Waangalizi wa EU wawasili Georgia | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waangalizi wa EU wawasili Georgia

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamewasili nchini Georgia wakiwa na lengo la kudumisha makubaliano ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Ufaransa kufuatia mzozo wa mwezi Agosti kwenye eneo la Kaukasus.

Msimamizi wa ujumbe wa EUMM Hansjörg Haber

Msimamizi wa ujumbe wa EUMM Hansjörg Haber

Chini ya makubaliano hayo Urusi iliridhia hatua ya kuondoa vikosi vyake ifikapo tarehe 10 mwezi Oktoba kufuatia mapambano ya yaliyodumu kwa kipindi cha siku tano katika eneo la Ossetia Kusini.


Kikosi hicho cha Umoja wa Ulaya EUMM kilicho na waangalizi zaidi ya 200 kilianza kushika doria mapema hii leo ikiwa ni hatua ya kudumisha makubaliano ya amani yaliyofikiwa chini ya upatanishi wa Ufaransa.Hata hivyo kikosi hicho hakina idhini ya kuingia kwenye maeneo yanayosimamiwa na wanajeshi wa Urusi.Chini ya makubaliano hayo Urusi inalazimika kuondoa vikosi vyake vyote ifikapo tarehe 10 mwezi huu wa Oktoba.

Waangalizi hao walianza kushika doria kwenye eneo la Bazaleti linalopakana na upande wa mashariki wa jimbo la Ossetia Kusini vilevile maeneo ya magharibi ya Poti na Zugdidi yanayopakana na jimbo la Abkhazia.

Mwanadiplomasia wa Ujerumani anayesimamia ujumbe huo wa EUMM Hansjoerg Haber anaeleza kuwa ''Ujumbe huo ni wa kiraia na hiyo ndiyo changamoto kubwa kwasababu utasimamia maeneo yaliokabiliwa na ghasia, mivutano na wizi.Nadhani wakazi wa eneo hilo wako tayari kushirikiana na watu ambao hawajajihami kwa silaha ila walio na mwelekeo wa kirafiki.''


Waangalizi hao ambao ni watalaam wa masuala ya kijeshi,haki za binadamu pamoja na sheria hawatajihami kwa silaha ila watatumia vifaa vya usalama. Jeshi la Urusi kwa upande wake limesisitiza kuwa waangalizi hao wanaidhini ya kuingia mpaka kwenye maeneo yanayopakana na majimbo yanayotaka kujitenga Ossetia Kusini na Abkhazia tu.Vikosi vyake vitaendelea kubakia kwenye majimbo husika ambayo iliyatambua kuwa huru wakati wa vita hivyo.

Hayo ni kwa mujibu wa Vitaly Manushko msemaji wa vikosi vya kulinda amani vya Urusi kwenye eneo la Ossetia Kusini. Eneo hilo ni njia muhimu ya kusafirishia mafuta na gesi kutoka Bahari ya Caspian.


Umoja wa Ulaya una imani kuwa Urusi itatimiza agizo la kuondoa vikosi vyake hatua kwa hatua ifikapo tarehe 10 mwezi huu.Azma ya hatua hiyo ni kuwezesha polisi wa Georgia kurejea katika maeneo hayo kwa lengo la kudumisha usalama na kuepuka uhalifu.

Kamishna wa masuala ya Kutetea Haki za Binadamu katika Baraza la Ulaya Thomas Hammarberg anaeleza ''Bado wako katika maeneo yanayosimamiwa na vikosi vya Urusi ambako kumeripotiwa vitendo vya uhalifu dhidi ya wakazi na wizi.Tatizo hasa liko katika eneo la Ossetia kusini ambako ujumbe wa Umoja wa Ulaya utasimamia. Majeshi ya Urusi yataondoka ifikapo tarehe 10 mwezi Oktoba.''


Mapigano hayo ya mwezi Agosti yaliathiri uhusiano kati ya Urusi na mataifa ya magharibi ila haikuwekewa vikwazo vyovyote vya moja kwa moja.Georgia kwa upande imeeleza kuwa Urusi inajaribu kuifanya hatua hiyo isuwesuwe.

Wakati huohuo mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo nchini Ufaransa wakiwa na lengo la kuimarisha masuala ya usalama ukiwemo ujumbe wa EUMM ulioko Georgia.


 • Tarehe 01.10.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FS8U
 • Tarehe 01.10.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FS8U
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com