Washirika wa serikali kuu wataka kupunguza kodi za mapato | Magazetini | DW | 07.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Washirika wa serikali kuu wataka kupunguza kodi za mapato

Mkutano wa kilele kati ya wakuu wa vyama shirika katika serikali kuu ya mjini Berlin, CDU/CSU na FDP, hatima ya Ugiriki na hali nchini Syria ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini hii leo.

default

Mwenyekiti wa CDU,Kansela Angela Merkel(kati) ,mkuu wa chama cha CSU Horst Seehofer(kulia) na kushoto mkuu wa chama cha FDP Philipp Rösler

Tuanzie lakini Berlin ambako washirika katika serikali kuu ya mjini Berlin wamekubaliana miongoni mwa mengineyo kupunguza kodi za mapato. Gazeti la "Landeszeitung" la mjini Lüneburg linajiuliza::

Muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali wa FDP wameweza kukubaliana kuhusu kupunguza kodi za mapato, kuufanyia marekebisho mfumo wa kuwatunza wagonjwa na pia kutolewa fedha ziada kwa ajili ya miundo mbinu. Inawezekana eti- mtu anaweza kujiambia. Hata hivyo, katika wakati huu wa mgogoro, hilo linaweza kutafsirika vibaya: Anaewahimiza wenye madeni katika kanda ya Euro wazidi kufunga mkaja, lakini nyumbani anamwaga fedha, hawezi kuaminika. Bila shaka, mpango huo uliobuniwa na ofisi ya kansela ni mbinu tu. Haijalengwa Athens, bali kwa wapiga kura nyumbani. Lakini Merkel na wenzake wanaonyesha wanashindwa kutambua hakuna tena majuha miongoni mwa wapiga kura wa Ujerumani. Kwa maneno mengine, lengo lao litawarejea wenyewe.

Deutschland Finanzkrise Euro Angela Merkel Regierungserklärung im Bundestag

Kansela Angela Merkel

Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linahisi mkutano huo wa kilele uliofanyika jana katika ofisi ya kansela mjini Berlin hautoshi. Gazeti linaendelea kuandika:

Makubaliano yaliyofikiwa hayamaanishi kwamba hakuna haja ya kuendelezwa majadiliano kuhusu sera za kodi ya mapato, kutunzwa wagonjwa na kadhalika. Matatizo ya kimsingi- ikiwa ni pamoja na kurahisisha mfumo wa malipo ya kodi, gharama watu wanazoweza kumudu za kuwatunza wagonjwa katika jamii inayozidi kuzeeka- bado yangalipo. Mabilioni ziada katika miradi ya usafiri ni tone tu katika janga la moto na hazitasaidia chochote. Mafanikio makubwa hayawi hivyo.

Einigung über Bildung einer Übergangsregierung in Griechenland

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papaandreou

Mada ya pili magazetini inahusiana na hatima ya Ugiriki kama mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linaandika:

Sio nchi zote 27 za Umoja wa ulaya zitafanikiwa kulifikia lengo kuu la umoja huo. Pengine hata mataifa 17 ya kanda ya Euro yasiweze kulifikia lengo hilo. Lakini wenye kujikokota hawatoweza tena kuamua kuhusu kasi ya kufuatwa. Umoja wa sarafu bado haujapwaya. Poland, Hungary na Lithuania, wote hao wanataka kujiunga nao. Na hali hiyo inamaanisha nini kwa Ugiriki? Ikiwa nchi hiyo itataka kurejesha upya sarafu ya Drachme, basi kuna hatari ya kukabwa na misuko suko ya kiuchumi ambayo athari zake zitakuwa mbaya kabisa. Na nchi hiyo itajikuta katika hali ya kutegemea zaidi misaada kutoka Ulaya. Ndio maana wagiriki wasiachie mgogoro wa Euro kuwa chanzo cha kujitoa katika Umoja wa ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Miraji Othman