Waapiga kura wa Uturuki waunga mkono mageuzi ya katiba | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waapiga kura wa Uturuki waunga mkono mageuzi ya katiba

Jumuia ya kimataifa yaipongeza Uturuki kutokana na kuungwa mkono na wananchi walio wengi mageuzi ya katiba

default

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan

Nchini Uturuki, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha AKP wanashangilia ushindi wa mabadiliko ya katiba kufuatia kura ya maoni mwishoni mwa wiki.Kupitishwa huko kwa mabadiliko ya katiba kumepongezwa na jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Ulaya, Ujerumani na Marekani.Hata hivyo ushawishi wa nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya unaonekana uko mbali miongoni mwa wanachama wa umoja huo.

Waungaji mkono na hata wale wanaoipinga Uturuki kuweza kujiunga na Umoja wa Ulaya, wamepongeza hatua hiyo ya kufanyiwa mabadiliko katiba inayolenga, kuufanyia mabadiliko mfumo wa sheria pamoja na kudhibiti ushawishi wa jeshi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema kura hiyo inaonesha dhamira ya Uturuki kuendelea na mpango wa mabadiliko ya ndani.

Hata hivyo lakini wakati Chama cha bwana Westerwelle cha FDP kikiipigia upatu Uturuki kupata uwanachama wa Umoja wa Ulaya, mshirika wake chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democrats hakioneshi kukubaliana na hoja hiyo.

Akitetea msimamo huo Waziri Westerwelle amesema Uturuki ni nchi muhimu isiyotahiki kutengwa.

"Uturuki inataka kupewa haki sawa, kuheshimiwa na kusikilizwa.Hakuna mtu atakayeweza kuiahidi Uturuki, lakini hakuna mtu atakaye iwekea mipaka nchi hii muihumu iliyofanya mabadiliko ya kimaendeleo.Hasa hiyo ndiyo sera yangu ya nje, kuweka uzani sawa."

Chama cha Kansela Merkel cha CDU kimekuwa mara zote kwa upande wake kikisisitiza sera zake rasmi kuwa Uturuki isipewe uanachama kamili wa Umoja wa Ulaya.

EU Deutschland Türkei Guido Westerwelle und Ahmet Davutoglu in Brüssel

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (kushoto) na waziri mwenzake wa Uturuki,Ahmet Davutoglu,walipokutana September 11 iliyopita mjini Bruxelles

Nao Umoja wa Ulaya kufuatia kura hiyo ya mabadiliko ya katiba, umeitaka Uturuki kutekeleza mabadiliko hayo na kutengeneza katiba mpya.Kamishna wa Umoja wa huo Stefan Fuele amesema Uturuki inawajibika kupitisha sheria itakayoruhusu utekelezaji wa mabadiliko hayo pamoja na kuwepo kwa katiba mpya.Amesema masuala hayo yataongeza demokrasia zaidi na kuendana na matakwa ya viwango vya Umoja wa Ulaya.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ambayo kwa sasa ndiyo inayoshikilia kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya Miguel Angel Moratinos, amesema kura ya mabadiliko hayo ya katiba yanatoa ujumbe wazi kuwa Uturuki imedhamiria kujiunga na umoja huo.Amesema kuwa pamoja na kwamba baadhi ya nchi wanachama bado zinawasiwasi lakini mwishowe mantiki itadhihirisha ukweli.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Carl Bildt amesema hatua hiyo ya Uturuki ni kufungua mlango wa Umoja wa Ulaya, ijapokuwa itachukuwa muda kukaribishwa ndani.

Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Uturuki katika kuukaribia ulimwengu wa kiislam,imepongeza hatua ya kufanikisha kura hiyo ya mabadiliko ya katiba.Marekani imekuwa ikiulaumu Umoja wa Ulaya kwa kuizuia Uturuki kuingia katika umoja huo.Rais Barack Obama amesema idadi kubwa ya watu waliyojitokeza katika kura hiyo ya inaonesha kuimarika kwa demokrasia nchini Uturuki.

Uturuki imewasilisha ombi la kujiunga na Umoja wa Ulaya miaka mitano iliyopita na imekuwa ikilalamika kuhusiana na kusuasua kwa majadiliano ya kuipatia uanachama huo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/DPA

Mhariri:Mohamed Abdulrahman

 • Tarehe 13.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PB5y
 • Tarehe 13.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PB5y
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com