Uwezo wa Gaddafi kutawala wazidi kupungua | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.02.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uwezo wa Gaddafi kutawala wazidi kupungua

Mapambano makali kati ya wanajeshi wa Muammar Gaddafi na vikosi vilivyoasi na kujiunga na waandamanaji nchini Libya yameripotiwa, huku Gaddafi akipumulia upumzi wa mwisho kulinda sehemu ya himaya yake iliyosalia.

Vizuizi vya njia vilivyowekwa na waandamanaji

Vizuizi vya njia vilivyowekwa na waandamanaji

Kutoka mji wa Misrata, taarifa zinasema kwamba, waasi wameiangusha ndege ya kijeshi iliyokuwa ikijaribu kushawambulia, katika mapambano ambayo vikosi vya Muammar Gaddafi vinajaribu kuvikusanya vipande vipande utawala wa kiongozi huyo unaoporomoka kwa kasi.

Shahidi mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, Mohammed, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwa njia ya simu, kwamba ndege hiyo iliangushwa asubuhi hii ilipokuwa ikikishambulia kituo cha redio, na kwamba sasa waandamanaji wanawashikilia marubani wake.

"Mapigano ya kudhibiti kituo cha jeshi la anga yalianza usiku na bado yanaendelea. Vikosi vya Gaddafi vinadhibiti sehemu ndogo tu. Waandamanaji wanadhibiti sehemu kubwa zaidi, ambayo ndiyo yenye silaha." Amesema Mohammed.

Duara la udhibiti la Gaddafi lazidi kupungua

Muammar Gaddafi

Muammar Gaddafi

Kwa siku sasa, vikosi vitiifu vimekuwa vikijaribu kulizima vuguvugu la umma, ambalo hadi sasa limefanikiwa kuvuna uungaji mkono wa sehemu kubwa ya jeshi, na kumaliza udhibiti wa kiongozi huyo kwa eneo la mashariki ya Libya na kuanza kushikilia miji ya magharibi iliyo karibu na mji mkuu wa Tripoli, ambayo ukiacha mji wake alikozaliwa, ni ngome pekee ya Gaddafi iliyobakia.

Kufikia mchana wa leo, bado waandamanaji wanaosaidiwa na vikosi kadhaa vilivyomuasi Gaddafi, ndio wameonekana wakizidi kujiimarisha, na sasa wafuatiliaji wa masuala ya kijeshi, wanasema ni suala la muda tu kwa kiongozi huyo aliyejijenga kama shujaa wa Afrika, hajafikwa alipo, ikiwa ataendelea kukaidi matakwa ya waandamanaji wanaomtaka awachie madaraka.

Katika mji wa tatu kwa umuhimu wa Misrata, ulio umbali wa kilomita 200 mashariki ya Tripoli na ule wenye mitambo ya mafuta wa Zawiyah ulio kilomita 50 magharibi ya Tripoli, ni umma unaosadiwa na wanajeshi walioasi ndio wanaoshikilia madaraka.

Saif al-Islam awa msemaji wa utawala wa baba yake

Saif al-Islam

Saif al-Islam

Leo hii pia mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, ambaye alikuwa ametarajiwa kuwa mrithi wake, lau kama si hili vuguvugu la umma, alijitokeza kwenye kundi la waandamanaji wanaomuunga mkono baba yake mjini Tripoli, akiapa kwamba baba yake atapambana hadi dakika ya mwisho, na kurudia kauli ya Gaddafi ya kuwapa silaha wafuasi wake ili wailinde nchi yao.

Katika mazungumzo yake na vyombo maalum vya habari alivyovichagua mwenyewe, Saif al-Islam ambaye sasa anaonekana ndiye msemaji rasmi wa utawala wa baba yake, amekanusha vikali taarifa kwamba, sehemu kubwa ya wanajeshi na polisi, aidha wamebwaga silaha chini, au wamejiunga na waandamanaji, akisema kwamba huo ni uzushi.

"Munachosikia ni uzushi, ripoti za uongo. Tafadhalini chukueni kamera zenu asubuhi ya kesho, muende mji wowote wa Libya, mukaone wenyewe. Kila kitu kiko shwari, kila mji uko kwenye utulivu." Saif al-Islam amewaambia waandishi hao.

Lakini wakati Saif al-Islam akisema hivyo, kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimemuonesha Jenerali Marzouk al-Jindali, mmoja wa makamanda wa kikosi cha jeshi la anga, akisema kwamba wao wamejiunga na wananchi kutetea maslahi ya umma.

"Kituo kizima cha kijeshi ambacho kiko chini yangu kimejiunga na mapinduzi ya umma. Tuna wapiganaji bora kabisa. Tukiwa kama wanajeshi, tunataka ifahamike kuwa haya si mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala. Sisi hatuongozi chochote. Haya ni mapinduzi ya umma yanayoongozwa na vijana. Dhima yetu ni kuyaunga mkono na kuyalinda. Hilo ndilo lengo letu." Amesema al-Jindali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFPE/Al-Jazeera
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com