Sudan yautaka Umoja wa Mataifa kuondoa majeshi yake | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sudan yautaka Umoja wa Mataifa kuondoa majeshi yake

Serikali ya Sudan imetuma barua rasmi kwa Umoja wa Mataifa ikiutaka uondowe kikosi chake cha wanajeshi wa kulinda amani nchini humo ifikapo tarehe 9 Julai mwaka huu, tarehe ambayo Sudan ya Kusini itakuwa taifa huru.

Wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan (UNMIS)

Wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan (UNMIS)

Mjumbe wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa aliiwasilisha barua rasmi ya serikali kwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon, hatua inayopinga pendekezo la Umoja huo la kuongezwa muda wa kuhudumu wa kikosi hicho cha walinda amani kwa miezi mitatu ya ziada.

Katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjumbe huyo pamoja na mwakilishi wa serikali ya Sudan Kusini, walilaumiana kuhusu kuzidi kwa hofu katika mpaka wao, huku eneo la Kusini likitarajiwa kujitenga rasmi.

Ombi hili linajiri wakati mzozo ukiendelea kuhusu umiliki wa jimbo la Abyei lililopo katika mpaka huo, ambalo mpaka sasa kila upande unadai ni lake. Vikosi kutoka Khartoum viliudhibiti mji huo zaidi ya wiki moja iliyopita na kusababisha kuzuka mapigano mapya kati ya maeneo hayo mawili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Hatua hii haikupokelewa vizuri na eneo la Kusini na akizungumza awali, Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Barnaba Marial Benjamin, aliishtumu hatua hiyo na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua zipasazo.

"Ilikuwa hatua haramu na isiyo ya kikatiba kuuvamia mji wa Abyei. Hii ni hatua ya kivita isiyo na lengo zuri kwa makubaliano ya amani. Tunatarajia jumuiya ya kimataifa, hususan Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa kwa jumla, kuchukuwa hatua muhimu." Alisema Barnaba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Ahmed Karti, amesema kuwa kura ya maoni kuhusu kujitenga kwa Sudan ya Kusini iliashiria mwisho wa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 (CPA) yaliyopelekea wanajeshi 10,000 wa kulinda amani kuangalia utekelezaji wa makubaliano hayo kati ya Kaskzini na Kusini.

Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Barnaba Marial Benjamin (kulia)

Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Barnaba Marial Benjamin (kulia)

Mkuu wa operesheni za kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Alain Le Roy, amesema ni jukumu la Baraza la Usalama la Umoja huo kuamua ni hatua gani italichukulia ombi la Sudan.

Hata hivyo Le Roy ameziomba pande zote mbili kuonyesha utashi wa kisiasa katika kutafuta suluhu la mzozo wa Abyei, jimbo ambalo hadi sasa halijapiga kura ya maoni kuhusu mustakabali wake.

Na kwa kuitikia wito huo, hapo jana serikali ya Sudan ilizindua mipango ya kuutatua mzozo huo, ikiwemo utawala wa kubadilishana kuliongoza eneo hilo, na pia jeshi lake liendelee kusalia katika eneo hilo hadi kura hiyo ya maoni itakapofanyika.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari na Sudan, SUNA, mapendekezo hayo yalichapishwa katika taarifa ya wizara ya mambo ya nje.

Hapo jana (31.05.2011), Makamu wa Rais wa Sudan ya Kusini, Riek Machar, alikubaliana na mwenzake wa Kaskazini, Ali Osman Taha. kuunda kamati ya pamoja itakautatuwa mzozo huo wa Abyei.

Lakini Taha alikataa ombi la Sudan ya Kusini kulitaka jeshi la Kaskazini liondoke katika jimbo hilo, akisema kuwa jeshi hilo litaondoka pale tu patakapopatikana suluhu ya kisiasa.

Mwandishi: Maryam Abdalla/DPAE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com