1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan hali ni tete

25 Mei 2011

Hali katika mkoa wa Sudan unaokabiliwa na machafuko ya Abyei imeendelea kuwa tete, baada ya Umoja wa Mataifa kuarifu kuwa helikopta zake nne zimeshambuliwa.

https://p.dw.com/p/11Nk3
Mripuko katika jimbo la Abyei
Mripuko katika jimbo la AbyeiPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Hua Jiang, amesema wanamgambo wa kabila la Waarabu la Misseriya ambao wanaungwa mkono na serikali ya Sudan kaskazini inawezekana kuwa wanahusika kwa shambulio hilo dhidi ya helikopta hizo za Umoja wa Mataifa katika mkoa huo wa Abyei, lakini, hata hivyo, wafanyakazi wake walitua salama.

Jumla ya mashambulio 14 yalifanywa wakati ilipokuwa ikianza kuruka hapo jana kutoka katika mji wa Abyei.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanamgambo hao waliuvamia mkoa huo wa Abyei na kuwalazimisha watu kuyakimbia makaazi yao, na kuongeza hali ya wasiwasi wakati ambapo Sudan kusini inaelekea kujitenga kama iliyopangwa ifikapo mwezi wa Julai.

Msemaji wa Umoja wa mataifa amesema kuwa kwa sasa wanamgambo hao kutoka Sudan kaskazini wanaelekea eneo la kusini.

Ameongezea kusema kuwa mapigano na matukio ya uporaji yamesimama baada ya waakazi wake kuondoka na kusema kuwa bidhaa nyingi za mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko katika eneo hilo pia yameibiwa.

Jeshi la Sudan ya kusini limepeleka vifaru vya kivita katika mkoa huo wa Abye, eneo la mpaka ambalo linakaliwa na watu wengi, na kusababisha kitendo hicho kupingwa na jumuia ya kimataifa na pia kuzuka hofu ya kuzuka mapigano mapya ya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na kusini.

Wakati huohuo, Rais wa Sudan Omar al Bashir amekataa kuyaondoa majeshi yake katika mkoa huo wa Abyei na kusema kuwa ni wa upande wake wa kaskazini.

Amesema kama kutatokea uchokozi wowote, ameshayaagiza majeshi yake kushambulia na kuongeza kusema kuwa amejiandaa kwa vita vipya juu ya mkoa huo.

Aidha akiipinga miito iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Ulaya kuondoa wanajeshi. Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Abdelrahim Mohammed Hussein, alisisitiza kuwa Abyei itabakia kuwa mji wa kaskazini mpaka watu wake watakapoamua wenyewe.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameitaka serikali ya Sudan kuhakikisha kuwa utaratibu wa sheria unafuatwa.

Ametaka pande zote mbili zisitishe shughuli zake za kijeshi na kuviondoa vikosi vyao katika eneo la Abyei na kuachana na uchokozi.

Kwa upande wake, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice, alionya matokeo mabaya kwa upande wa kibinadamu kuhusiana na kuvamiwa kwa mji huo wa Abyei na majeshi ya kaskazini, wakati yeye pamoja na wajumbe wengine wa baraza la usalama walipotembelea mji wa Juba, Sudan kusini hapo jana.

Mwandishi: Halima Nyanza (Reuters, AFP, AP)

Mhariri: Miraji Othman