Chama cha Kijani chajikuta pabaya kwa kuchelewesha Mercosur
28 Januari 2026
Inaonekana wazi kwa mwenyekiti mwenza wa chama cha Kijani (Grüne), Franziska Brantner, jinsi mjadala huu unavyomkera: mwanzoni mwa wiki anasimama mbele ya waandishi wa habari mjini Berlin. Brantner angependa sasa kuzungumzia mada za sasa, migogoro ya kisiasa ya kimataifa, Greenland na Ukraine, pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump.
Lakini waandishi wa habari wanarudi tena kuzungumzia Mkataba wa Mercosur, mkataba mkubwa wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya na nchi nne za Amerika Kusini—Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay. Mkataba ambao unapaswa kuwa ishara ya matumaini katika dunia inayozidi kukumbwa na utaifa mkali. Ishara ya biashara inayozingatia kanuni, si ushuru wa adhabu. Mazungumzo kuhusu mkataba huu yalichukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka 20.
Hata hivyo, katika Bunge la Ulaya, kuanza kutekelezwa kwake kulicheleweshwa tena wiki iliyopita—kwa kura za wengi wa wabunge wa Kijani kutoka Ujerumani. Na hilo lilitokea licha ya Brantner mwenyewe kujaribu hadi dakika za mwisho kuwashawishi wanachama wenzake wa chama chake huko Brussels waunge mkono mkataba huo.
Sasa mwenyekiti huyo mwenza anasema, licha ya ukaguzi wa kisheria unaochukua muda mrefu ambao uliidhinishwa kwa kura za chama chake, mkataba huo bado unaweza kuanza kutekelezwa: "Mara tu nchi moja ya Amerika ya Kusini itakaporidhia, Rais wa Tume, Ursula von der Leyen, ana mamlaka na pia tayari amepewa jukumu la kuanza kuutekeleza ipasavyo.” Aidha, "wenzake” katika Bunge la Ulaya tayari wamesema wenyewe kuwa mwenendo wao wa kupiga kura ulikuwa kosa.
Kura ya pamoja ya Kijani na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia
Na hivi ndivyo kosa hilo walilolikiri lilivyojitokeza: Wabunge wanane kati ya kumi na moja wa Kijani kutoka Ujerumani walipiga kura katika Bunge la Ulaya wiki iliyopita kuomba mkataba wa Mercosur uliokwishajadiliwa kikamilifu ukaguliwe tena na Mahakama ya Ulaya.
Kwa maoni ya wataalamu wengi, hatua hiyo inaweza kuchukua miaka kadhaa na kuchelewesha kwa kiasi kikubwa kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo muhimu. Na jambo nyeti zaidi: Kijani walipiga kura pamoja na wahafidhina wa mrengo wa kulia na wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika Bunge la Ulaya ili kulifikisha suala hilo mahakamani.
Hili ni jambo linalokinzana na msimamo wa awali wa Kijani wa Ujerumani, ambao walipinga kwa sauti kubwa zaidi pale CDU na CSU walipowasilisha, kabla ya uchaguzi wa Bundestag mwaka jana, hoja ya kudhibiti uhamiaji kwa kushirikiana na chama cha "Alternative für Deutschland” (AfD), ambacho baadhi ya mitazamo yake inachukuliwa kuwa ya mrengo wa kulia uliokithiri. Wakati huo, Kijani walisisitiza umuhimu wa "ukuta wa moto” dhidi ya wahafidhina wa mrengo wa kulia bungeni—yaani kutokuwepo kabisa kwa kura au ushirikiano nao. Lakini sasa, katika Bunge la Ulaya, ni Kijani wenyewe waliokiuka msimamo huo.
Wadephul: "Pigo kubwa kwa mkataba”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, naye alikikosoa chama hicho cha upinzani: "Yeyote anayezungumzia ukuta wa moto lazima awe tayari kuutimiza mwenyewe. Katika wiki hii, Kijani katika Bunge la Ulaya wameshindwa kufanya hivyo,” alisema mwanasiasa huyo wa CDU siku chache zilizopita katika redio ya Deutschlandfunk.
Aliongeza kuwa nchi nyingine, kama India, zinaangalia kwa makini "kama tuna uwezo wa kujadili mikataba kama hii na kisha kuipitisha kisiasa katika taasisi zote husika.” Kura ya Bunge la Ulaya, alisema waziri huyo, ni pigo kubwa kwa mkataba huo.
Chama cha Kijani, kinachojulikana kwa msimamo wake wa kulinda mazingira, kimekuwa kikikosoa Mkataba wa Mercosur tangu awali. Je, viwango vya juu vya ulinzi wa mazingira kwa wakulima wa Ujerumani vitaendelea kudumishwa iwapo watalazimika kushindana katika soko huria na wakulima kutoka Argentina, Paraguay, Uruguay na Brazil?
Wanachama wengi wa Kijani wameendelea kuwa na wasiwasi. Hata hivyo, kiongozi wa kundi la Kijani katika Bundestag, Britta Haßelmann, aliweka wazi hoja yake siku chache zilizopita: katika nyakati za kuongezeka kwa utaifa, mkataba wa aina hii kati ya mataifa mengi tayari una thamani yake yenyewe. "Ni muhimu kwa Ulaya na pia kwa Ujerumani kufanya hivi, ili kuonyesha kuwa sisi kama Ulaya tuna uwezo wa kuanzisha mikataba ya haki ya kibiashara na mataifa mengine,” alisema.
Kijani barani Ulaya sasa wataka kuridhia haraka
Kwa hiyo, athari hasi kwa Kijani ni kubwa zaidi sasa. Hata wakosoaji ndani ya chama wanalaumu uongozi wa chama huko Berlin kwa kushindwa kuratibu vya kutosha na wabunge wao mjini Brussels. Uongozi wa chama umejitokeza tena kuthibitisha uungaji mkono wake kwa mikataba mingine ya kibiashara, kwa mfano na nchi za kile kinachoitwa Ushirikiano wa Trans-Pasifiki, unaojumuisha Australia, Japan, Kanada, Mexico na mataifa kadhaa ya Asia ya Kusini Mashariki.
Pia na India, kama alivyoongeza mwenyekiti mwenza mwingine wa Kijani, Felix Banaszak, siku ya Jumatatu: "Ushirikiano wa kina na India, mkataba wa aina hii wa biashara huria, pia uko katika maslahi yetu. Na muwe na uhakika: Kijani katika Bunge la Ulaya hawataangalia kila koma.”
Mkataba wa Mercosur unalenga kuunda moja ya maeneo makubwa zaidi ya biashara huria duniani. Wakati Ulaya watakuwa wakisafirisha bidhaa kama magari na bidhaa za kemikali kuvuka Atlantiki, nchi za Mercosur zitakuwa zikiuza hasa mazao ya kilimo na malighafi kwenda Ulaya. Uchumi wa Ujerumani unatarajia ongezeko kubwa la mauzo ya nje kutokana na mkataba huo. Aidha, mkataba huu unaonekana kama ishara ya kujitegemea zaidi kutoka kwa Marekani.