Ulaya na Australia zakubaliana biashara huria
24 Machi 2026
Makubaliano hayo pia ni ya upatikanaji wa madini nadra, wakati ambapo kuna msukosuko wa kibiashara duniani. Haya yametangazwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese.
Tangazo hilo limekuja miaka 8 baada ya mazungumzokuhusiana na mkataba huo kuanza. Makubaliano hayo yanalenga kuondoa ushuru na vigingi vya kibiashara kwa pande zote mbili ili kuongeza biashara za bidhaa na huduma.
Mivutano na China na mahusiano mabovu na Marekani
Kumalizika kwa mazungumzo hayo ni sehemu ya msukumowa Umoja wa Ulaya kutafuta washirika tofauti wa kibiashara wakati mivutano na China kuhusiana na kutatizwa kwa masoko unapoendelea na uhusiano na Marekani ukiwa umekuwa mbaya chini ya Rais Donald Trump.
"Hatuwezi na hatutoufuata mfumo wa kibiashara wa China. Mwaka jana kwa mara ya kwanza, kila taifa mwanachama wa Umoja wa Ulaya lilikuwa na mapungufu ya kibiashara na China, kitisho katika usambazaji wa bidhaa pamoja na mshtuko katika msingi wa viwanda vyetu vinahitaji jawabu la haraka na hili ni jawabu tunaloweza kulipata pamoja kwa Ulaya na Australia," alisema Von der Leyen.
Kulingana na Umoja wa Ulaya, makubaliano hayo yanatoa fursa ya kuondolewa kwa asilimia 99 ya ushuru kwa bidhaa za Umoja wa Ulaya kwa Australia, hatua itakayoziokolea kampuni zote kubwa na ndogo karibu yuro bilioni moja kila mwaka kama ushuru.
Makubaliano hayo pia yanalenga kurahisisha hatua ya raia wa Umoja wa Ulaya kufanya kazi Australia.
Kulingana na Halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya, sekta za viwanda zinazoweza kunufaika na makubaliano hayo ni pamoja na uhandisi, viwanda vya kemikali, magari na kilimo.
Umoja wa Ulaya pia unatarajiwa kuweza kupata madini muhimu ya kimkakati ya Australia.
Kwa Australia, kuondolewa kwa bidhaa zake kama mvinyo na vyakula vya baharini ni muhimu. Bidhaa nyengine zaidi za kilimo kama nyama zinaweza kuuzwa katika mataifa ya Ulaya katika miaka ijayo.
Waziri Mkuu wa Australia Albanese amesema makubaliano hayo yatazinufaisha pande zote mbili.
"Makubaliano ya biashara huria ya Australia na Umoja wa Ulaya yatakuwa mafanikio ya mara moja yatakayelta ajira na maendeleo kwa vizazi vijavyo. Hii ilikuwa hatua muhimu kwa washirika wawili, ila kama tunavyojua, hatukuwa na budi. Ilitokana na juhudi na mazungumzo ya kujenga na ilihitaji pande zote zitazame manufaa makubwa na fursa zinazoweza kupatikana pande zote," alisema Albanese.
Albanese na Von der Leyen pia wametangaza ushirikiano mpya wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya na Australia. Serikali ya Australia imesema ushirikiano huo mpana utaongeza ushirikiano kote katika sekta ya ulinzi, mtandao, usalama wa kiuchumi, mapambano dhidi ya ugaidi na vitisho.
Idhini ya Umoja wa Ulaya na bunge lake
Makubaliano hayo lakini yanahitaji kuidhinishwa na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya na Bunge la Ulaya na vile vile Australia, kabla hayajatiwa saini.
Haijabainika ni lini mkataba huo utatekelezwa na itategemea pia iwapo utaidhinishwa kwa haraka na Umoja wa Ulaya.
Ikumbukwe kwamba hivi majuzi makubaliano makubwa ya biashara huria kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Mercosur ya Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay yalipelekwa katika Mahakama ya Kisheria ya Ulaya ili kupitiwa upya kisheria na wabunge wa Ulaya, jambo lililotishia utekelezwaji wake, licha ya kuwa tarehe ya muda ya utekelezwaji kuwekwa kuwa Mei mosi.
Mkataba huo wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya na mataifa ya Mercosur unakosolewa na wakulima wa Ulaya kwa kuwa wanahofia ongezeko la ushindani.
Vyanzo: DPA/AFP