Viongozi wa Marekani na Afrika wageukia biashara | Matukio ya Afrika | DW | 05.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Viongozi wa Marekani na Afrika wageukia biashara

Viongozi wa kisiasa na kibiashara kutoka Marekani na Afrika wanakutana Jumanne hii huku Washington ikitumai kuwa mkutano wa kilele wa kihistoria utapelekea kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika mkutano wa pamoja na waziri John Kerry siku ya Jumatatu.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika mkutano wa pamoja na waziri John Kerry siku ya Jumatatu.

Siku ya kwanza ya mkutano wa kilele kati ya Marekani na Afrika, ambao ndiyo mkubwa zaidi wa aina hiyo kuwahi kufanyika mjini Washington, ilishuhudia maafisa wa Marekani wakiwakosoa wageni wao kuhusiana na masuala ya mageuzi ya kidemokrasia na haki za kiraia. Lakini sasa rais Barack Obama na vigogo wa sekta ya biashara ya Marekani watajaribu kuwashawishi wenzao kwamba Marekani imedhamiria kushiriki katika hadithi ya ukuaji wa Afrika kama inavyofanya China au Ulaya.

Mazungumzo ya Jumatatu yalijikita zaidi katika kuheshimu haki za kiraia, kushughuliki kitisho kinachozidi cha ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi na changamaoto makhsusi kama vile joto dunia na biashara ya wanyamapori wanaolindwa. Lakini mazungumzo ya Jumanne yanaikabili hali halisi, kwamba China imepuuza masuala hayo yote ili kujiimarisha kama mshirika mkubwa zaidi wa Afrika, na kwamba Umoja wa Ulaya unaharakisha makubaliano ya biashara huru na kanda mbalimbali za Afrika.

Desemba 9, 2007 ulifanyika mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Lisbon Ureno, ambapo pande mbili zilisaini makubaliano muhimu ya ushirikiano wa kibiashara.

Desemba 9, 2007 ulifanyika mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Lisbon Ureno, ambapo pande mbili zilisaini makubaliano muhimu ya ushirikiano wa kibiashara.

Kerry: Tuko tayari kwa biashara na Afrika

Waziri wa mambo ya kigeni John Kerry alikuwa muwazi na malengo ya Washington siku ya Jumatatu. "Nasema bila wasiwasi: Tunataka na tutajitahidi kuyashawishi makampuni zaidi ya Marekani kuwekeza barani Afrika. Tunataka makampuni zaidi ya Afrika yawekeze hapa Marekani, na hakuna sababu kwa nini yasifanye hivyo," alisema.

China, Ulaya, Japan na hata India zimeipiku Marekani, kwa kuandaa mikutano ya kilele na viongozi wa Afrika, ambayo ilifikia makubaliano ya biashara ya mabilioni ya dola, na mfano wa China mwaka 2012, mikopo yenye thamani ya dola bilioni 20 kwa serikali za Afrika.

Waafrika wanasema Wamarekani bado wamejifunga katika fikira za zamani kuhusu bara la Afrika, na wanaogopa hasara kuliko washindani wao. Tajiri mzaliwa wa Sudan Mo Ibrahim, moja wa mabilionea wa kwanza wa Afrika alipigia msitari changamoto. "Nimeshangazwa kidofo, kwamba Waafrika niliyokutana nao kwenye ndege...wanakuja hapa kuwaambia wafanyabiashara werevu na wajuzi wa Marekani kuwa, mnajua nini, kuna fursa nyingi sana barani Afrika." Wanapaswa kujisomea kwanza," alisema.

Kila mahala barani Afrika kuna wafanyabiashara wa Kichina, kuna Wabrazil, hakuna hata moja wetu aliekwenda Brazil, au Asia au China kuwaambia waje kuwekeza Afrika. Waligundua wenyewe na wanakuja kuwekeza."

Programu ya Jumanne itashuhudia Waafrika wakishawishiwa na rais Obama, waziri John Kerry na rais wa zamani Bill Clinton, na vile vile maafisa kadhaa watendaji wa mashirika kama General Electric, Coca-Cola au Walmart. "Ukuaji ni wa kweli na ni sasa," alisema Mtendaji mkuu wa General Electric Jeffrey Immelt siku ya Jumatatu. "Hakuna sababu kwa nini biashara za Marekani haziwezi kufika walikofika wengine.

China iliitisha mkutano wa kilele na viongozi wa Afika Oktoba mwaka 2006 mjini Beijing.

China iliitisha mkutano wa kilele na viongozi wa Afika Oktoba mwaka 2006 mjini Beijing.

AGOA haijatimiza malengo

Lakini hata maafisa wa Marekani wanakiri kuwa muundombinu mkuu wa biashara kati ya Marekani na Afrika, sheria ya Ukuaji na Fursa barani Afrika, AGOA ya mwaka 2000, haijafanya vya kutosha kurahisisha njia ya usarishaji wa mafuta kutoka Afrika kwenda Marekani, na kwamba inawakilisha sehemu ndogo tu ya biashara ya China na bara hilo.

"Ni wazi kwamba Afrika ya mwaka 2014 siyo Afrika ya mwaka 2000," alisema mwakilishi wa biashara wa Marekani Michael Froman katika mkutano wa maafisa wa juu wa kiuchumi wa Afrika na wafanyabiashara siku ya Jumatatu. "Wengi wenu mnaondokana na bishara ya mataifa mawili na kuingia katika mikataba na washirika wa kibiashara kama vile Umoja wa Ulaya, unaotoa fursa kwenu kuingia katika soko lake."

Obama alichukuwa hatua siku ya Jumatatu kuonyesha dhamira ya Marekani kwa kutangaza kamati mpya ya ushirikiano baina ya mashirika, itakaongozwa na afisa mwandamizi wa baraza la usalama la ikulu ya White House, kuratibu juhudi za kukuza biashara na uwekezaji.

Changamoto halisi, wanasema wachambuzi na wafanyabiashara wa kiafrika, ni kuzishawishi biashara za Marekani kuondokana na hofu yao ya kihistoria juu ya kufanya biashara katika bara la Afrika na kutambua fursa za ukuaji, zikwemo tabaka kubwa la kati la Afrika.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.