Hungary kupinga vikwazo vya EU dhidi ya Urusi
22 Februari 2026
Hii ni hatua ya hivi karibuni ya Hungary kuishinikiza Ukraine kuanzisha tena mtiririko wa mafuta ya Urusi kupitia bomba linalosambaza nishati hiyo muhimu nchini mwake.
Szijjarto, amesema hadi pale Ukraine itaporuhusu kurejea kwa shughuli za usafirishaji mafuta kuingia Hungary na Slovakia kupitia bomba la Druzhba kutoka Ukraine, ndipo nchi yake itakaporidhia uamuzi wowote muhimu unaoihusu Kiev kupita.
Usafirishaji wa mafuta ya Urusi kwenda Hungary na Slovakia kupitia bomba la Druzhba umesitishwa tangu January 27, wakati Kiev iliposema droni kutoka Urusi ililenga kituo cha mitambo ya kusafisha mafuta.
Slovakia na Hungary zimesema Serikali ya Volodymyr Zelensky inapaswa kulaumiwa kwa tatizo hilo.
Ulaya inajitayarisha na duru ya 20 ya vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na vita vyake kwa jirani yake Ukraine. Wakati majadiliano hayo yakiendelea mataifa mengi wanachama wa Ulaya yangelipenda kulifanikisha hilo kabla siku ya kumbukumbu ya vita hivyo vinavyoingia mwaka wake wa nne Februari 24.