Umoja wa Ulaya na vizuizi vya Hungary
23 Septemba 2025
Kuondoka ukumbini kwa kisingizio cha "mapumziko ya kahawa,” mbinu ngumu za kisheria kuhusu matumizi ya mapato ya riba itokanayo na mali za Urusi zilizozuwiwa, au taarifa za mwisho za wakuu wa nchi na serikali bila Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban – mifano hii inaonesha jinsi Umoja wa Ulaya (EU) ulivyolazimika mara kadhaa kufanya maamuzi bila Hungary au kuitenga.
Hata hivyo, katika siasa za nje na usalama jambo hili linazidi kuwa gumu. Kila awamu ya vikwazo dhidi ya Urusi, ambazo sasa zimefika kwenye awamu ya 19 zinazojadiliwa, inapaswa kuidhinishwa na wanachama wote. Vivyo hivyo katika siasa za kodi au suala la kupokea wanachama wapya wa EU, taifa moja linaweza kukwamisha maamuzi yote kwa kura ya turufu.
Hali hii "siyo kosa kimaadili,” alissema Nicolai von Ondarza kutoka Taasisi ya Sayansi na Siasa (SWP) katika mazungumzo na DW. Anafafanua kuwa masuala hayo mara nyingi ni "mambo ya msingi ya uhuru wa kitaifa.” Kwa hivyo, mataifa mara chache hukubali kushindwa kwa kura yanapokuja masuala ya maslahi yao binafsi. Mfano ni Ujerumani, ambayo mara nyingi huonyesha msimamo tofauti katika siasa za EU kuhusu Israel.
Hata hivyo, Ondarza anasema tatizo kuu ni kwamba mara nyingi Hungary haitumii kura yake ya turufu kwa masuala husika, bali kama njia ya "kushinikiza” wanachama wengine ili kupata masharti au maslahi katika nyanja tofauti. Kwa lugha ya Umoja wa Ulaya, hili huitwa "kura ya turufu ya kimkakati”.
Hasa katika siasa za Umoja wa Ulaya kuhusu Ukraine, Waziri Mkuu Viktor Orban mara kwa mara huweka vizuizi. Hali hii imefanya msaada kwa Ukraine wenye thamani ya takribani euro bilioni 6.6 kutoka Mfuko wa Amani wa Ulaya kucheleweshwa na kutolipwa hadi sasa. Aidha, Hungary inapinga hatua zinazohusiana na uwezekano wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya, ikidai miongoni mwa sababu kwamba hatua hiyo inaweza kuivuta EU moja kwa moja vitani na Urusi. Hata hivyo, licha ya upinzani, serikali ya Orban mwishowe imekuwa ikikubali kila moja ya hatua 18 za vikwazo dhidi ya Urusi zilizopitishwa hadi sasa.
Kwa nadra sana, wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya pia hutumia mbinu hii ya turufu ya kimkakati, anasema mchambuzi wa siasa Nicolai von Ondarza. Mfano ni mwaka 2020, ambapo Cyprus ilizuia vikwazo dhidi ya Belarus ili kushinikiza hatua kali zaidi za Umoja wa Ulaya dhidi ya Uturuki.
Mawaziri wa mambo ya nje wanataka kujadili mbinu za kazi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen, alisema hivi karibuni katika mkutano usio rasmi mjini Copenhagen kwamba Umoja wa Ulaya una "tatizo la kikatiba.” Akifananua hali hiyo, alisema: "Meli ya polepole zaidi kwenye msafara ndiyo huamua kasi. Tunapaswa kupata njia ambazo msimamo wa wengi barani Ulaya unaweza kushinda.” Kwa sababu hiyo, alisisitiza kwamba EU inapaswa kutafuta "suluhisho za ubunifu.”
Hata hivyo, jinsi mbinu hizo mpya za kazi zinavyoweza kuonekana haikujadiliwa katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa Agosti. Mwakilishi Mkuu wa EU katika masuala ya kigeni, Kaja Kallas, alisema mjadala huo "kwa hakika” utafanyika katika miezi ijayo, akiongeza kwamba hili ni "swala la kuaminika” kwa Umoja wa Ulaya.
"Kundi la marafiki” linataka kupunguza maamuzi kwa kauli moja
Mnamo mwaka 2023, kwa msukumo wa Ujerumani, liliundwa "Kundi la Marafiki kwa ajili ya kuboresha maamuzi katika Sera ya Pamoja ya Mambo ya Nje na Usalama.” Kwa mujibu wa Baraza la EU, tayari mataifa 12 yanashiriki. Mbali na Ujerumani, wanachama wengine ni Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Italia, Luxemburg, Uholanzi, Romania, Slovenia, Uhispania na Sweden.
"Kundi la Marafiki” limependekeza, kwa mfano, kwamba maamuzi kuhusu vikwazo, tamko kuhusu masuala ya haki za binadamu au kutuma ujumbe wa kiraia yaamuliwe kwa kura ya wingi maalum (qualified majority). Wingi huo hupatikana pale angalau mataifa 15 wanachama yanapounga mkono, yakiwa yanawakilisha angalau asilimia 65 ya idadi ya watu wa EU. Hata hivyo, kunahitajika pia kinga ya kisheria inayolinda maslahi ya msingi ya kitaifa kwa kila mwanachama. Mapendekezo ya aina hii, hata hivyo, yatalazimika kuidhinishwa na wakuu wote 27 wa nchi wanachama.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa EU, baadhi ya mataifa ndani ya kundi hilo pia yanataka mijadala iendelee hadi kwenye siasa za kodi, ili kulegeza pia kanuni ya uamuzi kwa kauli moja katika eneo hilo. Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, naye aliunga mkono wito wa mageuzi hayo katika hotuba yake ya hali ya Umoja mapema Septemba. Alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kujiondoa kwenye "pingu za maamuzi ya kauli moja” katika baadhi ya maeneo, ili kuepuka vizuizi vya mara kwa mara.
Mabadiliko yanawezekana, lakini si jambo la uwezekano mkubwa
Njia nyingine ya kulegeza kanuni ya uamuzi kwa kauli moja ndani ya Umoja wa Ulaya ni kupitia mabadiliko ya mikataba ya EU, kwa mfano wakati wa kupokea mwanachama mpya, anaeleza Nicolai von Ondarza. Hata hivyo, mchakato huo unahitaji ridhaa ya nchi wanachama wote 27. Kwa sasa, mwanasayansi huyo wa siasa anasema kuwa idhini hiyo "kisiasa haiwezekani.”
Iwapo mataifa wanachama yatafanikisha kukuza zaidi kundi la marafiki, yanaweza kuongeza shinikizo dhidi ya wenzao na hatimaye kusukuma maamuzi ya wingi (majority voting) kupitishwa siku za baadaye. Hata hivyo, von Ondarza anatahadharisha kwamba Hungary huenda ikaendelea kudai gharama kubwa ili kuachia chombo chake cha nguvu — kura ya turufu.
Hata mjini Brussels, kundi la marafiki linaonekana kama chombo cha kuongeza shinikizo, kwa mujibu wa mwanadiplomasia wa EU aliyezungumza na DW. Hungary, anasema, inazidi kujikuta peke yake. Wakati huohuo, Tume ya Ulaya inafanya kazi juu ya mpango wa kutumia mali za Urusi zilizozuwiwa kufadhili ujenzi upya wa Ukraine. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Tume hiyo tayari inatafuta njia za kukwepa kura ya turufu ya Hungary mapema iwezekanavyo.