Friedrich Merz afanya ziara ya kwanza nchini Uhispania
18 Septemba 2025
Ingawa uhusiano kati ya Ujerumani na Uhispania kwa ujumla unazingatiwa kuwa mzuri, lakini kuna tofauti kubwa kati ya nchi hizo mbili kuhusiana na msimamo juu ya Israel.
Wakati Merz, yuko sawasawa na Sánchez, wote wanalikosoa vikali jeshi la Israel katika Operesheni yake kwenye Ukanda wa Gaza, Ujerumani hata hivyo hadi sasa imekataa swala la kuiwekea vikwazo Israel, lakini inaunga mkono juu ya kuzuia uuzaji wa silaha kwa Israel. Kinyume chake, Uhispania ilichukua hatua madhubuti mapema katika mzozo huo wa Gaza.
Mnamo mwaka jana wa 2024,Uhispania ilikuwa mwanachama wa kwanza wa nchi za Umoja wa Ulaya kujiunga na Afrika Kusini katika kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alitangaza vikwazo na marufuku kamili ya silaha kwa wote wanaohusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari, ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita huko Gaza.
Hatua kama hizo za vikwazo dhidi ya Israedl zimependekezwa na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula Von der Leyen ambaye siku ya Jumatano alisema makubaliano ya biashara huria yanapaswa kubatilishwa, na mawaziri pamoja na walowezi wa Israel wenye itikadi kali wachukuliwe hatua za kuwaadhibu.
Kwa mtazamo wa Tume ya Ulaya, Israel inakiuka haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu kutokana na operesheni ya jeshi lake ambayo imesababisha janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Hata hivyo serikali ya Ujerumani chini ya kansela Friedrich Merz bado hajatamka juu ya msimamo wake kuhusu mapendekezo hayo.
Kinachoendelea huko Gaza, maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuondoka kutoka kwenye mji wa Gaza City kutokana na mashambulizi ya Israel. Watu zaidi ya 16 wameuawa huku umeme ukikosekana katika sehemu kubwa ya mji huo baada ya Israel kushambulia miundombinu muhimu.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel katika eneo la kaskazini mwa Gaza yamesababisha hospitali kulemewa katika kutoa huduma na kwamba hospitali hizo zinaelekea kushindwa kabisa kutoa huduma za afya. Ghebreyesus ametoa mwito wa kukomeshwa hali hii inayokiuka ubinadamu.
Wakati huo huo, Mwendesha mashtaka mkuu wa Uhispania, Alvaro Garcia Ortiz amesema nchi hiyo itachunguza "ukiukwaji wa haki za binadamu huko Gaza" ili kuisaidia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ambayo inataka kutoa waranti wa kukamatwa maafisa wa Israel kwa madai ya uhalifu wa kivita.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Uhispania, ametoa amri ya kuundwa kikosi kazi kitakachopewa jukumu la kuchunguza ukiukaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu huko Gaza.
Vyanzo: DPA/AFP