1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Bashir kulitambua dola la Sudan ya Kusini

4 Januari 2011

Siku tano tu kabla ya kupigwa kura itakayoamua hatima ya Sudan ya Kusini, Rais Omar Al Bashir wa Sudan amewasili mjini Juba, akiahidi kuwa udugu wa Wasudan hautamalizika hata kama Kusini itaamua kuunda taifa lake.

https://p.dw.com/p/ztKh
Rais Omar Hassan Al-Bashir wa Sudan: Vyovyote ndugu zangu wa Kusini mutakavyoamua, sisi ni ndugu wa milele
Rais Omar Hassan Al-Bashir wa Sudan: Vyovyote ndugu zangu wa Kusini mutakavyoamua, sisi ni ndugu wa milelePicha: DW/AP

Ahadi ya Rais Omar Hassan Al Bashir kwa watu wa Sudan ya Kusini, iko wazi: vyovyote watakavyoamua hapo Jumapili ya tarehe 9 Januari 2011, yeye hatawakasirikia wala kuwagomea. Ni ndugu zake na wataendelea kuwa hivyo milele. Ndivyo alivyowaambia viongozi wa Sudan ya Kusini leo hii (4 Januari 2011) katika mkutano wao wa mjini Juba.

"Ili kuliondoa tatizo la Wasudan, ni kukiondoa chanzo cha tatizo hilo, ambalo ni vita. Sudan kamwe haitarudi tena kwenye vita. Tutakuwa nanyi, tutawaunga mkono, hata kama dola mpya itaanzishwa. Watu wote wa Sudan, Kusini na Kaskazini, tumejitolea na tunafungwa na ahadi yetu ya kujenga amani na kuleta maendeleo. " Ameahidi Al Bashir.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na kiongozi wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir, Al Bashir alisema wazi kwamba yeye, kama kiongozi wa Sudan hana kinyongo chochote kama watu wa Sudan ya Kusini wataamua kuanzisha taifa lao katika kura ya Jumapili ijayo, akisisitiza kwamba kuwa wamoja, hakumaanishi kuwa nchi moja.

"Tunakubali kwamba ni lazima watu wa Sudan ya Kusini wapewe haki ya kujitawala wenyewe, na hilo hatuna shaka nalo. Na sisi tunataka umoja, ambao si lazima tuwe nchi moja. Umoja ni maendeleo, ni amani, ni mshikamano." Alisisitiza Al Bashir.

Kiongozi wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir
Kiongozi wa Sudan ya Kusini, Salva KiirPicha: AP

Akipigia mfano wa Bara la Ulaya, Al Bashir amewaambia watu wa Kusini kwamba nchi za Ulaya zilianzisha Vita ya Kwanza na vya Pili vya Dunia, ambavyo viliua mamilioni ya watu na kuharibu kabisa dunia na bara lao, lakini baadaye walikaa kitako na kukubaliana kwamba amani ndio msingi wa kila kitu, ambapo sasa zimebakia kuwa na umoja na amani, huku kila nchi ikiwa na utambulisho wake na dola yake.

Wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Juba, mapema leo asubuhi, Rais Bashir alipokewa na Salva Kiir na wanasiasa wengine wa ngazi za juu wa Sudan ya Kusini, na kupitishwa juu ya zulia jekundu, ambapo alikagua gwaride maalum kwa heshima yake.

Hotuba yake aliyoitoa mwisho wa mwaka uliopita, ambayo ilisisitiza juu ya kuyatambua na kuyaheshimu maamuzi ya watu wa Kusini, inatajwa kwamba imempatia sifa katika jimbo hili, na tangu hapo maoni ya watu kuhusu Bashir yamekuwa mazuri.

Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Barnaba Marial, aliliambia Shirika la Habari la AFP, kwamba wangelimpa mapokezi makubwa Rais Bashir kwani hotuba yake ya mwisho wa mwaka iliwaridhisha wengi.

Karibuni wakaazi milioni nne wa Kusini wamejiandikisha kuwa wapiga kura, na wanatarajiwa kushiriki kwenye kuamua hatima ya eneo lao, Jumapili ijayo. Kura hii ni sehemu muhimu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kati ya Kaskazini na Kusini, ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili, vikiwa vimegharimu maisha ya raia milioni mbili na kuwageuza wengine milioni nne kuwa wakimbizi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Othman Miraj