Chanjo ya Covid-19 yaleta ahueni Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Chanjo ya Covid-19 yaleta ahueni Israel

Israel imeanza leo (21.02.2021) kuondoa sehemu kubwa ya vizuizi ilivyoweka kukabiliana na janga la virusi vya corona na kuruhusu kufunguliwa kwa shughuli za uchumi.

Israel Jerusalem | Markt

Shughuli za manunuzi zinaendelea kufunguliwa Israel

Hatua hiyo inafuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye kampeni yake ya taifa ya kutoa chanjo na vizuizi vikali vilivyosaidia kupunguza kiwango cha maambukizi.

Sehemu kubwa ya shule za msingi na sekondari zimefunguliwa baada ya kufungwa kwa karibu miezi miwili. Majumba ya makumbusho, maktaba, maduka makubwa ya mahitaji ya nyumbani na masoko pia yamefunguliwa.

Mfumo mzima wa elimu ya nchi hiyo unatarajiwa kufunguliwa mapema mwezi Machi.

Majumba ya mazoezi, mabwawa ya kuogelea, kumbi za sinema na mikahawa imeruhusiwa kufunguliwa kwa watu waliokwishapatiwa dozi mbili za chanjo ya virusi vya corona.

Hata hivyo vizuizi vinavyopiga marufuku watu wengi kukusanyika bado vinaendelea kutekelezwa.

Maisha ya kawaida yanaanza kurejea polepole

Kuelekea kufungua shughuli za uchumi, nchi hiyo imetangaza mpango wake wa kuwaruhusu wote waliochanjwa kikamilifu  kuhudhuria matamasha ya kitamaduni, kusafiri nje ya nchi pamoja na kuhudumiwa kwenye migahawa.

Weltspiegel 19.02.2021 | Corona | Israel Tel Aviv | Impfung

Chanjo inatolewa popote nchini Israel kuharakisha kampeni ya kuwachanja watu wengi

Chini ya mpango huo programu maalum inayotumia simu ya mkononi imebuniwa na kila mtu aliyetimiza masharti yaliyowekwa ataitumia kama kibali cha kumruhusu kufanya shughuli hizo.

Hadi kufikia sasa Israel imetoa dozi ya kwanza ya chanjo ya kampuni ya Pfizer/BioNTech kwa zaidi ya nusu ya raia milioni 9.3 wa taifa hilo. Raia wengine karibu milioni 3 tayari wamepatiwa dozi ya kwanza ya chanjo hiyo.

Hapo jana, serikali ya Israel ilisema chanjo ya Pfizer/BioNTech inatoa kinga ya asilimia 95.8 na kusaidia kupunguza uwezekano wa mtu kufa au kulazimika kulazwa hospitali kutokana na virusi vya corona.

Kadhalika chanjo hiyo inatoa kinga ya asilimia 98 dhidi ya mtu kupata homa au matatizo ya kupumua.

Taifa hilo hadi sasa limerekodi visa 743,000 vya maambukizi ya Covid-19 na ina vifo 5,521 tangu kuzuka kwa ugonjwa huo mwaka jana.

Na hatua tatu tofauti ya kuweka vizuizi vya kukabiliana na ugonjwa  huo imesababisha kudorora kwa uchumi na zaidi ya asilimia 20 ya watu kukosa ajira.

Uingereza na Ujerumani mapambano yanaendelea

London | Boris Johnson, Pressekonferenz zum Coronavirus

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson

Kwengineko, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameahidi kuwa kila mtu mzima nchini humo atapaswa kuwa amepatiwa chanjo ya virusi vya corona kabla ya mwisho wa mwezi Julai.

Utoaji wa chanjo hiyo kwa watu wengi utasaidia kuyanusuru makundi ya watuw alio kwenye hatari ya kuambukizwa na vilevile kuruhusu kulegezwa kwa vizuizi vilivyowekwa kukabiliana na janga la COVID-19.

Nchini Ujerumani, idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imepanda kwa visa vipya 7,676 na kufanya idadi jumla kufikia 2,386,559. Hayo ni kulingana na taasisi ya kuzuia magonjwa ya kuambukizwa ya Robert Koch.

Mpango wa utoaji chanjo wa nchi hiyo uko mashakani kutokana na baadhi ya watu kukataa chanjo ya AstraZeneca inayotengenezwa Uingereza.

WHO: Tanzania inapaswa kuwajibika kupambana na COVID-19

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli

Rais John Magufuli wa Tanzania

Huko barani Afrika serikali ya Tanzania imehimizwa kuchukua hatua za makusudi kupambana na janga la virusi vya corona katika wakati wasiwasi unaongezeka kuwa maambukizi yanashamiri.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni,Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema WHO haijapokea taarifa yoyote kutoka Tanzania juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na janga la corona.

Tedros amesema kwenye taarifa yake kwamba hali hiyo inatia wasiwasi na ameitolea wito serikali ya Tanzania kuanza kuratibu zoezi la kutoa data kuhusiana na COVID-19 nchini humo.

Mkuu huyo wa WHO amesema, mwishoni mwa mwezi Januari alishirikiana na kiongozi wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti, kuihimiza Tanzania kuongeza jitihada kwenye hatua za kiafya dhidi ya COVID-19 na kujiandaa na kutoa chanjo.

Ameitaka Tanzania kuchukua hatua za kuwalinda raia wake na watu wengine ndani na nje ya nchi hiyo.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Sudi Mnette