1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati waandamana kupinga mkutano wa G8

Saumu Mwasimba7 Julai 2008

Kilio chao ni kuwataka viongozi wanaokutana kukabiliana na umaskini,mabadiliko ya hali ya hewa na mfumko wa bei

https://p.dw.com/p/EXWb
Waandamanaji katika barabara za mji wa Sapporo kisiwani Hokkaido ''Picha: AP

Maandamano ya wanaharakati mbali mbali yanafanyika karibu na eneo kunakoendelea mkutano wa viongozi wakuu wa dunia huko Japan.

Waandamanaji hao ambao wamesafiri kutoka nchi mbali mbali kuanzia Korea Kusini,Ufilipino hadi Marekani wanapinga hatua ya kushindwa kwa viongozi hao kupambana na umaskini duniani miongoni mwa matatizo mengine.

Waandamanaji wa matabaka mbali mbali kuanzia wale walala hoi kutoka nchi za mbali hadi wanaharakati walio wenyeji wameamua kupiga kambi karibu na eneo kunakofanyika mkutano wa viongozi wakuu wa dunia.

Hawajaruhusiwa lakini kusogea karibu sana na eneo hilo.Kiasi cha wanandamanaji 1000 wamekaa katika matenti wakivumilia mvua kama kilomita 30 kutoka mjini Toyako mji ulioko milimani huko kaskazini mwa Japan.

Katika hatua ya aina yake maafisa nchini Japan wamewaruhusu wanaharakati hao kukaa bure katika eneo hilo katika juhudi za kupunguza matatizo ya hoteli za kulala pamoja na kuweka hali nzuri ya kudhibiti maandamano kuzuia ghasia.

wanaharakati hao wenye hasira wametundika mabango kila mahali huku wakipepea bendera zao kutoka milimani zilizoandikwa hakuna G8 .

Hata hivyo kuna baadhi ya wakaazi wa eneo hilo ambako wanaharakati wamepiga kambi hawana wanalojua kuhusu kinachoendelea hali ambayo inawafanya waandalizi wa maandamano hayo kuwashawishi wakaazi hao kujiunga nao wakijitolea hata kununua mboga za baadhi ya wafanyibiashara wadogo wa eneo hilo.

Wanaharakati hao lakini hawajavunjika moyo wanasema nia yao ni moja tu kufikisha ujumbe wao mahsusi kwa viongozi wakuu wa dunia wanaokutana katika hoteli ya kifahari bila ya kuwajali watu maskini wanaoteseka duniani

Mwanaharakati mmoja kutoka shirika la Oxfam alisema na hapa tukimnukulu.

''Badala ya viongozi wa G8 kuwa na wakati mzuri kama huu katika eneo hili la kitalii la kupendeza la Toyako kwanza wangechukua dhamana ya ahadi walizotoa kwa Afrika,wangechukua dhamana juu ya mzozo wa chakula na mabadiliko ya hali ya hewa.''

Wakaazi asili wa kisiwa cha Hokkaido kunakofanyika mkutano wa G8 wanaojulikana kama kabila la Ainu wamefanya maombi maalum ya kufanikisha maandamano yao dhidi ya viongozi hao wakiungwa mkono na kundi la wanaharakati wengine kutoka Korea Kusini walibeba mishumaa na kusali kwa kwa lugha yao ya Ainu.

Waainu waliachwa bila makaazi wakati masettlea wa bara kutoka Honshnu walipoamua kuingia na kuishi Hokkaido katika karne ya 19 na hadi sasa watu hao wa kabila la Ainu wameachwa nyuma kielimu,na kimapato katika nchi hiyo ya Japan.

Hawajakosekana pia waandamanaji wakijerumani ambao bado wanakumbuka maandamano makubwa waliyoyafanya mwaka jana mjini Hillegendam.

Halikadhalika nchini Ujerumani wapo wakosoaji wanaoghadhabishwa na tabia ya viongozi hao wa dunia wanaopenda kutoa ahadi nyingi bila ya kuzitekeleza kama vile Johannes Lauterbach kutoka shirika la Attac ambaye anasema.

''Katika mkutano wa Heiligendamm yalizungumzwa mengi lakini hakuna hata moja lililotekelezwa.Zilitolewa ahadi tupu kubwa kubwa kwa nchi zinazoendelea. lakini cha msingi ni kwamba hata suala la kuongeza misaada ya maendeleo bado halijafanyika.''

Maandamano ya kupinga mkutano wa safari hii wa viongozi wa G8 hata hivyo hayajawa na shime kama mwaka jana ujerumani ambapo maelfu kwa maelfu ya waandamanaji walishiriki na kuzusha ghasia mbaya wakitumia silaha hatari pamoja na mawe.