1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Polisi yarusha mabomu ya machozi kudhibiti maandamano Kenya

Shisia Wasilwa
25 Juni 2026

Polisi warusha mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji katika maeneo mbalimbali mjini Nairobi huku makundi yanayoongozwa na vijana yakikumbuka miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z.

https://p.dw.com/p/5G4R9
Kenia 2025 | Jahrestag der Anti-Regierungsproteste | Proteste in Nairobi
Polisi yatumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa katika kumbukumbu ya miaka miwili tangu maandamano makubwa ya kuipinga serikali, yaliyoongozwa na Gen Z kufanyika nchini Kenya Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Watu kadhaa wametiwa nguvuni kufuatia maandamano hayo.

Mawingu mazito ya moshi yalitanda angani huku umati wa watu ukikimbia kujinusuru, wengi wao wakifunika nyuso zao kutokana na harufu kali na madhara ya gesi hiyo.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozidhidi ya makumi ya vijana na wanaharakati waliokuwa wakitaka kuelekea kwenye majengo ya bunge la Taifa kuweka shada za maua kuwakumbuka vijana waliouawa miaka miwili iliyopita. Vijana hao walilazimika kutawanyika kuelekea mzunguko mkubwa wa Globe.

Makabiliano kama hayo yalizuka karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi na kando ya Barabara ya University Way, ambapo wanafunzi na waandamanaji wengine walikabiliana na polisi wa kukabiliana na ghasia waliokuwa wakijaribu kuwazuia kuingia CBD. Jacinta Anyango alimpoteza mwanaye leo aliungana na waandamanaji kwa kuwakumbuka wahanaga hao.

Mapinduzi ya Gen Z barani Afrika: Nini kinafuata 2026?

"Sisi tunataka haki Rais, nataka kuona serikali iliyoua mtoto wangu, angalau nitamsamhea. Leo hatutaki tear gas, bwana Rais.”

Viongozi wa Upinzani, wanaharakati na jamaa za waathiriwa hawakuruhusiwa kuweka shada za maua kwenye bunge ambapo tukio la mauaji lilitokea kwani eneo hilo lililikuwa limezingirwa na nyaya huku polisi wakiweka ulinzi mkali.

Matukio haya yanajiri wakati Wakenya wanakumbuka maandamano ya Juni 25, 2024 dhidi ya Mswada tata wa Fedha, yaliyogeuka kuwa machafuko ya kitaifa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 120 kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Maandamano ya leo kwa kiasi kikubwa yalielezwa kuwa ya amani, yakilenga kuwakumbuka waliopoteza maisha huku yakitaka haki, uwajibikaji kwa vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kufanywa na polisi, pamoja na kukomeshwa kwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela.

Kenia 2025 | Jahrestag der Anti-Regierungsproteste | Proteste in Nairobi
Muandamanaji katika kumbukum buku ya miaka miwili ya maandamano ya Gen Z kenya yaliyosababisha mauaji ya watu zaidi ya 50Picha: John Muchucha/REUTERS

"Niliamka Kwenda kazini asubuhi, kulikuwa na magari machache lakini sasa nimeshindwa kurudi nyumbani sababu hakuna magari.”

"Mimi nimelazimika kutembea mguu kutoka Ruiru hadi jijini na sasa nalazimika kurudi tena.”

Polisi walitetea matumizi ya nguvu na kufungwa kwa baadhi ya barabara wakisema ni hatua muhimu za kudumisha usalama na utulivu. Watu kadhaa waliripotiwa kukamatwa sambamba na matumizi ya mabomu ya machozi.

Baadhi ya viongozi wa upinzani walidaiwa kujikuta katikati ya vurugu hizo, huku video kadhaa zikionyesha wakipita katika mitaa iliyofunikwa na moshi wa mabomu ya machozi. Kufikia adhuhuri, biashara nyingi Nairobizilikuwa bado zimefungwa, na hali iliendelea kuwa ya taharuki huku makabiliano ya hapa na pale kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama yakiendelea.

Mjini Kisumu, shughuli za kawaida za kibiashara ziliendelea katika jiji hilo la kando ya Ziwa Victoria, huku huduma za usafiri wa umma zikiendelea bila usumbufu mkubwa licha ya kuongezeka kwa doria za polisi katika maeneo mbalimbali.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi