Walowezi wa Kiisraeli washambulia mali za Wapalestina | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.12.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Walowezi wa Kiisraeli washambulia mali za Wapalestina

Israel imewaweka wanajeshi wake katika hali ya tahadhari kuzuia machafuko zaidi katika mji wa Hebron kwenye Ukingo wa Magharibi.

A Jewish settler throws a stone from a rooftop overlooking Palestinian houses in the West Bank city of Hebron, Tuesday, Dec. 2, 2008. Dozens of Jewish settlers rioted Tuesday in the West Bank town of Hebron, clashing with the Israeli troops who guard them but who may also soon evict them from a disputed building they've occupied. (AP Photo/Nasser Shiyoukhi)

Mlowezi wa Kiyahudi arushia jiwe nyumba za Wapalestina katika mji wa Hebron.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya walowezi wa Kiisraeli kula kiapo kuwa watalipiza kisasi hatua ya kuwaondosha kwa nguvu Wayahudi wa itikadi kali kutoka nyumba inayogombewa na Wapalestina na walowezi.Eneo zima la kusini katika Ukingo wa Magharibi limetangazwa eneo la kijeshi ili kuwazuia Waisraeli kumiminika tena katika mji wa Hebron uliokumbwa na ghasia.

Walowezi wa Kiisraeli wametoa wito wa kuwepo "juma la kulipiza kisasi". Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari,hadi watu 25 walijeruhiwa na polisi pia ni miongoni mwao.Wakati huo huo walowezi katika mji wa Hebron uliotengwa wamekula kiapo kuendelea na harakati zao za kuwachosha maafisa wa serikali na vikosi vya usalama.Wamesema,mara kwa mara watarejea katika majumba walikofukuzwa mjini Hebron.Jana jioni vijana walisababisha ghasia na walichoma moto mali za Wapalestina katika mji wa Hebron.Moto uliharibu magari na nyumba moja ambako familia ya Kipalestina ilikuwa ikijificha.Mlowezi mwingine aliefyatulia risasi nyumba ya Wapalestina aliwajeruhi watu watatu.Mashahidi wamesema,baba mtu na mwanae wa kiume wapo katika hali mbaya.

Kwa upande mwingine,kiongozi wa walowezi aliezungumza hii leo na Redio ya Israel amesema,Mmarekani mwenye asili ya Kiyahudi alienunua nyumba iliyozusha ugomvi,ameahidi kununua nyumba zaidi katika mji wa Hebron ili kuimarisha kuwepo kwa Waisraeli katika kile alichokiita" mji wa mababu wa mababu zao".

Kuambatana na makubaliano ya mwaka 1988,mji wa Hebron umetengwa sehemu mbili zinazodhibitiwa na Waisraeli na Wapalestina.Kati ya Wayahudi 600 hadi 800 huishi miongoni mwa Wapalestina 200,000 chini ya ulinzi mkali wa majeshi ya Israel katika mji ulio mkubwa kabisa kwenye Ukingo wa Magharibi.Jamii hizo mbili zinaishi katika hali ya mvutano mkubwa na hali ilizidi kuwa mbaya tangu majuma kadhaa baada ya Mahakama Kuu ya Israel kuitaka serikali kuwatoa wapangaji wa Kiyahudi kutoka nyumba inayogombewa mpaka itakapoamuliwa kisheria nani alie mmiliki halisi.Tangu wakati huo Wayahudi wenye itikadi walikuwa wakimiminika Hebron kuzuia walowezi kuhamishwa kwa nguvu.Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak alitoa amri ya kuwaondosha kwa nguvu baada ya majadiliano pamoja na viongozi wa walowezi ya kuondoka kwa hiyari kutofanikiwa.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com