1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili wabakishwa kugombea ukuu wa IMF

14 Juni 2011

Kinyanga'nyiro cha kuwania ukuu wa Shirika la Fedha la Kimaifa (IMF), sasa kimeingia hatua ya fainali kati ya Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, na Gavana wa Benki Kuu ya Mexico, Augustin Carstens.

https://p.dw.com/p/11a1R
Christine Lagarde na Agustin Carstens, wagombea wa ukuu wa IMF
Christine Lagarde na Agustin Carstens, wagombea wa ukuu wa IMFPicha: picture alliance/dpa

Bodi ya wakurugenzi IMF sasa imewabakisha wagombea hao wawili kuuwania wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, baada ya mgombea wa tatu kusshindwa kupenya kwenye mchujo. Gavana wa Benki Kuu ya Israel, Stanley Fischer, aliyekuwamo katika kinyang'anyiro hicho, ameangushwa na umri wake wa miaka 67.

Linapokuja suala la kugombea wadhifa huu kwa mara ya kwanza, umri ni sheria muhimu kufuatwa na IMF, ambapo kwa mujibu sheria hiyo Stanley hawezi kugombea kwa kuwa ameshavuuka miaka 65.

Sasa msimamo thabiti wa nchi za Ulaya kumuunga mkono Lagarde wa Ufaransa, unamuweka mwanasiasa huyo katika nafasi nzuri ya kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la IMF kuziba pengo lililoachwa na Mfaransa mwenzake, Dominique Strauss-Kahn, aliyelazimika kujiuzulu mwezi uliopita kutokana, akikabiliwa na tuhuma za kujaribu kumbaka mtumishi wa hoteli, mjini New York.

Mkurugenzi wa zamani wa IMF, Dominique Strauss-Kahn
Mkurugenzi wa zamani wa IMF, Dominique Strauss-KahnPicha: AP

Hata hivyo, Lagarde, mwenye umri wa miaka 55, amekiri kuwa nafasi hii anayoiomba ni jukumu kubwa sana."Hii ni changamoto kubwa sana, ninayodhamiria kuitekeleza kwa unyenyekevu wote na natumai mwafaka wa kiwango kikubwa utafikiwa."

Lagarde amezunguka dunia ili kujipigia debe na anaungwa mkono hasa na nchi za Ulaya ambapo yeye mwenyewe amekuwa anaishugulikia migogoro ya fedha kwa undani sana. Nafasi ya kuchaguliwa kwake ni kubwa kwani anaungwa mkono pia na Misri, Indonesia na nchi kadhaa za Afrika.

Mshindani wake, Agustine Carstens, ana dhamira ya kuuvunja mwiko wa miaka 65 iliyopita kwenye taasisi hii kubwa kabisa ya kifedha duniani, ambapo hakuna kiongozi wake mkuu aliyetoka mataifa yanayoendelea.

Gavana wa Benki Kuu ya Israel, Stanley Fischer
Gavana wa Benki Kuu ya Israel, Stanley FischerPicha: picture alliance/dpa

Alijipigia dembe kwa waziri wa fedha wa Marekani, Timothy Geithner ambaye, hata hivyo, hakuhakikisha wala kukataa kumuunga mkono. Badala yake, Geithner amesema tu kwamba Carstens anachanganya kipawa juu ya mambo ya fedha na ustadi wa kisiasa.

Tokea IMF iundwe baada ya kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, nafasi ya ukurugenzi mkuu imekuwa ikishikiliwa na mtu kutoka barani Ulaya.

Ikiwa mtaalamu huyo wa uchumi aliyesomea Chuo Kikuu cha Chicago atafanikiwa kuchaguliwa, basi atakuwa mtu wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kuuvunja mwiko huo wa IMF.

Hata hivyo, hata mwenyewe Carstens amekiri kwamba Lagarde ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa IMF.

Bodi ya wakurugenzi ya taasisi hiyo imesema kwamba itakutana na wajumbe hao wawili kwa lengo la kukamilisha uchaguzi tarehe 30 ya mwezi huu.

Mwandishi: Abdu Mtullya/AFPE/RTRE/ZAR
Mhariri: Othman Miraji