1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle ajiuzulu uwenyekiti wa FDP, unaibu kansela

4 Aprili 2011

Wiki moja baada ya kushindwa vibaya kwa chama cha FDP katika chaguzi za mikoa ya Baden-Württemberg na Rheinland-Pfalz, mwenyekiti wa chama hicho, Guido Westerwelle, amejiuzulu wadhifa wake na ule wa unaibu kansela.

https://p.dw.com/p/10mz9
Guido Westerwelle
Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

Yumkini hakuna sababu moja tu ya kujiuzulu kwa Westerwelle, maana ukiacha maneno makali aliyokuwa akitupiwa na wenzake kwenye chama, kwa siku za karibuni amekuwa pia akishutumiwa na hata walio nje ya chama chake, kwa msimamo wa Ujerumani kujizuia kulipigia kura Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo liliruhusu uingiliaji kati kijeshi nchini Libya.

Matokeo yake ni kuwa, miaka yake kumi ya kuwa mwenyekiti wa chama hiki cha kiliberali, imemalizika kwa hotuba ya nusu dakika tu. Shinikizo kutoka ndani na nje ya chama chake, lilimfanya hapo jioni ya jana ashindwe hata kusubiri mawiyo ya leo (Jumatatu, 04.04.2011). Badala yake akaamua kuitisha mkutano wa waandishi wa habari ofisini kwake mjini Berlin, na kutangaza mwanzo wa mwisho wake kwenye siasa za uongozi wa FDP.

Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: dapd

"Sitogombea tena nafasi ya uenyekiti kwenye uchaguzi wa chama hapo mwezi Mei. Ninaweza kuwaambia kuwa uamuzi huu kwangu ulikuwa mzito kwa upande mmoja na mwepesi kwa upande mwengine. Mzito kwa kuwa mtu ambaye amekuwa kwenye chama kwa miaka kumi kama mwenyekiti inahitaji moyo kuwacha ghafla hivi. Lakini ni mwepesi kwa kuwa sasa tuna vijana wengi walio tayari kupigania nafasi za uongozi wa chama na kuchukua uongozi wa FDP." Ndivyo alivyowaambia waandishi wa habari.

Asubuhi ya jana tu, Westerwelle alikuwa ametoka safarini katika nchini za Asia. Wakati akiwa Japan na China, huku nyumbani kulikuwa kunatokota kauli za chinichini kumtaka awachie ofisi za uenyekiti wa chama.

Hadi hapo, bado marafiki na waungaji mkono wake, kama vile kiongozi wa FDP Bungeni, Birgit Homburger, na Katibu Mkuu wa chama Christian Lindner, hawakuwa wamependezewa na wazo la kujiuzulu kwa Westerwelle, kwani kwao hakuna kiongozi mwengine ambaye anaweza kujaa kikamilifu kwenye kiti cha uenyekiti.

Alijisahau

Akiwa kama mwenyekiti wa chama, Westerwelle anaonekana na wakosoaji wake kwamba amekuwa muda mwingi kujiengea haiba yake mwenyewe huku akisahau wajibu wake kwenye chama, jambo ambalo wanaona ni sababu ya kupoteza kwenye chaguzi za Baden-Württemberg na Rheinland-Pfalz.

Matokeo kama haya yalipotokea kwenye mkoa wa Mainz, Westerwelle alisema kwamba angelipendelea kuendelea kubakia mwenyekiti wa FDP, lakini si sasa tena. Hata hivyo, Westerwelle hajapoteza yote. Bado anaendelea kushikilia nafasi zake za uwaziri wa mambo ya nje.

Hata mwenyekiti wa FDP katika mkoa wa Schleswig-Holstein, Wolfgang Kubicki, ambaye ni mpinzani mkubwa wa Westerwelle, anatambua heshima ya Waziri huyu wa mambo ya nje.

"Kama FDP, tuna mengi ya kumshukuru Guido Westerwelle. Alikichukua chama hiki kutoka chini kabisa na kukiinua juu. Anatekeleza wajibu wake wa uwaziri wa mambo ya nje kwa ufanisi licha ya matatizo mengi, na kwa hili hapana suala la kumng'oa kwenye nafasi hizo." Anasema Kubicki.

Linapokuja suala la mrithi wa kiti cha Westerwelle, kwa sasa inaonekana kuwa, macho ya chama hiki cha kiliberali yanamuelekea sana Waziri wa Afya, Phillip Rösler, kijana wa miaka 38, mzaliwa wa Vietnam, aliyelelewa na wazazi wa Kijerumani kutoka jimbo la Niedersachsen, na ambaye alianza siasa tangu akiwa daktari kwenye jeshi la Ujerumani.

Mwandishi: Bettina Marx/ZPR Tafsiri: Mohammed Khelef Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman