1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yafanya kazi na wapinzani wa Libya

28 Februari 2011

Huku hali ya mambo ikizidi kwenda kombo huko Libya, na Muammar Gaddafi akizidi kupoteza udhibiti wa nchi, kuna dalili kwamba jumuiya ya kimataifa imeshaondoa uwezekano wa kiongozi huyo kurudi tena madarakani.

https://p.dw.com/p/10QZG
Waandamanaji mjini Benghazi
Waandamanaji mjini BenghaziPicha: AP

Katika mji wa Zawiyah, ulio umbali wa kilomita 50 tu, kutoka ngome kuu ya Muammar Gaddafi, waasi wanasubiri moja kati ya mawili: ama ushindi dhidi ya utawala wa Gaddafi au mashambulizi ya vikosi vyake, lakini kwa vyovyote vile hawakusudii kurudi tena nyuma.

Kiasi ya wanajeshi 2,000 wa Gaddafi wanaripotiwa kuuzingira mji huu, lakini aliyekuwa meja wa polisi na ambaye sasa amejiunga na waandamanaji.

"Tutafanya kila tuwezalo kupambana nao. Watashambulia muda si mrefu. Lakini ikiwa tunapigania uhuru, tuko tayari kufa kwa ajili yake." Amesema meja huyo.

Hata hivyo, Jenerali Ahmed el-Gatrani, mmoja kati ya viongozi wa juu wa jeshi la Gaddafi, ambaye sasa anapigana upande wa waandamanaji, mashariki wa Libya, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba vikosi vyake viko tayari kwenda kuwasaidia wenzao wa Magharibi kama vikihitajika.

"Ndugu zetu wa Tripoli wanasema: 'Tuko sawa hadi sasa, hatuhitaji msaada.' Lakini iiwa watahitaji msaada, tuko tayari kwenda." Amesema Jenerali el-Gatrani.

Wachambuzi wa mambo wanategemea waasi watauchukua mji mkuu wa Tripoli na kumkamata au kumuua Gaddafi, lakini inahofiwa kwamba Gaddafi ana uwezo wa kuiingiza nchi katika mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo yeye na mwanawe, Saif al-Islam, wameshaonya.

Mataifa yamtenga moja kwa moja Gaddafi

Maandamao dhidi ya Gaddafi
Maandamao dhidi ya GaddafiPicha: picture alliance / dpa

Katika hatua nyengine, mataifa yenye nguvu duniani, yanasema kwamba umeshafika wakati wa Gaddafi kuondoka madarakani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, amefikia umbali wa kusema kwamba nchi yake tayari imeanza kuwasiliana na makundi ya upinzani nchini Libya, akionesha pia utayari wa Marekani kuyasaidia makundi hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema kwamba ni wazi kuwa zama za Gaddafi madarakani zinakaribia kwisha na, kwa hivyo ni lazima yeye na familia yake wakaepusha umwagikaji damu zaidi.

"Japo hali ya Libya asubuhi hii haiwezi kutabirika, lakini mtu anaweza kuona kuwa ile nguvu ya familia ya mtawala na uwezekano wake wa kubakia madarakani unapotea. Kwa hivyo, tunasema na tunatarajia kuwa siku za dikteta zinahesabika." Amesema Westerwelle katika mahojiano yake na Deutsche Welle mapema leo asubuhi.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini, amesema kwamba, hali ilipofikia sasa, haiwezi tena kurudi nyuma, na kuongeza kuwa ni jambo lisiloepukika kwa Gaddafi kuondoka.

Uingereza imeondoa kinga ya kidiplomasia kwa Gaddafi na kusema kuwa inazuia mali za familia yake, huku Waziri wake wa Mambo ya Nje, William Hague, akisema kuwa: "Ni wakati wa Gaddafi kuondoka."

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, amesema kwamba, aliongea na Gaddafi kwa simu, siku ya Ijumaa, na kumshauri aondoke.

Ni Blair ndiye aliyechangia sana kurudishwa kwa utawala wa Gaddafi kwenye uso wa jumuiya ya kimataifa, baada ya kuwa umetengwa kwa takribani miaka 35.

Kwa upande wake, Ufaransa imesema kwamba itaanza kupeleka misaada kwa upinzani kwenye maeneo ambayo tayari yako mikononi mwa wapinzani. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Francois Fillon.

Akizungumza na kituo cha redio cha RTL, Fillon amesema kuwa ndege zilizobeba madaktari, manesi, madawa na vifaa vya matibabu zingeliondoka Paris kuelekea Benghazi asubuhi hii.

Kikao cha mawaziri wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kinafanyika leo hii mjini Geneva, Uswisi, ambapo pia mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Ulaya watakutana kujadiliana hatua za pamoja kuelekea Libya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman