Wanaharakati wa Misri wangali macho | Magazetini | DW | 21.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wanaharakati wa Misri wangali macho

Mada kuu katika magazeti ya Ujerumani leo jumatatu,ni machafuko mapya nchini Misri, uchaguzi wa Uhispania na pia hatua zinazozingatiwa kuchukuliwa na serikali ya Ujerumani kukabiliana na wanazi mamboleo.

Basi tutaanza na BAADISCHE ZEITUNG linaloandika:

"Waandamanaji nchini Misri wanajikinga dhidi ya viongozi wa serikali ya zamani, ambao wametazamiwa kushika madaraka kwa muda wa mpito tu. Lakini majenerali wa kijeshi wanangánia kubakaia madarakani. Wamisri wengi wana hofu kuwa baraza tawala la kijeshi, halitokuwa tayari kuikabadhi madaraka serikali ya kiraia na kidemokrasia baada ya uchagauzi ujao. Kwa hivyo, haistajaabishi kuwaona vijana wa vuguvugu la mageuzi wakikusanyika tena kwenye uwanja wa Tahrir, baada ya polisi kupambana na waandamanaji. Ujumbe wao ni kuwa wanaharakati wangali macho. "

Gaazeti la STUTTGARTTER NACHRICHTEN likiandika kuhusu mada hiyo linaeleza hivi:

"Wimbi la furaha limepita, lakini nchi hiyo haitorejea kule ilikotokea. Umma wa Misri unangojea kwa hamu kubwa, uchaguzi ujao na hakuna mamlaka yo yote nchini humo itakayoweza kuzuia uchaguzi wala kuikandamiza hamu ya umma unaotaka uhuru. Kwa maoni ya gazeti hilo, demokrasia haitopatikana haraka, lakini yeyote atakaeshika madaraka, atapaswa kukumbuka kuwa sasa umma wa Misri unajiamini."

Tukitupia jicho Uhispania inayopambana na mzozo wa madeni makubwa, gazeti la DER NEUE TAG limeandika:

"Ikiwa serikali mpya ya Uhispania haitofanikiwa kuwasilisha kwa umma mpango wa kupunguza matumizi unaohitajiwa kwa dharura, basi nchi hiyo ipo katika hatari ya kusambaratika kiuchumi na hilo litakuwa na athari zake katika nchi zingine za Ulaya vile vile. Hata kama Uhispania italazimika kuomba msaada wa kimataifa, ukweli ni kwamba wasiwasi unazidi kuhusu uwezo wa nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya kuyalipa madeni yake."

Gazeti la BILD ZEITUNG likiandika juu ya mada hiyo hiyo linasema:

"Sasa inatosha, kwani tangu miaka miwili iliyopita, Ujerumani imetoa msaada kwa nchi za Ulaya zinazokabiliwa na kitisho cha kufilisika. Ujerumani imedhamini mikopo ya mabilioni ya euro katika mfuko maalum wa kuziokoa nchi za kanda ya euro. Madeni hayo yatapaswa kulipwa na wajukuu wa vizazi vijavyo. Msaada huo umetolewa kwa kuzingatia sababu za kiuchumi. Lakini moja lapaswa kuzuiliwa. Madeni hayo ya mabilioni yasiondoshwe kwa Benki Kuu ya Ulaya ECB kuchapisha fedha zaidi - yaani kuendelea kuchapisha fedha kwa azma ya kuyamaliza madeni ya kila nchi iliyoshindwa kudhibiti matumizi yake. Matatizo ya madeni hayawezi kutoweka kwa kuchapisha fedha zaidi."

Kwa kumalizia udondozi wa magazeti ya Ujerumani tunageukia mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari nchini Ujerumani - itikadi kali za mrengo wa kulia na makundi ya wanazi mamboleo. Gazeti la VOLKSSTIMME kutoka Magdeburg linasema:

"Mpango uliotangazwa na waziri wa sheria wa Ujerumani Sabine Leutheusser-Schnaarrenberger, wa kutaka kuzilipa fidia familia za wahanga wa mauaji yaliyofanywa na wanazi mamboleo, unaazimia wema lakini ni mapema mno kufanya hivyo. Kwani kuna hatari ya fidia hiyo kueleweka vibaya, ilimradi makosa na uzembe uliofanywa na maafisa hayakutangazwa rasmi na kutathminiwa vipi wanazi mamboleo waliweza kufanya mauaji kwa miaka kadhaa bila ya kugunduliwa. Ili kuzuia hiyo, waziri huyo labda angeanzisha mfuko maalum wa kuzisaidia familia za wahanga hao. Mazungumzo ya kulipa fidia yafanywe baada tu ya kujua kila kitu kuhusu kashfa hiyo na kuwatambua wale waliowajibika."

Mwandishi:Martin,Prema/dpa

Mhariri: Josephat Charo