1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasimamizi wa Haki za Binadamu hatarini

P.Martin9 Mei 2007

Hatua ya kuzindua “mfumo wa maadili” kuhusu mashirika huru 41 ya wasimamizi wa Umoja wa Mataifa,imesababisha hofu ya kupunguzwa kwa mamlaka na haki za makundi hayo.

https://p.dw.com/p/CHEe

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa(HRC) linalosimamia mashirika hayo huru ambayo huchunguza masuala ya mateso,ubaguzi wa ukabila,mauaji na hata matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake,linatazamiwa kujadili azimio lililopendekezwa na nchi za Kiafrika.Azimio hilo,linatoa mwito wa kuchunguzwa kikamilifu utaratibu wa hivi sasa wa mashirika hayo ya usimamizi.Tarehe ya mwisho ya kufanywa uchunguzi huo ni 18 mwezi Juni.

Lakini zaidi ya watu 12,000 kutoka nchi 147,ikiwa ni pamoja na mashirika 17 ya kimataifa yasio ya kiserikali,wamepeleka waraka uliotiwa saini kwa rais wa HRC,wakieleza upinzani wao kuhusu hatua iliyopendekezwa kuchukuliwa.Miongoni mwa mashirika yasio ya kiserikali ni makundi ambayo hutetea haki za binadamu duniani kama Amnesty International,Human Rights Watch.Waraka hiyo vile vile imetiwa saini na wabunge,wajumbe wa kitaifa wanaotetea haki za binadamu na vile vile wahanga wa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Wapinzani wa azimio ambalo limependekezwa na nchi za Kiafrika wanasema,baadhi ya wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu wanaunga mkono mapendekezo ambayo yatadhoofisha utaratibu maalum,kwani itakuwa vigumu kufanya kazi kwa uzuri na uhuru,bila ya kuingiliwa na serikali.Si hayo tu bali imependekezwa kuwa serikali ziwachague wasimamizi wa haki za binadamu. Wapinzani wanasema,hatua kama hiyo huenda ikaingiza ushawishi wa kisiasa katika utaratibu wa usimamizi.

Hivi sasa mashirika hayo ya usismamizi hayahusiki na serikali kikazi wala katika uchaguzi wa wajumbe wake,kwani huchaguliwa na rais wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Mfumo wa uchunguzi na usimamizi wa mashirika hayo,rasmi huitwa “utaratibu maalum”.Kutokana na uchunguzi wa makundi hayo huru,wanachama wengi wa Umoja wa Mataifa wamekosolewa kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu na makosa mengine.Mjumbe wa Amnesty International katika Umoja wa Mataifa,Yvonne Terlingen amesema, usimamizi unaofanywa na wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa mafanikio makuu kabisa katika mfumo wa haki za binadamu.Amesema,wanachama wote katika Baraza la Haki za Binadamu wanapaswa kutimiza ahadi ya kuhifadhi viwango vya juu kabisa vya haki za binadamu.Kwa hivyo pendekezo la kuchunguza kikamilifu utaratibu maalum,litumiwe kama nafasi pekee ya kuimarisha mfumo wa wataalamu walio huru na sio kupunguza uwezo wao wa kufanya kazi kwa uhuru.