1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Lebanon: Mashambulizi yazua hofu ya mzozo kutanuka

1 Novemba 2025

Wadadisi wa masuala ya usalama wanaonya mashambulizi ya Israel dhidi ya maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon yanaweza kusababisha mlipuko wa vita vipya, licha ya juhudi za kidiplomasia kuzuia mzozo huo kuongezeka.

https://p.dw.com/p/52x8Z
Libanon Kfar Tibnit 2025 | Israelische Luftangriffe im Südlibanon
Picha: Mahmoud Zayyat/AFP

Mvutano kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran umeendelea kupamba moto. Siku chache zilizopita, jeshi la Israel lilishambulia kambi inayodaiwa kuwa ya mafunzo ya Hezbollah katika eneo la Bakaa, kaskazini-magharibi mwa Lebanon. Siku moja kabla, ndege isiyo na rubani ya Israel ilimuua kamanda wa kundi hilo, Issa Ahmad Karbala, kusini mwa Lebanon, kwa mujibu wa taarifa za Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF).

Karbala alitajwa kuwa mmoja wa makamanda wa kikosi cha Radwan cha Hezbollah, kilichohusishwa na mashambulizi dhidi ya Israel. Jeshi la Israel limesema litaendelea na operesheni za kijeshi kuhakikisha hakuna tishio kwa usalama wake, likiituhumu Hezbollah kwa kukiuka makubaliano ya amani yaliyopo kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon, watu 274 wameuawa tangu kuanza upya kwa mashambulizi ya Israel, wakiwemo zaidi ya raia 100. Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema zaidi ya makombora 950 yalirushwa kutoka Israel kuelekea Lebanon kati ya Novemba 2024 na Oktoba 2025, huku Hezbollah nayo ikirusha makombora 21 kuelekea Israel katika kipindi hicho.

Mashambulizi hayo yanakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotaka pande zote mbili kuacha mashambulizi mara moja. Mkataba huo uliitaka Israel kuondoa vikosi vyake kutoka Lebanon, huku Hezbollah ikitakiwa kuweka silaha zake chini na kuondoka hadi umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa Mto Litani. Hata hivyo, pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kutotekeleza makubaliano hayo.

Israel imeendelea kuilaumu Hezbollah kwa kujenga upya uwezo wake wa kijeshi, ikisema ni kinyume cha mkataba wa amani.

Kuondoa silaha za Hezbollah si jukumu la Israel pekee

Wiki iliyopita, Tom Barrack, balozi wa Marekani nchini Uturuki na mjumbe maalum wa rais wa Marekani kwa ajili ya Syria, alisema kupitia mtandao wa X kwamba "kuondoa silaha za Hezbollah si jukumu la Israel pekee, bali ni fursa ya kuhakikisha usalama wa eneo zima.”

Lebanon bado inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na kisiasa, hali iliyozorota zaidi baada ya vita vya miezi mitatu kati ya Septemba na Novemba mwaka 2024. Mashambulizi ya Israel mwaka huo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 4,000 na kuharibu sehemu kubwa ya Beirut na vijiji vya kusini. Benki ya Dunia inakadiria gharama ya ujenzi upya kufikia dola bilioni 11.

Licha ya misaada kutoka Marekani na Saudi Arabia, changamoto kubwa inabaki katika juhudi za kuwapokonya silaha wapiganaji wa Hezbollah — suala linaloonekana kudhoofisha mchakato wa kurejesha usalama wa kudumu. Israel bado imeweka wanajeshi wake katika maeneo matano kusini mwa Lebanon, ikisema hatua hiyo inalenga kulinda usalama wake wa taifa.

Wachambuzi wanasema ushawishi wa Iran, ambayo ni mshirika wa Hezbollah, na uungwaji mkono wa Marekani kwa Israel, vinapunguza nafasi ya serikali ya Lebanon kudhibiti makundi ya kijeshi huru nchini humo. Wanaonya kuwa mashambulizi ya angani na mauaji ya kulenga huenda yakazidisha mateso ya raia.

Mariam Fneish, mkazi wa Beirut mwenye umri wa miaka 25, aliiambia DW kwamba maisha yamekuwa ya hofu kutokana na ndege zisizo na rubani za Israel zinazoruka kila siku juu ya anga la jiji hilo.

"Ni vigumu kuhisi salama. Kila siku tunasikia kelele na ngurumo za ndege za kijeshi juu ya nyumba zetu,” alisema.