Trump: Huu ni mwanzo wa enzi mpya ya Mashariki ya Kati
13 Oktoba 2025
Rais Trump amewaeleza wabunge wa Israel leo Jumatatu kwamba nchi yao haina tena malengo ya kutimiza katika medani za vita na lazima ifanye kazi kuelekea upatikanaji wa amani katika kanda ya Mashariki ya Kati baada ya miaka miwili ya vita dhidi ya Hamas na mapigano na Hezbollah na Iran.
Ingawa makubaliano ya Marekani ya usitishaji vita kati ya Israel na Hamas yanasalia kuwa tete, lakini Trump anadhamiria kutumia fursa hiyo ili kufanikisha amani ya kikanda. Trump amesema hilo litakumbukwa na vizazi kama "wakati ambao kila kitu kilianza kubadilika", alisema hayo katika bunge la Knesset alikopokelewa kama shujaa.
"Huu sio tu mwisho wa vita, huu ni mwisho wa enzi ya vitisho na kifo na mwanzo wa enzi ya imani na matumaini, ya Mungu. Ni mwanzo wa mapatano makubwa na maelewano ya kudumu kwa Israel na mataifa yote ya kanda ambayo hivi karibuni ltakuwa eneo zuri sana, ninaamini hivyo kwa nguvu sana. Huu ni mwanzo mpya wa kihistoria wa Mashariki ya Kati mpya," alisema Trump.
Katika hali isiyotarajiwa, Trump pia alimwomba rais wa Israel amsamehe Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye alimuelezea kama "mmoja wa viongozi wakubwa" wa kivita. Amemsifu Netanyahu kuwa "mtu asiye mwepesi kushughulika naye, lakini hilo ndilo linamfanya kuwa thabiti."
Itakumbukwa kuwa Netanyahu anakabiliwa na mashitaka ya rushwa, licha ya kwamba usikililizwaji wa kesi dhidi yake umekuwa ukisogezwa mbele mara kadhaa wakati wa mzozo na Hamas. Trump ameitolea wito Israel kuvipa kisogo vita hivyo vya nyuma akisema "nchi imeshinda vyote kwa nguvu ya silaha".
"Mmeshinda. Namaanisha mmeshinda. Huu ni wakati ambao mnapaswa kutafsiri ushindi huu wote dhidi ya magaidi katika uwanja wa vita kuwa tunzo ya amani na mustakabali wa kanda nzima ya Mashariki ya Kati".
Katika hotuba yake, kiongozi huyo wa Marekani ameahidi kusaidia kuijenga upya Gaza, ambayo imeharibiwa vibaya na kuwarai Wapalestina "kuachana na mwenendo wa vita na ghasia".
"Baada ya maumivu makubwa na kifo na shida, sasa ni wakati wajikite katika kuwajenga watu wao badala ya kujaribu kuibomoa Israel".
Aidha pia Trump alitumia hotuba hiyo kutuma ujumbe kwa Iran ambayo aliishambulia wakati wa vita vya siku chache na Israel mapema mwaka huu, akisema "mkono wa ushirikiano na urafiki uko wazi", akiongeza kuwa kila mmoja anataka kuishi kwa amani na hakuna anayetaka kuishi kwa vitisho.
Wakati wa hotuba yake, mbunge wa mrengo wa kushoto aliondolewa bungeni baada ya kujaribu kukatiza hotuba ya Trump.
Alichokisema Netanyahu bungeni
Kabla ya Trump kuhutubia, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye alihutubia bunge hilo na kutoa hakikisho la kuunga mkono makubaliano na Hamas ya kumaliza vita vya Gaza huku akimsifu Trump kwa kufanikisha makubaliano hayo. Netanyahu amesema anajitolea kwa amani hiyo na kuongeza kuwa maadui wa Israel sasa "wanaelewa kuwa kuishambulia Israeli mnamo Oktoba 7 lilikuwa kosa kubwa". Netanyahu hatosafiri kuelekea Misri kuhudhuria mkutano wa kilele wa amani ya Gaza. Netanyahu anatazamiwa kumtunuku Trump nishani ya juu sana ya Israel, akiwa ni raia wa kwanza wa kigeni kutunukiwa.
Wafungwa wa Kipalestina waachiwa
Na Wapalestina waliojawa na furaha wamewapokea wafungwa walioachiliwa huru na Israel wakati walipowasili kwa mabasi katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza leo Jumatatu. Wafungwa hao wameachiwa baada yaHamas kuwaachia mateka wote 20 hai waliochukuliwa wakati wa shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023. Maelfu ya watu walikusanyika ndani na viunga vya karibu na hospitali ya Nasser huko Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza kuwapokea jamaa zao.