Tetemeko la ardhi lawaua watu zaidi ya watu 100 Venezuela
25 Juni 2026
Kumeripotiwa mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi nchini humo na tayari timu za uokoaji zimekuwa zikiendelea na juhudi za kuwaokoa manusura wa mkasa huo.
Mitetemeko hiyo yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter iliyotokea jana jioni imeripotiwa kuwa miongoni mwa mikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha zaidi ya karne moja, na iliyatikisa maeneo mengi ya kanda hiyo.
Uwanja mkuu wa ndege wa Venezuela uliharibiwa pakubwa huku mamlaka zikilazimika kuufunga wakati athari za mitetemeko hiyo zikisababisha uhamishaji wa watu kutoka majengo katika maeneo ya mbali kama msitu wa Amazon nchini Brazil, takriban kilomita 1,700 kutoka mji mkuu wa Caracas.
Picha zilizopeperushwa na televisheni za nchini humo zilionyesha waokoaji wakitumia vifaa maalum kuvunja vifusi katika juhudi za kuwaokoa waliokwama ndani.
Wakazi wa Caracas walionekana wakikimbilia mitaanikutokana na hofu wakati wa mitetemeko hiyo, na baadaye walionekana wakitafuta ndugu na jamaa zao kati ya mabaki ya majengo yaliyoanguka na nguzo za umeme zilizoporomoka.
Tamko la Umoja wa Mataifa
Kaimu rais Delcy Rodríguez alisema serikali imezipeleka timu za uokoaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwenda La Guaira, ambalo liko kaskazini mwa Caracas. Rais huyo alisema kwamba juhudi zinaendelea kufanikisha zoezi hilo hatari.
Serikali imeeleza kuwa makumi ya majengo yameharibiwa vibaya katika eneo hilo, na operesheni kubwa za uokoaji zinaendelea ili kuokoa maisha ya watu. Video zilizosambazwa mtandaoni pia zilionyesha majeruhi wakipatiwa matibabu nje ya hospitali, baadhi wakiwa chini na wengine wakiwa kwenye vitanda vilivyowekwa nje.
Umoja wa Mataifa kupitia kwa naibu katibu mkuu wa shirika hilo anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura,Tom Fletcher ,umeitaka serikali kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi na mawasiliano ili kusaidia juhudi za uokoaji na kulinda maisha ya wananchi.
Hali ya dharura yatangaza Venezuela
Serikali ya Venezuella pia,imetangaza hali ya dharura na kutenga dola milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali na nyumba zilizoharibiwa. Mataifa mbalimbali yameanza kutoa msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutuma timu za uokoaji, vifaa vya matibabu na rasilimali nyingine muhimu.
Viongozi wa dunia wanaendelea kutuma salamu za pole na mshikamano kwa wananchi wa Venezuela, huku operesheni za uokoaji zikiendelea katika juhudi za kuokoa maisha na kuwasaidia waathirika kurejea katika hali ya kawaida.
Ingawa Venezuela iko karibu na mikondo ya kijiolojia, mitetemeko yenye nguvu kama hii si ya kawaida sana ikilinganishwa na maeneo mengine ya Amerika ya Kusini. Serikali imewaomba wafanyabiashara kusaidia kwa kutoa vifaa maalum ili kurahisisha shughuli za uokoaji, huku timu za kimataifa zikitarajiwa kuwasili kusaidia.
Katika mji wa Caracas, shuguli za kawaida zilisambaratika kwa muda huku watu wakikaa nje kwa saa kadhaa wakihofia mitetemeko ya baadaye. Mamia yao walikesha katika maeneo ya wazi kama bustani na viwanja vya magari. Mamlaka zilikuwa zimewataka wananchi kutoingia kwenye majengo yaliyoharibika kwa kuhofia kuporomoka zaidi.
Miundombinu muhimu pia iliathirika ikiwemo umeme na huduma za simu. Huduma ya usafiri wa treni ya chini ya ardhi ilisimamishwa, na usambazaji wa gesi asilia kusitishwa kwa muda. Shule zimefungwa kwa siku kadhaa, huku baadhi ya majengo yakitumika kama makazi ya muda na vituo vya misaada.