1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Je, utawala wa Iran utaanguka? Dalili zinaibua maswali

14 Januari 2026

Utawala wa Iran unaendelea kukabiliwa na shinikizo la ndani na nje lakini kwa mujibu wa wachambuzi wa eneo la Mashariki ya Kati, hakuna dalili za moja kwa moja zinazoashiria kuanguka kwa mfumo huo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/56oBK
Großbritannien London 2026 | Demonstranten mit brennenden Bildern Chameneis und Reza Pahlavis
Picha: Amanda Rose/Avalon/Photoshot/picture alliance

Akizungumza na DW, Daniel Gerlach amesema ingawa katika maandamano imejitokeza tena bendera ya Simba na Jua iliyotumika kabla ya mapinduzi ya mwaka 1979 nchini Iran bado hali halisi haielezei umoja wa upande wa wapinzani wanaoishi nje ya nchi.

Ameelezea kwamba kuna takriban Wairan milioni tano wanaoishi nje ya nchi hiyo, ambao wengi wanaipinga Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu za kisiasa, kijamii, au kiuchumi.

Ndani ya kundi hilo, Wairan wanaounga mkono kurudishwa kwa utawala wa Shah wana sauti na wanaonekana kuwa wamejipanga vizuri ingawa kundi hilo lina wafuasi wachache hasa ndani ya Iran.

Gerlach amebainisha kuwa hata tabaka la wafanyabiashara wa jadi ambao kihistoria wamekuwa msingi wa nguvu kwa utawala wa Iran, wamechangia katika kuchochea wimbi la sasa la maandamano.

Mwitikio wa serikali dhidi ya maandamano

Amesema sura ya mwanamfalme Reza Pahlavi inayojitokeza zaidi katika miezi ya hivi karibuni, kwa sehemu ni kutokana na juhudi kubwa za ujumbe na kuhamasisha ambao harakati zake zinapokelewa vizuri.

Gerlach amesisitiza kwamba uungwaji mkono wa kifalme ndani ya Iran ni mdogo. Watu ndani ya Iran wamesema halitakuwa wazo zuri kurudisha utawala wa kifalme, kutokana na uhusiano wa kifalme na ukoloni, akitoa mfano wa kihistoria wa Uingereza kumwondoa madarakani Reza Shah na kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh kwa msaada wa CIA.

Mtaalamu wa Mashariki ya Kati Daniel Gerlach amesema Wairani wengi, bado wanaamini kwamba kupanda kwa madaraka ya Ayatollah Khamenei pia kulipangwa na wahusika wa kigeni.

Ameongeza, kuwa ni wazo baya kwa Wairan wengi kuwa na mtu mwingine aliye uhamishoni kurudi na kuchukua madaraka nchini humo.

Marekani yaanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran

Hata hivyo, amekiri kwamba ujumbe wa sasa wa Pahlavi unaosisitiza huduma kwa wairan kuliko mamlaka unaweza kuwagusa hata wasiowaunga mkono watawala wa kifalme.

Alipoulizwa kama maandamano hayo yamesababisha nyufa katika misingi ya utawala wa Iran, Gerlach amesema hayo bado hayajatokea.

Gerlach ameieleza DW kwamba ingawa kuna dalili za matukio yasiyo ya kawaida kama vile maandamano katika ngome muhimu ya utawala ya Mashhad yanayotokea karibu na kambi ya Walinzi wa Mapinduzi na bila kutokea hatua zozote za ukandamizaji mara moja hakuna ushahidi wa uwezekano wa kuvunjika nguzo kuu za utawala.

Utawala wa Iran unategemea nguzo tano au sita muhimu miongoni mwao ni Huduma ya ujasusi, Walinzi wa Mapinduzi, viongozi wa dini na mahakama  na mpaka sasa hakuna hata moja kati ya hizi inayoonekana kudhoofika au kulegeza msimamo wa kuuunga mkono Utawala wa Iran.