1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kuharakisha kuipatia Ukraine silaha

Mohammed Khelef
23 Machi 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana hivi leo mjini Brussels na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kujadiliana na pia kupitisha mpango wa kuharakisha msaada wa makombora kwa Kyiv.

https://p.dw.com/p/4P6xz
Belgien EU-Verteidigungsaußenminister
Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya walitazamiwa siku ya Alkhamis (23 Machi) kuidhinisha makubaliano ya risasi milioni moja za makombora nchini Ukraine ndani ya kipindi cha miezi 12 kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na vikosi vya Urusi. 

Mpango huo wa uharakishaji utumwaji silaha ulipendekezwa na mkutano wa mawaziri wao wa mambo ya kigeni na wa ulinzi mwanzoni mwa wiki, na mkutano wa leo wa kilele mjini Brussels ulikuwa na jukumu tu la kuupa baraka za kisiasa. 

Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo, Josep Borrell, alisema amepata idhini ya pendekezo lake la kutoa euro bilioni moja kuyashajiisha mataifa wanachama kutoa makombora kwenye maghala yao na oda nyengine yoyote mpya itakayotolewa.

Soma zaidi: Putin asema yuko tayari kuujadili mpango wa China kuhusu Ukraine
Ulaya kuipatia Ukraine risasi milioni 1

Euro nyengine bilioni moja zingelitumika kuharakisha oda mpya na kuyawezesha mataifa wanachama kushirikiana kwenye manunuzi kupitia Wakala wa Ulinzi wa Ulaya ama kwa makundi ya nchi angalau tatu tatu.

Belgien EU-Verteidigungsaußenminister
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell (kushoto), akiwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ubelgiji, Hadja Lahbib, kwenye mkutano wa kujadili uharakishaji utumwaji silaha Ukraine.Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Kwenye mkutano huo wa siku mbili, viongozi wa Umoja wa Ulaya walitazamiwa kuungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kwa ajili ya uzinduzi hivi leo, na baadaye Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kuhutubia kwa njia ya video.

Kumkamata Putin ni kutangaza vita - Medvedev

Kwa upande mwengine, naibu mwenyekiti wa baraza la usalama la Urusi, Dmitry Medvedev, alisema jaribio la kumkamata Rais Vladimir Putin nje ya nchi baada ya waraka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) lingelichukuliwa na Moscow kwamba ni tangazo la vita.

Medvedev, aliyekuwa rais wa Urusi baina ya mwaka 2008 na 2012, alisema kwenye mahojiano yaliyorushwa Jumatano jioni (Machi 22) kwamba silaha za Urusi zingeilipiga nchi yoyote ambayo ingelimkamata Putin.

Russland | Dmitri Medwedew
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, Dmitry Medvedev.Picha: Alexei Maishev/TASS/IMAGO

 

Soma zaidi:Rais wa zamani wa Urusi aionya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuhusu vita vya nyuklia

"Kwa hakika, hilo kamwe halitatokea, lakini tukisie kwamba limetokea. Rais wa taifa lenye nguvu za nyuklia, mathalani., anakuja Ujerumani na anakamatwa. Hicho ni nini? Ni tangazo la vita dhidi ya Urusi. Kwenye hali hiyo, nguvu zetu zote zitaelekea Bundestag, ofisi ya Kansela, na kadhalika. Anajuwa kuwa hilo litakuwa tangazo la vita? Au alishindwa kupima vizuri?" Alisema.

Wiki iliyopita, ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, ilitangaza waranti ya kumkamata Putin kwa tuhuma za kuwasafirisha watoto wa Ukraine.

Mahakama hiyo pia ilitowa waranti kwa kukamatwa Maria Lvova-Belova, rais wa kamisheni wa haki za watoto ya Urusi.

Siku ya Jumanne (Machi 21), Urusi nayo ikatangaza kuanza uchunguzi wa uhalifu dhidi ya mwendesha mashitaka mkuu wa ICC, Karim Khan, na majaji wengine kadhaa wa mahakama hiyo, ikisema uamuzi wao ulikuwa kinyume na sheria.
 

Vyanzo: Reuters, AFP