1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Tutaishambulia Iran na kuirejesha katika zama za kale

2 Aprili 2026

Rais wa Marekani Donald Trump amesema vikosi vya Marekani vitairudisha Iran katika zama za kale za mawe, wakati ambapo teknolojia ilikuwa ya kiwango cha chini kabisa.

https://p.dw.com/p/5Ba19
USA Washington D.C. 2026 | Donald Trump spricht bei Fernsehansprache zum Nahostkonflikt
Picha: Alex Brandon/AFP

Akilihutubia taifa kuhusu muelekeo wa vita vya Iran vilivyoingia siku yake ya 34,  Trump amesema katika wiki mbili hadi tatu zijazo, vikosi vya Marekani vitaendelea kuishambulia vikali nchi hiyo na kuirejesha katika zama hizo za kale za mawe huku akisifu operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran, akisema malengo ya Washington yametimizwa kuliko ilivyotarajiwa.

"Tunatumia mkakati wa kimfumo kuusambaratisha uwezo wa utawala wa kuitishia Marekani au kuonyesha nguvu zake nje ya mipaka yake. Hii inamaanisha kuuharibu kabisa uwezo wa jeshi la majini la Iran, ambalo kwa sasa limesambaratishwa, tumelisambaratisha pia jeshi lao la anga pamoja na mifumo yao ya kurushia makombora katika viwango ambayvo havijawahi kuonekana. tumevunja uwezo wao wa kuendelea kuwaunga mkono mawakala wa vita na makundi ya kigaidi, na pia kuwanyima nafasi ya kuwa na silaha za nyuklia," alisema Trump.

USA Washington D.C. 2026 | Donald Trump spricht über den Krieg gegen den Iran
Rasi wa Marekani Donald Trump alihutubia taifa lake kuhusu muelekeo wa vita vya Iran Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Donald Trump hata hivyo hakusema lolote kuhusu  Marekani kuzungumza na Iran kuhusu usitishwaji vitahivyo au hata kugusia kuhusu muda wa  mwisho alioutoa kwa Iran wa Aprili 6, wa kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumika kusafirishia asilimia 20 ya gesi na mafuta ya dunia, pamoja na bidhaa nyengine muhimu ikiwemo chakula. Awali rais huyo wa Marekani alikuwa ametishia kushambulia miundombinu ya mafuta na maji ya Iran, iwapo eneo hilo muhimu lililofungwa na Iran halitofunguliwa.

Iran yaapa kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Israel na Marekani

Katika hotuba yake, Trump pia hakuelezea namna ya kudhibiti kuyumba kwa masoko ya nishati yanayosababisha bei ya mafuta kupanda maradufu, na pia hakuzungumzia pia uwezekano wa kutuma majeshi ya ardhini Iran na wala hakuitaja kabisa Jumuiya ya Kujihami NATO, muungano ambao ameukosoa vikali kwa kushindwa kutuma meli zao za kivita kusaidia kuufungua mlango bahari wa Hormuz.

Huku hayo yakiarifiwa Iran imejibu ikisema itaendelea kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Marekani na Israel. Kamanda anayeongoza operesheni ya vita ya Khatam Al-Anbiya, Ebrahim Zolfaqari, amesema wanaamini kwamba Mungu atawapa nguvu ya kuendelea kuwashambulia hadi pale watakapoaibika, umbuka, kujutia na hatimae kusalimu amri.

Iran Teheran 2025 | Präsident Masoud Pezeshkian beim ECO-Innenministertreffen
Iran yaapa kuendelea na mashambulizi yake dhidi ya Marekani na Israel Picha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Haya yanajiri wakati Israel ikisema Iran imeishambulia hii leo asubuhi, huku Umoja wa Falme za kiarabu ukisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa tena ikikabiliana na "vitisho” vya makombora na droni.

China yatoa wito wa vita kusitishwa haraka

Kwengineko wizara ya mambo ya nchi za nje ya China imetoa taarifa ikisema sababu ya kufungwa Mlango wa Hormuz na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani, kumetokana na operesheni ya kijeshi  iliyosema siohalali nchini Iran.

Beijing imetaka vita hivyo kusitishwa mara moja hasa baada ya Trump kusema Marekani itaendeleza mashambulizi yake huko kwa wiki kadhaa zijazo.

Wakati huo huo Uingereza imesema inapanga kukusanya mataifa 35 kwa mazungumza hii leo Alhamisi kwa njia ya vidio, kujadili njia mbadala za kidiplomasia na kisiasa za kuifungua njia hiyo muhimu ya kusafirishia mafuta. Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer, amesema waziri wake wa mambo ya nje Yvette Cooper atasimamia hilo.