1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inataka kufikia malengo gani nchini Lebanon?

10 Aprili 2026

Jeshi la Israel limekuwa likiendesha mashambulizi ya anga dhidi ya Lebanon kujibu mashambulizi makubwa ya maroketi na droni kwa lengo la kuiunga mkono Iran. Lakini je Israel inataka kufikia malengo gani Lebanon?

https://p.dw.com/p/5BymQ
Israel Jerusalem 2024 | Israel Katz
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz Picha: Menahem Kahana/AFP/Getty Images

Kwa hakika mashambulizi ya hivi sasa ya kijeshi yanayofanywa na Israel ambayo yamesababisha vifo vingi ni sehemu ya mgogoro mkubwa wa kikanda. Lakini Israel imekataa kutazama vita vyake ndani ya Lebanon kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji vita kati ya Marekani na Iran, na badala yake imefanya kinyume kabisa. Imeishambulia kwa nguvu kubwa Lebanon,ikiwemo mji mkuu Beirut  mnamo siku ya Jumatano. Wizara ya afya ya nchi hiyo imesema zaidi ya watu 180 wameuwawa wengi wakiwa ni raia na karibu wengine 900 wamejeruhiwa.

Kwa jicho la Israel msingi wake wa  kushambulia nchini Lebanon sio tu unahusu kujibu mashambulizi ya wanamgambo wa Hezbollah,bali Israel  imekuwa na malengo ya muda mrefu ya kimkakati ambayo inapania kuyatimiza, na malengo hayo ni kulidhoofisha na kulimaliza kabisa kundi la Hezbollah, kukamata eneo la mpaka la Kaskazini  na kuzuia ushawishi wa Iran katika kanda hiyo.

Hata hivyo sio tu kwenye mataifa ya kiarabu lakini hata ndani ya Lebanon kwenyewe umekuwepo wasiwasi wa muda mrefu kwamba Israel huenda kwa mara nyingine ikafanya mbinu zote kuchukuwa hatua ya kudumu ya kunyakuwa na kulikalia eneo la Kusini mwa Lebanon kama ilivyowahi kufanya huko nyuma.

Libanon Beirut 2026 | Rauch über südlichen Vororten nach israelischem Luftangriff
Israel inalitazama kundi la Hezbollah kama kitisho kikubwa kwa nchi yake.Picha: Alkis Konstantinidis/REUTERS

Israel inalitazama kundi la Hezbollah kama kitisho kikubwa kwa nchi yake. Kundi hilo la wanamgambo wa kishia linamiliki hifadhi kubwa ya maroketi likiwa pia ni kundi lenye mfumo wa kijeshi uliopangwa vizuri kama ilivyodhihirika kwa mara nyingine kwenye wiki kadhaa za vita.

Kwa muhibu wa tathmini zilizofanywa na vyanzo vya usalama vya Israel, kundi hilo lina silaha zinazoweza kufika kwenye maeneo takriban yote ya Israel. Na kwa mujibu wa gazeti la Israel la Haaretz mkuu wa jeshi la ulinzi la nchi hiyo IDF Eyal Zamir alibainisha wazi mwanzoni mwa mwezi March kwamba Israel haiwezi kuvimaliza vita ikiwa kitisho kinachosababishwa na kuwepo kundi la Hezbollah hakijaangamizwa.

Afisa huyo wa kijeshi amesema lengo ni kulidhoofisha,au kuvunjavunja  kabisa uwezo wake wa kijeshi ndani ya Lebanon. Mtaalamu kuhusu Israel katika taasisi moja ya Ujerumani inayojihusisha na masuala ya kimataifa na usalama SWP iliyoko mjini Berlin, anauona mtazamo huo wa Israel kama ni mwelekeo mpya wa kimkakati wa kijeshi ambao umejitokeza baada ya mashambulizi ya Hamas Oktoba 7.

Mtaalamu huyo akizungumza na DW mnamo mwanzoni mwa mwezi Marchi, alifafanuwa kwa kusema, Lengo laIsrael inaonesha sio tena kuwadhibiti maadui  zake bali ni kuwakabili kijeshi mpaka pale watakapohakikisha sio tena kitisho kwa taifa hilo.

Lengo jingine ni kuweka uthabiti wa kudumu wa hali ya usalama kaskazini mwa nchi hiyo ambako tangu Hamas walipoishambulia Israel 2023 mapambano ya mara kwa mara na Hezbollah,yamesababisha Waisrael wengi kuhamishwa  kwenye eneo hilo la mpaka na Lebanon.

Juu ya yote hayo lakini, mtaalamu huyo kuhusu Isreal anasema, Hezbollah imekita mizizi ikiwa ni sehemu ya jamii nchini Lebanon,na kwahivyo kulimaliza kabisa kundi hilo sio jambo linalowezekana kiuhalisia.

Lakini anasema kitu ambacho kinawezekana huenda ni Israel ikajaribu kuweka eneo la usalama upande wa kusini na kuyadhibiti maeneo yaliyoshikiliwa na Hezbollah.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW