Serikali ya Uturuki yaanza juhudi za kuibadili katiba | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Uturuki yaanza juhudi za kuibadili katiba

Serikali ya Uturuki hii leo imeanza juhudi za kuibadili katiba ili rais wa nchi hiyo aweze kuchaguliwa na raia badala ya bunge. Jana serikali ilipata pigo jipya wakati wabunge wa upinzani walipogoma kuingia bungeni kwa mara ya pili kuzuia kura ya kumchagua rais mpya. Kufuatia hatua hiyo, mgombea wa chama tawala, Abdullah Gul, alijiondoa kutoka kinyang´anyiro cha kugombea urais wa Uturuki.

Abdullah Gül

Abdullah Gül

Serikali ya Uturuki leo inajaribu kushinikiza katiba ibadilishwe ili rais wa nchi achaguliwe moja kwa moja na wananchi badala ya kuchaguliwa na bunge. Kujiondoa kwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Abdullah Gul kutoka kinyang´anyiro cha kuwania urais ni pigo jipya kubwa kwa chama tawala cha AKP, ambacho kimelazimika kuitisha uchaguzi wa mapema ili kuutanzua mzozo wa kisiasa nchini Uturuki.

Abdullah Gul, alijiondoa kutoka kwa wadhifa wake kufuatia mbinyo wa jeshi la Uturuki na waandamanaji waliokishutumu chama tawala cha AKP kwa kutaka kuibadili Uturuki kuwa taifa la kiislamu. Bwana Gul alichukua uamuzi huo, ambao huenda ukautanzua mgogoro wa kisiasa nchini Uturuki, baada ya chama chake kushindwa kuwa na idadi ya wabunge inayotakikana bungeni kuweza kumchagua.

Alipotangaza kujondoa kwake, Abdulah Gul alisema mpasuko wa kisiasa unaondelea kuhusu uteuzi wake kama mgombea wa wadhifa wa urais kati ya chama tawala na wabunge wa upinzani wasiozingatia sana maadili ya kidini, kumelizuia bunge kufanya kazi yake ya kumchagua rais wa nchi.

´Hakuna haja ya kuwa na duru mpya ya uchaguzi. Bunge limekwama na kwa hivyo jambo sahihi la kufanya ni Waturuki wamchague rais wao mpya,´ alisema Abdullah Gul wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Ankara. Bwana Gul alisema duru za uchaguzi zisizo na maana zimeishusha hadhi ya bunge la Uturuki.

Mzozo wa kisiasa nchini Uturuki umedhihirisha wazi mpasuko mkubwa unaozidi kati ya Waturuki walio wafuasi wa malimwengu na wafuasi wa chama cha waziri mkuu Reccep Tayyip Erdagan kilicho kita katika misingi ya dini ya kiislamu katika taifa ambamo maoni kwamba dini isiwe msingi wa elimu na maadili yamejumulishwa katika katiba na yanalindwa vikali na mahakama na jeshi.

Chama cha AKP ambacho kimekuwa kikipigania Uturuki ijiunge na Umoja wa Ulaya na ambacho pia kimeleta mageuzi ya mataifa ya magharibi nchini Uturuki, kinapinga kwamba misingi yake imekita katika dini ya kiislamu.

Bunge nchini Uturuki lina jukumu la kumchagua rais ambaye hutawala kwa kipindi cha miaka saba. Chama cha AKP kinatarajiwa kushinda uchaguzi mkuu ujao nchini Uturuki, lakini kwa mujibu wa kura ya maoni ni mapema mno kusema ikiwa kitaweza kuunda serikali ya chama kimoja. Wachambuzi wanasema ushindi katika uchaguzi mkuu unatakiwa kukipa chama cha AKP haki ya kuwasilisha mgombea wake wa wadhifa wa urais kupitia bungeni au kwa kuchaguliwa na raia.

 • Tarehe 07.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEm
 • Tarehe 07.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEm

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com