Wajapan washangilia ushindi kombe la dunia | Michezo | DW | 18.07.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Wajapan washangilia ushindi kombe la dunia

Japan ililipuka kwa furaha, baada ya timu yao ya taifa ya wanawake kuibuka kidedea katika fainali ya kombe la dunia jana Jumapili mjini Frankfurt ,nchini Ujerumani, baada ya kuishinda Marekani kwa mabao 3-1.

default

Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake wa Japan wakishangilia bao.

Japan yalipuka kwa furaha baada ya timu yao ya wanawake kunyakua ubingwa wa dunia , na kutimiza "ndoto yao" na "miujiza" kwa nchi hiyo ambayo inajichomoza kutoka katika maafa makubwa ya tetemeko la ardhi na tsunami.

Mlinda mlango wa Marekani Hope Solo, asema kulikuwa na kitu kisichokuwa cha kawaida nyuma ya timu hii ya Japan , pamoja na moyo wa kutokata tamaa, kocha wa Marekani , Pia Sundhage nae asema ushindi wa Japan utasaidia soka la wanawake kukua . Katika Copa America , vigogo vya soka Brazil na Argentina vyaaga mashindano.

Wajapani wamelipuka kwa shangwe , furaha na vifijo alfajiri ya leo , baada ya timu yao ya wanawake kushinda ubingwa wa kombe la dunia,kwa wanawake na kutimiza "ndoto yao", na pia kile kinachoelezwa kama "miujiza", kwa nchi hiyo ambayo ndio kwanza inaanza kupona majeraha ya maafa ya tetemeko la ardhi na tsunami.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeripoti kwa kina kuhusu jinsi watu wanaoishi katika maeneo ya kujihifadhi kaskazini mashariki ya nchi hiyo baada ya tsunami , walivyopokea ushindi huo.

Katsuo Mori, mzee wa miaka 74 ambaye nyumba yake ilizolewa na tsunami, ameliambia shirika la habari la Jiji, kuwa hii itasaidia kuleta uangavu katika eneo hili tunaloishi. Itaimarisha juhudi zetu za kuendelea kuishi.

Katika makaazi hayo ya muda katika mji wa Natori , mama mmoja mwenye umri wa miaka 50 ambaye anafanyakazi za muda Yoshiko Saito ameliambia shirika hilo la habari kuwa ; Wanawake ni imara. Naamini wanawake wataendelea kuwa wakakamavu hapo baadaye.

Japan imekuwa timu ya kwanza kutoka bara la Asia kushinda kombe la dunia la wanawake. Mamia ya mashabiki , wengi wao wakivalia jezi za rangi ya buluu zinazovaliwa na timu ya taifa ya Japan waliingia mitaani katika eneo maarufu la Shibuya, eneo lenye starehe nying kwa vilabu vya usiku, wakiimba , Nippon , Nippon, baada ya kumalizika kwa mchezo huo kiasi saa kumi na mbili na dakika 20 alfajiri saa za Japan.

Ni ushindi mnono ambao unatupa nguvu ya kuendelea na ujenzi mpya , amesema Yukihito Abe, mkuu wa chama cha soka katika mji ambao umeathirika zaidi na janga la tsunami wa Minami-sanriku.

Rais wa heshima wa shirikisho la kandanda nchini Japan Saburo Kawabuchi ametamka kuwa , " sasa naweza kufahamu kuwa miujiza inaweza kutokea". Mlinzi wa timu ya taifa ya Japan , Saki Kumagai ambaye alitumbukiza mpira wavuni akimwacha mlinda mlango wa Marekani Hope Solo akigaagaa , bila kujua la kufanya katika mkwaju wa mwisho wa penalti aliwahi kutembelea eneo la Minami-sanriku kujionea mwenyewe uharibifu uliotokea.

Mlinda mlango wa Marekani Hope Solo alifanikiwa kuweka matumaini ya Marekani hai katika mashindano haya ya kombe la dunia kwa kuonyesha uhodari wake mara kwa mara , lakini alitambua kuwa anakabiliwa na zaidi ya wanawake 11 kutoka Japana jana Jumapili.

Frauen-Fußball-WM Japan USA FINALE JAPAN WELTMEISTER Trauer HOPE SOLO

Mlinda mlango nyota wa Marekani Hope Solo, katika hali ya masikitiko baada ya Japan kuweka wavuni bao la ushindi.

Wanawake hawa wa Japan ambao hawakati tamaa , walicheza kwa moyo wao wote na kuwastua Wamarekani katika fainali, kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mikwaju ya penalti baada ya mara mbili kurejesha mabao dakika za mwisho katika muda wa kawaida na hata katika muda wa nyongeza. Tumefungwa na timu kamambe, Solo amenukuliwa akisema katika tovuti ya timu ya taifa ya Marekani .

Japan imecheza kwa nguvu ambazo hazimithiliki wakati wote wa mashindano haya na kulaza kigogo baada ya kigogo cha soka, ikiwa ni pamoja na mabingwa watetezi na wenyeji wa mashindano Ujerumani katika robo fainali, na vigogo wa sasa Sweden katika nusu fainali.

Kocha wa Marekani Pia Sundhage amesema kuwa timu yake imecheza vizuri zaidi kuliko ilivyofanya katika michezo iliyotangulia katika mashindano hayo lakini walipoteza nafasi nyingi.

Frauen-Fußball-WM 2011 Halbfinale Frankreich - USA

Kocha wa Marekani Pia Sundhage.

Kwa mashabiki wa Marekani ilikuwa ni huzuni kubwa. Wachezaji wa Marekani walikuwa na hakika ya kupata ushindi wa tatu wa kombe hilo, lakini ndoto hizo hazikutimia. Mmoja wa mashabiki wa Marekani alisema.

"Ulikuwa mchezo wa kusisimua sana. Timu zote zilicheza vizuri sana. Mchezo ulikuwa sawa, lakini timu yetu ilicheza vizuri zaidi, lakini walishindwa katika penalti. Nimejisikia furaha kuja hapa kutazama soka safi ya kombe la dunia, hata kama Marekani hatimaye haikushinda".

Kocha wa Marekani Pia Sundhage hata hivyo aliimwagia sifa tele Japan, akisema kuwa ushindi huo utasaidia soka la wanawake kukua baada ya mafanikio hayo nchini Ujerumani mwaka 2011.

Na huko Latin America, Paraguay imeitupa nje ya mashindano mabingwa watetezi Brazil katika michuano ya Copa America jana Jumapili, kwa kushinda mpambano wao wa robo fainali kwa mikwaju ya penalti ,kwa mabao 2-0 baada ya mchezo ambao haukupendeza uliomalizikia kwa sare ya bila kufungana hata baada ya muda wa nyongeza. Siku moja baada ya wanyeji wa mashindano hayo Argentina kuaga mashindano hayo kwa kutupwa nje na Uruguay, mitikisiko imeendelea kutokea katika soka la mataifa ya Amerika ya kusini wakati Venezuela ilipofikia nusu fainali kwa mara ya kwanza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chile. Rais wa Venezuela ambaye anaendelea na matibabu ya saratani nchini Cuba alikuwa wa kwanza kuipongeza timu hiyo inayoitwa kwa jina la utani "Vinotinto".

Na Machester City ya Uingereza imekubali kumuuza mshambuliaji nyota wa Argentina Carlos Tevez kwa timu ya Brazil ya Corinthians, amesema meneja wa timu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza, Premier League , Roberto Mancini leo.

Kwa mujibu wa ripoti makubaliano hayo yatakamilishwa wakati masharti ya binafsi kati ya Tevez mwenye umri wa miaka 27 na klabu yake hiyo mpya yatakapokubaliwa.

Klabu hiyo ya Brazil imekubali kutoa kitita cha euro milioni 40 kwa kupata saini ya mshambuliaji huyo wa Man City lakini Man City imekuwa ikisita kukubali kitita hicho na Corinthians inasemekana wameongeza kidogo dau. Mshambuliaji huyo anataka kuondoka Man City kwa kuwa mwanae wa kike anaishi Latin America na mama yake.

Riadha:

Mkimbiaji Oscar Pistorius ,wa Afrika kusini, anayejulikana kwa jina la utani kama " Blade Runner", ameshindwa jana katika jaribio lake la hivi karibuni la kupata muda wa kuweza kufikia kiwango cha kushiriki katika mbio za mita 400 katika michuano ijayo ya dunia. Oscar mwenye umri wa miaka 24 alikuwa wa nne kwa kutumia sekunde 46.65, akiwa bado nje ya muda wa sekunde 45.25 ambao unahitajika kushiriki katika mashindano hayo ya dunia mjini Daegu nchini Korea ya kusini mwezi ujao wa August.. Mjamaica Lansford Spence alishinda mbio hizo za jana kwa kutumia sekunde 46.34, wakati martyn Rooney kutoka Uingereza akishika nafasi ya pili kwa kutumia sekunde 46.36.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri : Miraji Othman