Bunge la Ujerumani lafunguliwa rasmi | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bunge la Ujerumani lafunguliwa rasmi

Bunge la Ujerumani Bundestag, limefunguliwa rasmi siku ya Jumanne, licha ya ukweli kwamba bado hakuna serikali, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

Muonekano wa jumla wa Bunge la Ujerumani, Bundestag.

Muonekano wa jumla wa Bunge la Ujerumani, Bundestag.

Kikao hicho cha wabunge 631 kinafanyika siku moja kabla Kansela Angela Merkel kuanza duru ya kwanza ya mazungumzo na chama kikuu cha upinzani cha SPD yenye lengo la kuunda serikali mpya ya mseto.Wabunge hao watakuwa na jukumu la kumchagua Spika wa Bunge, ambapo mwanasiasa wa chama cha CDU Norbet Lammert ana uhakika wa kuchaguliwa tena. Lammert mwenye umri wa miaka 64 amekuwa spika wa bunge hilo tangu mwaka 2005.

Mbunge mwenye umri mkubwa zaidi Heinz Reisenhuber, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha bunge.

Mbunge mwenye umri mkubwa zaidi Heinz Reisenhuber, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha bunge.

Mada za kwanza kujadiliwa
Kikao cha leo kinafunguliwa na mbunge wenye umri mkubwa zaidi, mwanasiasa wa chama cha CDU, Heinz Reisenhuber mwenye umri wa miaka 77, ambaye pia ndie aliefungua kikao cha kwanza cha bunge jipya la mwaka 2009. Wabunge pia wataamua ni manaibu wangapi atakuwa nao spika wa bunge. Katika muhula uliyopita, kila moja kati ya vyama vitano vilivyokuwa bungeni kilitoa naibu moja. Na wakati huu, ambapo vyama vya CDU, CSU na SPD ambavyo vitaingia mazungumzo ya kuunda serikali, vinataka vitoe manaibu wake, licha ya ukweli kwamba vitakuwa upande mmoja.

Mada nyingine itakayojadiliwa katika kikao hiki cha kwanza itakuwa juu ya haki za wapinzani wachache. Kama kutakuwepo na muungano mkuu, basi vyama vya Die Grüne na die Linke vitakuwa na jumla ya asilimia 20 tu ya wabunge wote. Haki muhimu za upinzani, kama vile udhibiti wa kamati za uchunguzi zimewekwa katika sheria ya msingi, lakini kwa sharti la kuwa na asilimia 25 ya wabunge.

Lakini mwanasiasa Reisenhuber hadhani kama upinzani utashindwa kufanya kazi yake ya kuiwajibisha serikali. Katika mahojiano na gazeti la Passauer Neuen Presse, Reisenhuber alisema anaamini kutakuwepo na upinzani wa kusisimua bungeni.

Upinzani imara
SPD kinataka kuimarishwa kwa mchango wa vyama vya Die Grüne na die Linke bungeni, iwapo itaundwa serikali ya muungano mkuu. Katibu wa bunge Thomas Opperman kutoka chama cha SPD, aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa demokrasia haihitajji tu serikali imara, bali pia upinzani imara, na kuongeza kuwa upinzani unapaswa kuwezeshwa ili kuiwajibisha serikali ipasavyo.

Kansela Angela Merkel, katikati ya viongozi wa wabunge wa CDU na CSU, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha bunge.

Kansela Angela Merkel, katikati ya viongozi wa wabunge wa CDU na CSU, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha bunge.

Jioni ya leo, rais wa Ujerumani Joachim Gauck anatarajiwa kuivunja rasmi serikali ya Kansela Merkel iliyokuwa inaundwa na vyama vya CDU/CSU kwa kushirikiana na chama cha Kiliberali FDP, kufuatana na sheria. Lakini serikali hiyo itaendelea kubaki madarakani hadi bunge litakapomuidhinishamkuu mpya wa serikali baada ya kuundwa.

Mwafrika wa kwanza bungeni
Kwa mara ya kwanza bunge la Ujerumani litakuwa na mbunge mwenye asili ya Afrika , Karamba Diaby, mzaliwa wa Senegal kutoka chama cha SPD. Mbunge mdogo zaidi ni Mahmut Ozdemir pia kutoka SPD mwenye umri wa miaka 26, na mzee zaidi bungeni ni Heinz Reisenhuber, aliezaliwa mwaka 1935.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpa, dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com