Wanamaji wa Uingereza wakaribishwa nyumbani | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wanamaji wa Uingereza wakaribishwa nyumbani

Wanamaji 15 wa Uingereza waliokuwa wakishikiliwa na Iran kwa siku 13 wamerudi nyumbani hapo jana katika hali ya hisia nzito baada ya kumalizika kwa mzozo ambao Waziri Mkuu Tony Blair amesema umetatuliwa bila ya makubaliano yoyote yale.

Simon Massey na Kaye Turney wanamaji wawili kati ya 15 wakizungumza kwa furaha baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Heathrow.

Simon Massey na Kaye Turney wanamaji wawili kati ya 15 wakizungumza kwa furaha baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Heathrow.

Kukaribishwa nyumbani kwa wanamaji hao kumewacha masuala mengi yanayodai majibu.

Kuna masuala licha ya furaha za makaribisho baada ya serikali ya Iran kusema kwamba imepokea taarifa ya kuomba radhi kutoka Uingereza ambalo lilikuwa dai kuu ililolitowa kwa ajili ya kuwaachilia wanamaji hao 15.

Wanamaji hao wa Kingereza walisafirishwa kwa helikopta mbili za kijeshi kwenda kwenye kambi ya kijeshi ya Devon kusini magharibi ya Uingereza baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow wakiwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Uingereza British Airways kutoka Tehran.

Wanamajji hao wanaume 14 na mwanamke mmoja walionekana kutulia na kutabasamu huku wakikumbatiana kwa furaha kabla ya kujiunga na familia zao.

Pongezi juu ya mwenendo wao zimetoka kwa kiongozi wa kijeshi wa ngazi ya juu kabisa Naibu Jemedari wa Kikosi cha Anga Sir Jock Stirrup ambaye amesema ana fahari kubwa mno na kundi hilo ambalo lilitekwa na wanajeshi wa Iran kaskazini mwa Ghuba hapo tarehe 23 mwezi wa Machi.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Des Browne amesema utendaji wa wanamaji hao ulikuwa wa ushujaa mkubwa na heshima baada ya Iran kuwashutumu kuwa wameingia kwenye bahari ya eneo lao kinyume na sheria dai ambalo linakunushwa na Uingereza.

Pande zote mbili katika mzozo huo mzito wa kidiplomasia zinadai kuuvuka kwa ushindi wa kimaadili ikiwa ni masaa 24 baada ya Rais Mahmoud Ahmedinejad kusema kwamba anawaachilia huru wanamaji hao kama zawadi kwa wananchi wa Uingereza.

Ali Akbar Velayati waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Iran na mshauri mpya kwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei amesema Uingereza ilituma baruwa ya kuomba radhi kwa Iran siku moja kabla ya tangazo la Ahmedinejad.

Afisa mwandamizi wa Iran anasema serikali ya Iran imefanikisha malengo yake katika mzozo huo wa mateka.

Lakini wakati wanamaji hao 15 wakiwasili nyumbani wakiwa katika sare zao za kijeshi badala ya suti walizovalishwa Tehran Blair amesema kuachiliwa kwao kumekuja bila ya makubaliano yoyote yale,bila ya mazungumzo na bila ya makubaliano ya pembeni ya aina yoyote ile.

Kurudi kwa kundi la wanamaji hao kumekwenda sambamba na kuuwawa kwa wanajeshi wanne wa Uingereza nchini Iraq ambapo Blair ameseme kumeonyesha ubaya halisi wa ugaidi katika eneo hilo. Pia amerudia kutowa shutuma zake kwa Iran kuhusika na ugaidi.

Amesema wakati ndio kwanza wanafurahia kurudi kwa wanamaji 15 leo pia wanahuzunika na kuomboleza kupoteza wanajeshi wao huko Basra ambao wameuwawa kama matokeo ya kitendo cha ugaidi.

Katika mkutano na waadishi wa habari hapo Jumatano Ahmedinejad amesema kwamba Uingereza ilituma baruwa ikiahidi kwamba jeshi lake halitoingia kwenye bahari ya eneo la Iran.

Aliidhihaki Uingereza kwa kutia chumvi mno kwenye vyombo vya habari wakati wa mzozo huo na rais huyo wa Iran amempa nishani kamanda wa Walinzi wa Kikosi cha Mapinduzi kilichowateka Waingereza hao.

Uingereza ilikuwa imekasirishwa kwa namna wanamaji hao walivyokuwa wameanikwa kwenye televisheni ya Iran wakionekana kuomba radhi jambo ambalo inasema wamelifanya kwa kushurutishwa.

Kuachiliwa kwa wanamaji hao kunafuatia vita vya propaganda vilivyoendeshwa kwenye vyombo vya habari vya nchi mbili hizo kadhalika jitihada za siri za kidiplomasia ikiwa ni pamoja na repoti kwamba Syria na Qatar zimesaidia suala la kuachuiliwa kwao.

 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGo
 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com