Wajumbe wa ECOWAS wawasili Cote d'Ivoire
28 Desemba 2010Marais Bon Yayi wa Benin, Ernest Koroma wa Sierra Leone na Pedro Pires wa Cape Verde wamepelekwa Abidjan na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS kumuonya Gbagbo kuwa vikosi vya kanda hiyo huenda vikapelekwa Cote d'Ivoire kumngóa madarakani akiendelea na ubishi wake.Kwa kweli, marais hao watatu si miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Gbagbo katika ECOWAS, lakini wamekwenda na ujumbe uliotiwa saini na viongozi wenye usemi zaidi kama vile Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, ukimtaka kiongozi huyo angátuke madarakani.
Hata hivyo, hakuna ishara kuwa Gbagbo atauitikia wito huo kwani anaenedelea kushikilia kuwa yeye ndie aliechaguliwa kihalali kuwa kiongozi wa Cote d'Ivoire. Vile vile ameonya kuwa kitisho cha kutumia nguvu za kijeshi za ECOWAS huenda kikazusha vita katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi.
Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Ndani Emile Guirieoulou alisema kuwa wajumbe wa ECOWAS watakaribishwa kama ndugu na marafiki lakini wanapaswa kuheshimu uhuru wa Cote d'Ivoire. Serikali haitovumilia mambo yake kuingiliwa kati wala haitoitikia mwito wo wote ule wa kumkabidhi madaraka Ouattara. Msemaji wa serikali Ahoua Don Melo amesema, hakuna taasisi yo yote ile ya kimataifa iliyo na haki ya kuingilia kati na kumweka rais katika nchi inayojitawala yenyewe.
Wote Gbagbo na Ouattara wanadai kushinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita na kila mmoja wao amejitangaza rais.Lakini Ouattara ndie alietambuliwa na wasimamizi wa uchaguzi wa Umoja wa Mataifa na madola makuu kama mshindi wa uchaguzi huo wa rais. Ouattara anaeitumia hoteli moja mjini Abidjan, kama makao yake makuu analindwa na vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa kwani amezingirwa na wanajeshi wanaomuunga mkono Gbagbo.
Zaidi ya watu 170 wameuawa katika machafuko yaliyozuka nchini humo kufuatia uchaguzi wa mwezi uliopita. Inahofiwa kuwa nchi hiyo ipo katika hatari ya kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi.P.Martin/AFPE/RTRE
Mpitiaji:Josephat Charo