1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU, Mercosur kuunda kanda kubwa zaidi ya biashara duniani

Iddi Ssessanga
30 Desemba 2018

Umoja wa Ulaya na Japan zitakuwa eneo kubwa zaidi la bishara duniani hivi karibuni. Lakini rekodi hii itadumu kwa muda mfupi wakati EU ikifkuzia makubaliano na Mercosur ya Amerika Kusini, yanayotarajiwa kusainiwa 2019.

https://p.dw.com/p/3Am9c
Argentinien Container im Hafen von Buenos Aires
Picha: picture-alliance/dpa/A. Perez Moreno

Baada ya makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Japan kuanza kutekelezwa Febuari mosi, umoja huo unapanga kuelekeza juhudi zake katika kufanikisha makubaliano na kundi la Amerika Kusini la Mercosur kabla ya mwisho wa mwaka 2019, yatakayounda kanda kubwa zaidi ya kibiashara.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstroem katika mazungumzo na shirika la habari la Ujerumani DPA siku ya Jumamosi.

Eneo la Biashara la Mercosur linayajumlisha mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na Brazil, Paraguay, Uruguay, na Venezuela. Idadi jumla ya watu katika nchi hizo ni milioni 260.

Uanachama wa Venezuela hata hivyo umesimamishwa kwa muda tokea 2016, kutokana na rekodi yake ya haki za binadamu.

Iwapo mpango huo utakamilika, biashara ya pande zote mbili itaweza kuokoa mamilioni ya fedha za ushuru.

Cecilia Malmström
Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmström.Picha: picture-alliance/EPA/S. Lecocq

Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya na Mercosur wamekuwa wakifanyia kazi makubaliano ya biashara huria tangu mwaka 2000.

Mapema mwaka 2018, waziri wa mambo ya nje wa Argentina Jorge Faurie alisema makubaliano hayo yangekamilishwa kufikia mwezi Septemba, lakini mazungumzo yalionekana kusuasua katika miezi ya karibuni.

Moja ya sababu za kuchelewa ilikuwa ushindi wa Jair Bolsonaro, mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Brazil, Kamishna Cecilia Malmtroem aliiambia DPA Jumamosi.

Wakati Bolsonaro akijiandaa kuchukua madaraka mwezi Januari, serikali inayomaliza muda wake ilishindwa kutoa ahadi zozote kuhusu biashara.

Hata hivyo Malmstroem aliongeza kuwa hakukuwa na ishara kwamba serikali ya Bolsonaro itavuruga mazungumzo hayo. "Waziri mpya wa mambo ya nje alituambia kuwa atafurahi kufanikisha makubaliano na kwamba wataendeleza mazungumzo," alisema Malmstroem.

'Cognac' kutoka Cognac

Wakati Umoja wa Ulaya unatumai kuwa makubaliano hayo yatakuwa tayari kufukia mwishoni mwa mwaka 2019, Brussels bado inasisitiza kuhusu masuala kadhaa, ikiwemo mfumo wake wa kulinda majina ya vyakula - kama kuita aina moja tu maalumu ya jibini inayotengenezwa Ugiriki "feta" au kuruhusu vinywaji vinavyotengenezwa katika mji wa Ufaransa wa Cognac kubeba jina hilo.

Uruguay Mercosur-Gipfeltreffen in Montevideo
Wakuu wa mataifa yanayounda jumuiya ya Mercosur - Rais wa Paraguay Mario Abdo Benitez, rais wa Argentina Mauricio Macri, rais wa Uruguay Tabare Vazquez, rais wa Brazil Michel Temer na rais wa Bolivia Evo Marales.Picha: Reuters/A. Stapff

Huko nyuma Brussels imelalamika pia kuhusu uingizwaji mkubw awa nyama kutoka Amerika Kusini. Kwa upande mwingine, washirika wa Amerika Kusini wana wasiwasi kuhusu kufunguliwa zaidi kwa sekta yao ya magari.

Baada ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya Machi 2019, soko la pamoja la umoja huo litakuwa na wakazi karibu milioni 450. Kanda hiyo kubwa kiuchumi tayari ina makubaliano na mataifa kadhaa makubwa, yakiwemo Mexico na Canada.

Hata hivyo, mazungumzo juu ya kuunda eneo la pamoja la biashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya yamesitishwa baada ya Rais Donald Trump kuchaguliwa mwaka 2016.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW

Mhariri: Yusra Buwayhid