Waziri wa Ajira wa Ufaransa huenda akajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa Ajira wa Ufaransa huenda akajiuzulu

Waziri wa Ajira wa Ufaransa, huenda akajiuzulu kwa sababu ya tuhuma kuwa alipokea michango ya fedha kinyume na sheria, wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais katika mwaka 2007.

French President Nicolas Sarkozy listens to speeches during his visit at Brie-Comte-Robert hospital, some 30km east of Paris, France, 06 July 2010. Sarkozy rejected 06 July allegations that he and his party treasurer received illegal campaign donations, branding them political smears. An accountant, identified by the investigative website Mediapart as Claire T., said Eric Woerth, a Sarkozy ally and treasurer of his UMP party, received the donation in March 2007, ahead of Sarkozy's election victory in May. EPA/YOAN VALAT

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.

Kashfa hiyo ni changamoto kali kabisa kwa serikali ya Rais Nicolas Sarkozy na leo usiku atahotubia taifa kwa njia ya televisheni katika jitahada ya kuituliza kashfa hiyo.

Kashfa hiyo imesababisha umaarufu wa Rais Sarkozy kupungua kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu alipoingia madarakani mwaka 2007. Hata chama chake tawala cha UMP kinachofuata sera za kihafidhina kimefedheheshwa. Kashfa hiyo imechangia pia serikali kushindwa katika uchaguzi uliofanywa siku ya Jumapili kugombea kiti cha mbunge katika mtaa uliokuwa ukidhibitiwa na chama cha UMP.

Ni matumaini ya Rais Sarkozy kuwa leo usiku atakapotoa hotuba yake ya taifa kupitia televisheni, atafanikiwa kuizima kashfa hiyo na kurejea katika mipango yake ya kurekebisha mfumo wa malipo ya uzeeni. Waziri wake wa ajira,Eric Woerth anashughulikia mageuzi hayo.

Waziri huyo ndio anaetuhumiwa kupokea mchango wa Euro 150,000 kutoka kwa mwanamke tajiri kabisa nchini Ufaransa, Lilliane Bettencourt, anaemiliki kampuni ya vipodozi ya LÓreal. Inadaiwa kuwa waziri huyo alipokea fedha hizo, wakati wa kampeni ya uchaguzi wa rais uliogombewa na Sarkozy mwaka 2007.

Bibi Bettencourt mwenye umri wa miaka 87, ni mmojawapo wa matajiri waliofaidika sana kwa nafuu ya kodi iliyoidhinishwa na Sarkozy baada ya kushinda uchaguzi huo. Bettencourt alirejeshewa Euro milioni 30 kama nafuu ya kodi.

Wakati huo, Woerth alikuwa waziri wa bajeti akaiwa pia na dhamana ya kuzuia ukwepaji wa kodi. Wakosoaji wake wanauliza iwapo alitumia vibaya madaraka yake ili kumkinga Bettencourt dhidi ya ukaguzi wa kodi. Waziri Woerth amekanusha kupokea fedha zo zote kinyume na sheria. Na ripoti iliyotolewa haraka hiyo jana na serikali, imesema, hakuna uashahidi wo wote kuwa waziri huyo aliingilia kati kumlinda Bettencourt dhidi ya ukaguzi wa malipo ya kodi.

Hata hivyo, waziri Woerth hii leo amesema kuwa anafikiria kujiuzulu kama mweka hazina wa chama cha UMP ili kujiepusha na dhana ya kuwepo mgongano wa maslahi, kati ya dhima yake ya kukusanya michango ya chama na kama kiongozi serikalini. Wafuasi wa Sarkozy wanasema mada hiyo imeshamalizika, lakini wapinzani wa serikali wanashikilia kuwa bado kuna masuala mengi yanayongojea jawabu.

Mwandishi:P.Martin/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com