1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Wataalam wa UN: Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza

17 Septemba 2025

Tume ya wataalamu huru walioteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wametoa ripoti rasmi, wakihitimisha kuwa Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

https://p.dw.com/p/50XNb
Krieg in Nahost | Israelische Angrife auf Gaza Stadt | Al Ghafari-Turm
Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Ripoti hiyo, iliyotolewa Septemba 16, 2025, imesema Israel imefanya vitendo vinne kati ya vitano vinavyotambuliwa kimataifa kama mauaji ya kimbari, katika mzozo wake na Hamas ikiwemo:

Kuua raia kwa makusudi, kusababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili, kuweka mazingira yanayolenga kuangamiza kundi la watu na kuzuia kwa makusudi huduma za afya na misaada ya kibinadamu.

Tume hiyo iliyoongozwa na mkuu wa zamani wa haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay, imeutuhumu uongozi wa Israel kuchochea kadhia hiyo.

"Mauaji ya kimbari yanafanyika Gaza na yanaendelea kufanyika na taifa la Israel ndilo linafanya hayo. Tumewataja watu watatu kwenye ripoti hii, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi wa zamani Yoav Gallant, na Rais Isaac Herzog, ambao matamshi yao yalichochea mauaji ya kimbari," amesema Pillay.

Israel imeikataa ripoti hiyo, ikiitaja kuwa ya "upotoshaji na uongo.”

Israel ilianza vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas baada ya Kundi hilo linalotajwa kuwa la kigaidi na Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya kushambulia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023na kuua watu 1,200 na kuwashika mateka zaidi ya 250.