Wajuwe wagombea urais wa Guinea | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.11.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wajuwe wagombea urais wa Guinea

Jumapili hii (7 Novemba 2010) taifa la Guinea linaingia kwenye uchaguzi wa marudio, na huu hapa ni wasifu wa wapinzani wawili wakubwa wa uchaguzi huo, Cellou Dalein Diallo na Alpha Conde.

Mpiga kura nchini Guinea katika mwezi Juni 2010

Mpiga kura nchini Guinea katika mwezi Juni 2010

Cellou Dalein Diallo ana umri wa miaka 58. Kwa miaka 10 alikuwa kwenye baraza la mawaziri la kiongozi wa kijeshi Jenerali Lansane Conte kabla hajajiunga na chama kikuu cha upinzani mwaka 2007, ambapo katika awamu ya kwanza ya uchaguzi alipata asilimia 43 ya kura.

Cellou Dalein Diallo

Cellou Dalein Diallo

Diallo anatokea kwenye kabila kubwa la Fulani nchini Ivory Coast na alilelewa na familia ya maimamu. Baba yake alikuwa na wake wanne na watoto 20. Alisomea utawala katika chuo kikuu cha Conackry na aliingia kwenye serikali akiwa na miaka 24. Alifanya kazi benki kuu ya nchi hiyo chini ya utawala wa Conte na kupanda vyeo hadi kufikia waziri mkuu. Mwaka 2006 alifukuzwa kutoka wadhifa huo kwa kile anachosema ni jitihada zake za kujenga utawala bora na "hujuma za kundi la kimafia lililokuwa limemzunguka rais".

Wakati kundi la wanajeshi vijana walipochukua madaraka mwaka 2008, mwanzoni Diallo aliwaunga mkono akiamini kwamba wangeliendesha kipindi cha mpito kwa salama kuelekea utawala wa kiraia, lakini alianza kutafautiana nao alipong'amua kwamba walikusudia kuendelea kubakia madarakani milele. Wakati vikosi vya kijeshi vilipouwa waandamanaji 150 na katika uwanja wa mpira, yeye alipigwa vibaya na vikosi hivyo hali iliyosababisha apelekewe matibabuni jijini Paris, Ufaransa.

Alpha Conde

Alpha Conde

Kwa upande wake, Alpha Conde, yeye ni mtu mzima wa miaka 72, ambaye ametumia sehemu kubwa ya maisha yake akiwa uhamishoni nje na kipindi fulani katika jela za nchini mwake pale alipokuwa akipingana na tawala za kijeshi.

Mpinzani huyu wa miaka mingi anasifika kwa kipaji chake cha kuzungumza ambacho huwavuta sana wasikilizaji wake. Waungaji mkono na wapinzani wake wanamuelezea kama mtu mwenye amri na anayejisikiliza sana mwenyewe kuliko kusikiliza watu wengine.

Alizaliwa tarehe 4 Machi 1938 katika eneo la Boke na wazazi wa kabila la Malinke. Alihamia Ufaransa akiwa na miaka 15 tu kwa ajili ya masomo, ambako alihitimu shahada za uchumi, sanansi ya jamii na sheria na baadaye kuwa mwalimu katika chuo kikuu cha Sorbonne, jijini Paris.

Katika miaka ya '60 aliongoza Shrikisho la Wanafunzi wa Kiafrika nchini Ufaransa na akongoza vuguvugu lililoupinga utawala wa kidikteta wa Rais wa kwanza wa Guinea huru, Ahmed Sekou Toure. Naye Sekou Toure akajibiza upinzani huo wa Conde kwa kumuhukumu kifo akiwa uhamishoni hapo mwaka 1970. Conde hakurudi Guinea mpaka hapo mwaka 1991, ikiwa ni miaka saba baada ya kifo cha Sekou Toure.

Rais Lansana Conte, aliyeshika madaraka kupitia mapinduzi, alihalalisha vyama vya siasa uliomuwezesha Conde kushiriki chaguzi za mwaka 1993 na 1998, ambazo zote mbili zimelalamikiwa kwamba ziliibiwa.

Mwanzilishi huyu wa chama cha Rally of Guinean People (RPG) alikamatwa mara tu baada ya mwaka 1998 na kuwekwa kizuizini hadi mwaka 2000 kwa "kulihujumu taifa". Lakini adhabu hiyo ilifutwa mwaka 2008 kutokana na shinikizo la kimataifa. Baada ya mapinduzi ya 2008, Conde alipigania ufanyike uchaguzi na daima amekuwa akilituhumu jeshi la nchi yake kwa mauaji ya maangamizi dhidi ya watu 150 waliokuwa wakiandamana kwenye uwanja wa mpira mjini Conackry.

Mwandishi: Mohammed Khelef

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com