1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa ASEAN waridhia mpango wa kugawana mafuta

Amina Abubakar afp,reuters,dpa
8 Mei 2026

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa bara la Asia, ASEAN wamekubaliana kuanzisha mpango wa kikanda wa kugawana mafuta unaopaswa kuridhiwa haraka.

https://p.dw.com/p/5DV8q
Philippinen Cebu 2026 | ASEAN-Gipfel | Gruppenfoto der Staats- und Regierungschefs
Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa bara la Asia, ASEAN Picha: Aaron Favila/AP Photo/dpa/picture alliance

Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja unaozidi makubaliano ya kugawana mafuta katika kanda hiyo inayotegemea pakubwa uagizaji wa mafuta. Kanda hiyo inakabiliwa na  ukosefu wa nishati hiyo muhimu kufuatia kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz. Iran iliufunga Mlango huo kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi yake vilivyoanza Februari 28.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa bara la  Asia,  ASEAN ambaye pia ni rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr, ameelezea matumaini yake kwamba nchi wanachama zitakamilisha haraka uidhinishaji wa mpango huo wa hiari unaoendeshwa kwa misingi ya kibiashara, lakini akasisitiza kwamba taratibu za utekelezaji bado zinahitaji kufanyiwa kazi. Mpango huo unatarajiwa kupunguza athari ya vita vya Iran kwa mataifa yao, raia wake na uchumi kwa ujumla.

Viongozi hao sasa wametoa wito wa mkakati maalum utakaopelekea usafirishaji wa chakula na mafuta wakati mzozo kati ya Iran na Marekani ukiendelea kutanuka na mlango huo kufungwa kwa siku ya 70 sasa.

Thailand na Cambodia wakubaliana kujadiliana kuelekea amani 

Ferdinand Marcos Jr, amesema vita hivyo vya Iran vimesababisha msukosuko mkubwa wa kiuchumi na kuonyesha umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili kanda hiyo.

Philippinen Cebu 2026 | ASEAN- | Ferdinand Marcos Jr.
Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos JrPicha: Aaron Favila/REUTERS

Amesema mzozo huo umelikumbusha bara hilo ni kwa namna gani uchumi wao upo hatarini kutokana na mabadiliko hayo ya ghafla akisisitiza kwamba mgogoro ukiendelea zaidi utalifanya bara na dunia nzima kuchukua miaka mengi ya kujikwamua kiuchumi.

Kando na mzozo huo, Rais Ferdinand Marcos pia alisistiza umuhimu wa uhuru wa usafiri katika bahari ya China baada ya mvutano mkubwa kati ya Manila na Beijing kutokana na madai ya ya kila upande ya kumiliki visiwa vilivyojaa rasilimali za gesi asilia.

Katika mkutano wa Jumuiya hiyo ya ASEAN makubaliano ya kutafuta amani pia yalitangazwa kati ya nchi hasimu za Thailand na Cambodia. Rais Ferdinand Marcos Jr ametangaza kuwa baada ya mazungumzo, viongozi wa nchi hizo wameamua kujenga mahusiano ya kuaminiana, ili kufanikisha makubaliano tata ya usitishawji vita. Marcos Jr ameongeza kuwa nchi zote mbili zimesisitiza umuhimu wa kuvumiliana na kuwa na majadiliano kuelekea amani.