1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Tanzania yazipiga marufuku taasisi kuzungumzia Corona

George Njogopa10 Februari 2021

Serikali ya Tanzania imezipiga marufuku taasisi kutoa matangazo ya tahadhari kuhusiana na uwepo wa janga la covid-19, baada chuo kimoja kutoa waraka unaowatahadharisha wanafunzi kuhusu maambukizi ya virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3p9mY
Tansania Dar es Salaam | Grafitty zu Corona
Picha: Eric Boniphace/DW

Ikifutilia mbali tangazo la tahadhari la makamu mkuu huyo wa chuo, serikali imewataka wakuu wote wa vyuo nchini kujiweka kando na utoaji wa matangazo ya aina hiyo na badala yake imewahimiza kuendelea kufuata miongozo ya serikali kuhusu udhibiti wa janga hilo linaloendelea kugonga vichwa vya habari duniani kote.

Soma pia: COVID-19: Uingereza yapiga marufuku abiria kutoka Tanzania

Katika taarifa yake ya tahadhari kwa jumuiya ya wanafunzi makamu mkuu wa chuo kikuu huria, Profesa Elifasi Tozo Bisanda pamoja na kubainisha tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na jumuiya hiyo lakini pia alionyesha wasiwasi wake kuhusiana na vifo vilivyojitokeza hivi karibuni vikiwahusisha pia wasomi kadhaa wa vyuo vikuu.

Aliwatahadhari pia wale wanaokusudia kusafiri nje ya nchi katika kipindi hiki akisema siyo salama kufanya hivyo kutokana na janga hilo. Bila kukawia, serikali imelipuuza tangazo hilo huku ikiwaondolewa wasiwasi wanafunzi kwa kuwataka kuendelea na masomo yao ya kawaida.

Tansania Dar es Salaam | Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akihutubia taifa wakati wa sala ya kitaifa dhidi ya virusi vya corona jijini Dar es Salaam, Aprili, 22, 2020.Picha: Tanzania Presidents Office

Taarifa iliyotolewa na serikali inasema " wizara inatoa onyo kwa viongozi na watumishi wizara ya elimu, sayansi na teknolojia pamoja na taasisi zake kuacha kutumia nembo za serikali wanapotoa maoni yao binafsi.” 

Soma pia: Tanzania haina mpango wa kuikubali chanjo ya corona

Tangu kuzuka kwa kile kinachosemwa wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona, kumeshudiwa taasisi mbalimbali zikitoa waraka wa tahadhari ikiwamo ule wa mwanzo kabisa uliotolewa kanisa katoliki kwenda kwa waumini wake na kufuatiwa na makanisa mingine kadhaa.

Vifo visivyothibitishwa chanzo chake

Vyuo vya elimu ya juu ambavyo hukusanya idadi kubwa ya wanafunzi, navyo pia vimekuwa sehemu ya taasisi zinazotoa waraka wa namna hiyo wenye lengo la kuwaasa wanafunzi na jamii juu ya tahadhari wanazopaswa kuchukua wakati huu.

Maoni ya Watanzania juu ya Covid 19 na chanjo yake

Wakati hayo yakiendelea, kumekuwa na taarifa za vifo zinazoendelea kuripotiwa kila uchao katika maeneo mbalimbali ya nchini. Ingawa hakuna mamlaka zozote zinazothibitisha juu ya kile kinachosababisha vifo hivyo, lakini ripoti nyingi zinasema wengi wao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kile kinachojulikana sasa kama tatizo la kupumua.

Soma pia: SADC yawataka wanachama kujihadhari na corona

Kwa sasa kumekuwana mitazamo tofauti kuhusiana na hali hii inayoendelea, na mchambuzi Sammy Ruhuza anasema kuna haja ya kuvunja ukimya. Kwa ujumla kumekuwa na hali ya sintofahamu inayoshuhudiwa kutoka kwa baadhi ya wananchi na baadhi yao wameanza kumiminika kwa wingi katika maduka kwa ajili ya kupata dawa za asili.

Kumekuwa na wasiwasi pia namna ya matumizi ya dawa hizo ambazo wengi wao huzitumia kupita kiasi jambo ambalo wataalamu wanatahadharisha juu ya uwezekano wa kuathiri afya ya mwili.