waziri Mkuu Sarraj.

Mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita afa Ujerumani

Kiongozi wa zamani wa waasi wa Rwanda amefariki dunia akingojea kusomwa upya kwa kesi yake nchini Ujerumani, baada ya kutiwa hatiani kwa uhalifu wa kivita uliotendeka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo takribani muongo mmoja uliopita. Ignace Murwa-na-shyaka, mwenye umri wa miaka 55, alikuwa rais wa kundi la FDLR baina ya mwaka 2008 na 2009, wakati waasi hao wakiendesha mapambano yao mashariki mwa Kongo. Mwaka 2015, kiongozi huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13 jela na mahakama ya mjini Stuttgart kwa makosa ya kuongoza kundi la kigaidi na makosa mengine manne ya uhalifu wa kivita. Hata hivyo, hukumu hiyo ilitenguliwa mwaka jana kutokana na makosa ya kisheria na kesi yake ilikuwa imepangwa kuendeshwa tena, huku akisalia kizuizini. Mahakama hiyo ilisema kuwa afya ya Murwa-na-shyaka ilibadilika ghafla tarehe 11 mwezi huu, na siku chache baadaye alikufa akiwa hospitalini.

'Simba' mkubwa kabisa agunduliwa Kenya

Utafiti mpya umebaini kwamba mmoja wa wanyama wakubwa kabisa anayekula nyama aliishi nchini Kenya yapata miaka milioni 23 iliyopita. Mnyama huyo aliyepewa jina la "Simba Mkubwa Kutoka Afrika", alitambuliwa kutokana na meno na mabaki ya mifupa iliyozikuliwa magharibi mwa Kenya miongo kadhaa iliyopita. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Ohio nchini Marekani wanaamini mnyama huyo alikuwa mkubwa zaidi kuliko simba wa sasa na hata kuliko dubu. Ushahidi wa mabaki hayo unaonesha kuwa huenda simba huyo aliishi kwa kuwinda na kuwala wanyama wa jamii ya tembo na viboko ambao walikuwapo kwenye eneo hilo katika zama hizo.

Jammeh alifanya ufisadi wa dola bilioni moja

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh, anatuhumiwa kusimamia wizi wa takribani dola bilioni moja kabla hajakimbilia uhamishoni mwaka 2017. Shirika la Uchunguzi wa Uhalifu wa Kupangwa na Ufisadi lenye makao yake nchini Marekani linasema limepitia maelfu ya nyaraka zilizovujishwa ambazo zinaelezea namna fedha za umma zilivyoibiwa ndani ya kipindi cha miaka 22 ya utawala wa Jammeh. Waandishi wa habari za uchunguzi wanasema fedha hizo zilichukuliwa kutoka vyanzo kadhaa, ikiwemo benki kuu na mashirika ya mawasiliano yanayomilikiwa na serikali, na kwamba zilitumika kununulia majengo na magari ya kifakhari. Mnamo mwaka 2017, utawala wa Trump nchini Marekani ulimuwekea Jammeh vikwazo kutokana na historia ya muda mrefu ya uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na ufisadi. Rais huyo wa zamani anaishi uhamishoni nchini Guinea ya Ikweta.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Tazama vidio 01:18
Matangazo