Washukiwa wa mtandao wa Al-Qaeda wauawa Yemen. | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Washukiwa wa mtandao wa Al-Qaeda wauawa Yemen.

Jeshi la Yemen limewaua zaidi ya wapiganaji 30 wanaodaiwa kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, ikiwa ni kampeni ya nchi hiyo kupambana na mtandao huo wa kigaidi.

Jeshi la Yemen likiwa katika operesheni yake kupambana na magaidi.

Jeshi la Yemen likiwa katika operesheni yake kupambana na magaidi.

Kwa mujibu wa Kamati ya Ngazi ya juu ya Usalama nchini humo, shambulio hilo lililofanyika mapema leo liliwalenga wanachama wa Al-qaeda waliokuwa wakikutana katika jimbo la Shabwa mashariki mwa Yemen, kupanga mashambulio.

Kamati hiyo imesema shambulio hilo la leo lililofanywa na Yemen, lililokuwa likilenga kuzuia mashambulio ambayo yangefanywa na watu hao, lilidhamiriwa katika mkutano huo wa magaidi, waliokuwa wakikutana katika mji wa Wadi Rafadh, kupanga kuishambulia Yemen na vitega uchumi vingine vya kigeni nchini humo, ambapo miongoni mwa waliokuwa wakihudhuria mkutano huo ni pamoja na Kiongozi wa Al Qaeda katika rasi ya Uarabuni Nasser al Wahaishi na msaidizi wake Said al Shihri.

Hata hivyo duru za habari hazikufahamisha nini kilichowatokea viongozi hao wawili.

Miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo ni raia wa Saud Arabia na Iran, lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na raia hao.

Jeshi la Yemen lilifanya shambulio hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wa nchi hiyo, ambao waliujulisha uongozi wa eneo hilo kuhusiana na mkutano huo.

Mbali na kupanga kushambulia vitega uchumi nchini Yemen, washukiwa hao walikuwa wakipanga pia kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi, kufuatia mashambulio yaliyofanywa na Yemen wiki iliyopita.

Desemba 17, Yemen ilifanya shambulio la anga katika moja ya kambi za mafunzo za kundi hilo, katika jimbo la Abyan na kuwaua wanachama 34 wa Al Qaeda.

Maafisa nchini humo na vyanzo vingine vya habari vinasema raia 49 wakiwemo wanawake 23 na watoto 17 ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.

Katika siku hiyo hiyo, wanachama wanne wa Al Qaeda waliuawa katika mji wa Abhar uliopo kilomita 35 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa, katika kile ambacho uongozi nchini humo walichokisema kwamba ni operesheni ya kuzuia mashambulio yaliyopangwa kufanywa na mtandao huo wa kigaidi wa Al Qaeda.

Shambulio hilo la leo, linafanya jumla ya wanachama wa Al-qaeda waliouawa na Yemen kufikia 68, kwa muda wa siku nane zilizopita.

Wizara ya Ulinzi ya Yemen imesema zaidi ya wanachama 30 wa Al Qaeda wamekamatwa tangu kufanyika kwa shambulio la Desemba 17.

Yemen imekuwa ikiendesha operesheni yake hiyo kupambana na mtandao wa ugaidi huku ikiungwa mkono na Marekani, ambapo Wizara ya Ulinzi ya Marekani imethibitisha kuipa karibu dola milioni 70 katika kuisaidia kijeshi Yemen katika kipindi cha mwaka huu, msaada ambao unalenga kusaidia kuzuia kujipanua kwa mtandao huo wa kigaidi nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(ap, afp)

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan

 • Tarehe 24.12.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LD7i
 • Tarehe 24.12.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LD7i
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com