Amani ndilo jambo la msingi - Al-Bashir | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Amani ndilo jambo la msingi - Al-Bashir

Licha ya watu wa Sudan ya Kusini kumpokea Rais Omar Hassan al-Bashir kwa mabango yanayounga mkono kujitenga kwa eneo lao, mwenyewe ameapa kuheshimu maamuzi yoyote watakayoyatoa hapo Jumapili ijayo kuhusu hatima yao.

Maandamano ya kushajiisha kura ya maoni kwenye eneo la Sudan ya Kusini

Maandamano ya kushajiisha kura ya maoni kwenye eneo la Sudan ya Kusini

Rais Omar Hassan Al-Bashir amewasili mjini Juba, Kusini mwa Sudan, na ujumbe wa amani. Na hakuna wakati ambao amekuwa muwazi na kuzungumza moja kwa moja kama leo. Kwa maneno makavu na yasiyo na njia za kuzungukazunguka, aliwaambia viongozi wa Sudan ya Kusini alipokutana nao mjini Juba kwamba umoja wa kweli baina ya watu, huwa hauji kwa kutumia nguvu, bali ni jambo la hiari na la kimaumbile.

Kwa hivyo, hata kama Jumapili ijayo (9 Januari 2011), Wasudan ya Kusini wataamua kujitenga na kuunda taifa leo, Kaskazini itaheshimu uamuzi huo na wala huo hautakuwa mwisho wa udugu uliopo kati yao baina yao.

"Tunaamini kwamba umoja wa kuulazimisha kwa nguvu umeshindwa, japokuwa tunakubali pia kwamba umoja ndio njia bora ya kuhakikisha maendeleo, utulivu na ustawi wa watu wote wa Sudan." Amesema Al-Bashir.

Darfur

Darfur

Hotuba hii ya leo inaonekana kama kauli ya mwisho ya al-Bashir kwa wakaazi wa Sudan ya Kusini, ambao, ikiwa Jumapili ijayo wataamua kujitenga, kama inavyotabiriwa na wengi, basi taifa jipya litazaliwa na watasita kuwa raia wake siku chache zijazo.

Katika namna ya kiongozi anayelilia hatima ya taifa lake, al-Bashir alizungumza kwa hisia kali, kwa mifano, na kwa nasaha nyingi mbele ya mwenzake wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir, pamoja na wanasiasa wa ngazi za juu wa eneo hilo, lakini alichagua maneno yanayoashiria amani badala ya visasi.

Al-Bashir alipuuzia kabisa uwezekano wa kuzuka tena kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, akisema kwamba tayari wa Kusini na Kaskazini walishajifunza kwamba vita sio suluhisho la matatizo yao, bali amani ndio lengo la kila mmoja wao.

"Tunaweza kuuonesha ulimwengu kwamba sisi ni watu tuliostaarabika, na kwamba tunafanya mambo yetu kistaarabu. Hatutairuhusu tena Sudan hii kurudi kwenye vita." Amesema Al-Bashir.

Takribani wapiga kura milioni nne wa Sudan ya Kusini wanatarajiwa kwenda kwenye visanduku vya kura Jumapili ijayo, lakini wachambuzi wa mambo wanasema, tayari wapiga kura hao wameshafanya uamuzi wa kujitenga.

Hata hivyo, bado kuna mambo ya kimsingi ambayo hayajafikiwa muafaka kati ya Kaskazini na Kusini, likiwemo suala la uraia, mapato ya mafuta, mustakbali wa jimbo la mpakani lenye utajiri wa mafuta la Abyei na namna ya kuligawa deni la dola bilioni 38 la Sudan.

Hotuba ya leo (4 Januari, 2011) ya al-Bashir inakwenda sambamba na ile aliyoitoa mwisho wa mwaka uliopita, ambayo ilisisitiza juu ya kuyatambua na kuyaheshimu maamuzi ya watu wa Kusini. Hotuba hii inatajwa kwamba ilimpatia sifa kwa watu Sudan ya Kusini na tangu hapo mwangwi wa maneno yake umekuwa masikioni mwa watu.

Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Barnaba Marial, aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba wangelimpa mapokezi makubwa Rais Bashir, kwani anastahiki kutokana na hotuba yake hiyo ya mwisho wa mwaka.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFPE

Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ztZs
 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ztZs
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com