Bashir asema Abyei ni sehemu ya Sudan Kaskazini | Matukio ya Afrika | DW | 25.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Bashir asema Abyei ni sehemu ya Sudan Kaskazini

Rais Omar Hassan Al-Bashir amesema kwamba majeshi ya nchi yake yaliyoingia kwenye jimbo la Abyei linalogombewa kati ya Kaskazini na Kusini, hayataondoka huko kwa kuwa hiyo ni sehemu ya Kaskazini.

Rais Omar Hassan Al-Bashir

Rais Omar Hassan Al-Bashir

Rais Bashir ametoa kauli hiyo, muda tu baada ya waziri wake wa shughuli za Baraza la Mawaziri, Luka Biong Deng, kujiuzulu wadhifa wake huo katika serikali ya Sudan hapo jana, akilalalamikia kile alichokitaja kuwa ni uhalifu wa kivita katika jimbo la Abyei, linalodhibitiwa na vikosi vya majeshi ya Kaskazini.

Deng, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, alisema walitaraji kuunda mataifa mawili yatakayokuwa na uhusiano mwema, lakini wenzao wa Kaskazini wanaonekana hawataki amani.

Mwanachama huyo wa chama cha Sudanese People's Liberation Movement (SPLM ), na ambaye anatokea jimbo hilo la Abyei linalokabiliwa na mzozo, amesema hawezi kuendelea kuhudumu katika serikali kuu ya Sudan kwa sababu vikosi vyake ndivyo vinavyofanya uhalifu huo wa kivita jimboni mwake.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema kiasi ya watu 15,000 wamekimbia ghasia katika eneo hilo la Abyei na hali inazidi kuwa tete.

Mwanzoni serikali ya Kaskazini mjini Khartoum ilikuwa imesema kuwa wanajeshi wake wako katika eneo hilo kurejesha utulivu tu, baada ya mashambulizi mabaya yaliyofanywa na vikosi vya Kusini Alhamis iliyopita.

DW inapendekeza