1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya kifo yatishia kuligawa baraza kuu la Umoja wa Mataifa

Josephat Charo1 Novemba 2007

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 192 linatarajiwa kuipigia kura hukumu ya kifo, pengine mwanzoni au katikati ya mwezi huu wa Novemba. Hukumu ya kifo inaelezwa kuwa swala tete la kisiasa linalosababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/C7fn
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York MarekaniPicha: AP

Nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, zikiungwa mkono na karibu mashirika yote makubwa ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu, yatawasilisha pendekezo la mswada kuhusu hukumu ya kifo ambalo huenda likawagawanya baraza kuu la Umoja wa Mataifa katika makundi mawili.

Umoja wa Ulaya una hakika utapata wingi mdogo wa kura na hivyo pengine azimio lipitishwe ambalo lakini halitakuwa na mafungamano yoyote kisheria. Kuna upinzani mkali unaolikabili azimio hilo kutoka kwa muungano wa nchi za kiislamu, OIC, jumuiya ya nchi za kiarabu, China na nchi kadhaa katika eneo la Karibik na mataifa ya Asia, ambako adhabu ya kifo bado imo kwenye vitabu vya sheria.

Singapore ambayo imekuwa ikiunga mkono hukumu ya kifo inadhani pendekezo la Umoja wa Ulaya litaligawa baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Balozi wa Singapore katika Umoja wa Mataifa, Vanu Gopala Menon, anasema ikiwa Umoja wa Ulaya utaliwasilisha pendekezo hilo la azimio, litapingwa na nchi nyingi ambazo zina hukumu ya kifo katika sheria zao na ambazo zina maoni kwamba hukumu ya kifo haihusiani na haki za binadamu bali ni swala linalohusu sheria na utengamano.

Menon amesema na hapa ninamnukulu, ´Tukizingatia hali hii ingekuwa bora kwa Umoja wa Ulaya kutoliwasilisha pendekezo lake,´ mwisho wa kumnukulu balozi huyo wa Singapore. Balozi Menon amehoji kwamba azimio la aina hiyo litavuruga mambo ndani ya kamati ya tatu itakayojadili na kulipigia kura azimio hilo kabla kuwasilishwa kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa na hatimaye kusababisha mgawanyiko usiohitajika katika baraza hilo.

Balozi Menon wa Singapore amesema haijabainika wazi kwake ni lengo gani Umoja wa Ulaya inalotaka kulitimiza kupitia azimio lake hilo. Huenda likaupa hisia za kutosheka kimaadili lakini halitabadili misimamo ya nchi zinazounga mkono kwamba hukumu ya kifo inafaa kuzuia uhalifu mkubwa. Menon ameonya kwamba hatua ya Umoja wa Ulaya kulazimisha maadili pia itaonekana kama hujuma na nchi nyingi.

Afisa wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaja jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba pendekezo la azimio hilo limetayarishwa na nchi 36 zikiwemo nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Lakini akaongeza kuwa nchi zinazolidhamini azimio hil0 zinakaribia 70.

Alipoulizwa ikiwa Umoja wa Ulaya una hakika ya kupata kura nying1 miongoni mwa wanachama 192 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, afisa huyo amesema ni vigumu kubashiri kwa sababu pendekezo la azimio hilo bado linajadiliwa na halijakamilika.

Mwanadiplomasia mmoja wa kiarabu anayelipinga azimio hilo la Umoja wa Ulaya amesema amesikia kuwa baadhi ya wanachama wa umoja huo hawaridhishwi na azimio hilo na wametaka lifanyiwe mabadiliko. Hatua hiyo imechelewesha kuwasilishwa kwa azimio hilo kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Lakini katika Umoja wa Ulaya kuna mgawanyiko ikiwa unatakiwa kuruhusu mabadiliko yaliyopendekezwa na nchi zinazolidhamini azimio hilo ambazo si wanachama wa umoja huo. Mwanadiplomasia huyo wa kiarabu amesema pia kuna tetesi za mkakati wa kutafuta uungwaji mkono kutumia diplomasia ya malipo.

Kwa kuwa pendekezo la azimio hilo bado linajadiliwa, Umoja wa Ulaya bado haujaliwasilisha rasmi hivyo kuzusha wasiwasi zaidi na kuwaacha wanachama wengine wakibahatisha vipengele vilivyojumulishwa katika azimio hilo.