Gaza yawazika Wapalestina waliouwawa | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Gaza

Gaza yawazika Wapalestina waliouwawa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaendelea na mkutano wa dharura kujadili mgogoro wa Gaza wakati ambapo maelfu ya wakaazi wa Gaza Jumanne ya leo wafanya mazishi ya Wapalestina waliouawa na wanajeshi wa Israeli

Miili kadhaa ya Wapalestina waliouwawa ilipitishwa kwenye mitaa ya Ukanda wa Gaza kabla ya kupelekwa makaburini kwa kwa ajili ya mazishi. Takriban watu 61 waliuawa na majeshi ya Israeli wakati wa maandamano ambapo Wapalestina 35 walizikwa hapo jana Jumatatu, siku mbaya zaidi  itakayokumbukwa katika Ukanda wa Gaza tangu vita vya mwaka 2014 kati ya Israeli na kundi la Hamas. Nchi mbali mbali zinaendelea kutoa miito ya kufanyika kwa uchunguzi huru baada ya kutokea vurugu hizo zilizosababisha watu kuuwawa.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema Ujerumani inaunga mkono hatua ya kufanyika uchunguzi huru baada ya Marekani kuzuia taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inayotaka kufanyike uchunguzi huo. Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imemuamuru balozi wa Israeli nchini humo kundoka kwa muda katika hatua ya kupinga mauaji ya mjini Gaza. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani mauaji ya Wapalestina.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert (picture-alliance/dpa/K. Nietfeld)

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert

Uturuki, ni mkosoaji  mkubwa wa vurugu za huko Gaza na pia hatua ya kufunguliwa kwa Ubalozi mpya wa Marekani huko Jerusalem. Erdogan ameitisha mkutano wa dharura wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu siku ya Ijumaa, na amesema pia nchi yake itawaita mabalozi wake kutoka Washington na Tel Aviv kwa mashauriano zaidi.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, amesema vurugu hizo mjini Gaza zimeuvuruga zaidi mchakato wa amani. Msemaji huyo amesema Uingereza ina wasiwasi sana na kiwango cha vurugu na watu kupoteza maisha huku idadi kubwa ya Wapalestina wakiwa wamejeruhiwa, na kutoa wito kwa pande zote kujiepusha na vurugu zaidi.

Wizara ya mambo ya nje ya Ireland pia imemwita balozi wa Israel nchini mwake kuelezea mshtuko na mfadhaiko wao kutokana na umwagikaji damu kwenye Ukanda wa Gaza. Saudi Arabia imesema inapinga uamuzi wa Marekani wa kuuhamishia ubalozi wake katika mji wa Jerusalem kutoka Tel Aviv. Taarifa hiyo ilmechapishwa kwenye shirika la habari la taifa (SPA).

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarifr (Getty Images/AFP/A. Kenare)

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif

Miongoni mwa nchi zilizo laani mashambulio hayo ni Iran ambapo msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje Bahram Ghasemi amesema Maafisa wa Israeli wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kivita kutokana na mauaji hayo ya kikatili dhidi ya waandamanaji wa Gaza.

Mwandishi:Zainjab Aziz/RTRE/DPAE/AFPE/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com