Orban: Wahangari wa Ukraine wanatumika kwa propaganda
9 Aprili 2026
Peter Filipovics, mwanajeshi wa Ukraine mwenye asili ya Hungary anayepigana kwenye mstari wa mbele mashariki mwa Ukraine, anasema mara kwa mara hufuatilia habari kutoka Hungary, hasa kampeni za uchaguzi za Orbán ambazo mara nyingi huilenga Ukraine, nchi ambayo yeye binafsi anaitetea dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Wanasiasa wa chama tawala cha Fidesz nchini Hungary wamekuwa wakiitaja Ukraine kama "taifa la kifisadi, la kimafia na la kigaidi,” huku wakisambaza madai yasiyo na ushahidi kuwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, anatumia fedha za Umoja wa Ulaya kujenga anasa kama vyoo vya dhahabu.
Filipovics anasema madai hayo yanapingana na ukweli, akitolea mfano kashfa ya ndani ya Hungary iliyomhusisha aliyekuwa mkuu wa benki kuu, György Matolcsy, ambaye aliripotiwa kuweka vifaa vya kifahari katika majengo ya benki. Anaamini kuwa kabla ya kuikosoa Ukraine, viongozi wa Hungary wanapaswa kujitathmini wao wenyewe.
Wahangari wapatao 8,000 wanaishi Ukraine
Kwa mujibu wa makadirio yasiyo rasmi, takribani Wahungary 80,000 wanaishi Ukraine, hasa katika eneo la Transkarpatia, na wanaunda sehemu ndogo sana ya wakaazi jumla. Hata hivyo, Orbán amelifanya suala lao kuwa sehemu kuu ya sera zake za nje na kampeni za kisiasa, akidai kwa muda mrefu kuwa wananyanyaswa na kulazimishwa kujiunga na jeshi.
Pamoja na madai hayo, serikali ya Hungary imekuwa ikishirikiana na Urusi kuhamisha wafungwa wa vita wenye asili ya Hungary kutoka Urusi kwenda Hungary bila kushirikisha mamlaka za Ukraine, hatua inayotajwa na Kremlin kama ya kibinadamu, lakini inayozua maswali ya kisheria na kisiasa.
Nchini Ukraine, mfumo wa uandikishaji wanajeshi umeibua malalamiko, huku vituo vya uandikishaji vikilaumiwa kwa kutumia nguvu au mbinu kali, na hata Kamishna wa haki za binadamu wa Ukraine, Dmytro Lubinets, amekosoa ukiukwaji wa haki na mazingira mabaya katika baadhi ya vituo hivyo.
Hata hivyo, wachambuzi na viongozi wa jamii ya Wahangari nchini Ukraine wanakataa madai kuwa Wahangari wanaandikishwa kwa kiwango kikubwa kupita wengine, wakisema idadi yao jeshini ni ndogo kuliko uwiano wao katika jamii, jambo linalopingana na simulizi ya serikali ya Hungary.
Kuhusu uhamishaji wa wafungwa wa vita, baadhi ya waliowahi kushikiliwa wanasema walishinikizwa kushiriki katika propaganda za Urusi ili waweze kupelekwa Hungary, huku wengine wakikataa na kulipa gharama ya kuendelea kuzuiliwa na kuteswa kabla ya kuachiliwa.
Licha ya propaganda na mvutano wa kisiasa, wanajeshi kama Filipovics wanaendelea kupigana kwenye mstari wa mbele, wakisema wanatetea uhuru wa nchi yao dhidi ya uvamizi wa Urusi, na hawana nia ya kuondoka Ukraine wala kuishi katika Hungary wanayoiona kuwa karibu zaidi na msimamo wa Urusi.