1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na viongozi 20 wazindua "ukurasa mpya wa amani" Gaza

14 Oktoba 2025

Viongozi zaidi ya 20 wamekutana mjini Sharm el-Sheikh kujadili mustakabali wa Gaza. Rais Trump amesema sasa ni wakati wa kuijenga upya Gaza isiyo na silaha, huku Umoja wa Mataifa ukisifu hatua hiyo ya kihistoria.

https://p.dw.com/p/51vhE
Misri 2025 | Mkutano wa kilele wa Gaza na Abdel-Fattah al-Sisi na Donald Trump
Rais wa Misri alimsifu Trump kama kiongozi pekee anaeweza kuleta amani Mashariki ya KatiPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mkutano wa kimataifa wa amani uliofanyika mjini Sharm el-Sheikh, Misri, umefungua ukurasa mpya katika juhudi za kurejesha utulivu Gaza, baada ya miaka miwili ya mapigano yaliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 67,000. Tukio hilo limefuatia mabadilishano ya mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina yaliyotekelezwa chini ya makubaliano mapya ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump aliitaja Jumatatu hiyo kuwa "siku kubwa ya kihistoria kwa Mashariki ya Kati,” wakati akisaini tamko la pamoja la amani na viongozi wa Misri, Qatar na Uturuki. Alisema hatua hiyo inaleta "mwisho wa mateso na damu kumwagika,” na kwamba sasa kazi kubwa ni kuijenga upya Gaza kwa amani na utulivu.

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Trump alisisitiza kuwa ujenzi wa Gaza unahitaji eneo hilo liwe bila silaha na lisimamiwe na polisi wa kiraia watakao hakikisha usalama wa raia. Alisema makubaliano hayo ni "urithi wa pamoja” wa dunia, na akatoa wito kwa mataifa mengine kusaidia kurejesha amani ya kudumu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi zaidi ya ishirini, akiwemo Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, na viongozi wa Ulaya wakiwemo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Viongozi hao walitia saini tamko la kuunga mkono juhudi za amani na kujitolea “kudumisha urithi huu wa kihistoria.”

Misri 2025 | Donald Trump katika mkutano wa kilele wa Gaza unaoongozwa na al-Sisi
Rais wa Marekani, Donald Trump, akionyesha tamko kuhusu vita vya Gaza katika mkutano wa kilele wa Gaza ulioongozwa na Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Rais Trump pia alikutana kwa muda mrefu na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ambaye ameonyesha nia ya kushiriki katika utawala wa baadaye wa Gaza licha ya upinzani wa Israel. Hatua hiyo imeibua matumaini ya ushirikiano mpya wa kisiasa katika ukanda huo.

Mvutano wa kidiplomasia na uwepo wa Netanyahu

Hata hivyo, kulikuwa na mivutano ya kidiplomasia iliyoonekana nyuma ya pazia. Chanzo cha kidiplomasia kiliiambia AFP kwamba baadhi ya viongozi wa Kiarabu, Rais Erdoğan na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez, walitishia kususia mkutano huo endapo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu angehudhuria. Hatimaye, Netanyahu alifuta ziara yake dakika za mwisho, akitaja likizo ya kidini kama sababu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya diplomasia, ndege ya Erdoğan ilichelewesha kutua hadi ikathibitishwa rasmi kuwa Netanyahu hatakuwapo kwenye mkutano huo — ishara kwamba bado kuna mitazamo mikali kuhusu nafasi ya Israel katika mchakato wa amani wa Gaza.

Umoja wa Mataifa, kupitia Katibu Mkuu Antonio Guterres, ulipongeza makubaliano hayo. Kupitia msemaji wake Farhan Haq, alisema makubaliano hayo "yanatoa tumaini jipya kwa watu wa Gaza na Israel kuona mwanga baada ya miezi ya uharibifu.”

Farhan Haq alisema: "Katibu Mkuu amekaribisha utekelezaji unaoendelea wa makubaliano ya kusitisha vita Gaza kwa msingi wa pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump. Ameyapongeza mataifa ya Qatar, Misri, Marekani na Uturuki kwa juhudi zao za upatanishi na kulitambua jukumu muhimu la Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa usalama na utu.”

Umoja wa Mataifa pia uliripoti kuwa mashirika yake yameanza kufikia maeneo ambayo kwa miezi kadhaa yalikuwa hayafikiki, yakitoa chakula, dawa na misaada ya dharura. Licha ya hali hiyo, maafisa wa UN wameonya kwamba changamoto ya kibinadamu bado ni kubwa.

Misri Sharm el-Sheikh 2025 | Mkutano wa kilele wa amani kuhusu Gaza ukihusisha viongozi wa kimataifa
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Emir wa Qatar, wakirishi kikao mjini Sharm El Sheikh, Misri, Oktoba 13, 2025, kabla ya kushiriki katika Mkutano wa Amani.Picha: Eliot Blondet/ABACA/picture alliance

Furaha na machozi baada ya mabadilishano ya mateka

Kwa upande wa Israel, jeshi lilithibitisha kuwa limepokea mateka wote 20 waliokuwa bado hai, hatua iliyoleta hisia kali za furaha na machozi miongoni mwa wananchi waliokusanyika mjini Tel Aviv kushuhudia tukio hilo kupitia runinga za umma.

Wakati huo huo, katika mji wa Khan Younis na maeneo mengine ya Gaza, maelfu ya watu walijitokeza kuwapokea wafungwa wa Kipalestina waliokuwa wakirejea nyumbani. Malori kadhaa yaliyowabeba wafungwa karibu 2,000 yalipokewa kwa shangwe, huku baadhi ya watu wakibeba bendera na picha za ndugu zao waliouawa vitani.

Rais Trump alisema kuwa makubaliano hayo yanachukuliwa kama "hatua ya kwanza ya amani ya kikanda”, akiongeza kwamba yatachochea maridhiano mapya Mashariki ya Kati, ikiwemo uwezekano wa makubaliano kati ya Israel na Iran — jambo ambalo aliliita "ndoto ya amani ya kweli.”

Katika hotuba yake mbele ya Bunge la Israel, Knesset, Trump alisema: "Israel, kwa msaada wetu, imepata yote kwa njia ya kivita. Sasa ni wakati wa kuyatafsiri mafanikio haya kuwa amani na ustawi wa kudumu kwa Mashariki ya Kati nzima.”

Hata hivyo, wachambuzi wanasema changamoto bado ni nyingi. Miongoni mwa masuala mazito ni nani ataongoza Gaza baada ya vita, iwapo Hamas itakubali kuachia silaha, na ni vipi usalama wa muda mrefu utawekwa bila kurudi kwenye ghasia.

Israel Jerusalem 2025 | Mbunge wa Knesset anaondolewa bungeni baada ya kufanya maandamano.
Mjumbe wa bunge la Israel, Knesset, akiondolewa na walinzi baada ya kuonyesha ujumbe wa upinzani wakati wa hotuba ya rais Donald Trump, uliosemeka: Itambue Palestina.Picha: Kenny Holston/REUTERS

Mustakabali wa Gaza na mipango ya ujenzi mpya

Kwa mujibu wa mpango wa Marekani, Gaza itasimamiwa kwa muda na mamlaka ya kimataifa itakayoshirikiana na wataalamu wa Kipalestina katika kuendesha shughuli za kila siku. Pia kutaundwa jeshi la usalama la Kiarabu na polisi wa Kipalestina kuhakikisha utulivu, huku vikosi vya Israel vikiondoka hatua kwa hatua.

Mpango huo pia unataja uwezekano wa kuundwa kwa taifa la Palestina, lakini suala hilo limeendelea kugawanya viongozi, hususan Waziri Mkuu Netanyahu, ambaye amekuwa akipinga wazo hilo kwa muda mrefu.

Kwa upande mwingine, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi alisema mazungumzo ya Sharm el-Sheikh yalilenga "kuijenga Gaza upya kwa misingi ya amani, usalama na haki.” Alisema mafanikio ya mpango huo yatategemea "uaminifu na utekelezaji wa vitendo” kutoka pande zote.

Mkutano huo wa Sharm el-Sheikh umeacha matumaini makubwa lakini pia maswali mengi. Wengi wanajiuliza kama makubaliano hayo yatadumu, hasa ikizingatiwa historia ndefu ya ukosefu wa imani kati ya Israel na Wapalestina.

Kwa sasa, misaada ya kibinadamu inaendelea kumiminika Gaza, huku viongozi wa dunia wakisisitiza haja ya kutunza amani hii changa. Kama alivyoeleza Trump, "anga sasa ni tulivu, milio ya bunduki imesimama, na jua linachomoza katika ardhi takatifu ambayo hatimaye imepumua kwa amani.”

Rais Trump awasili Israel kulihutubia bunge la Knesset

Chanzo: APE, RTRE, AFP, DPA