Viongozi wa G7 kujadili juu ya chanjo za COVID-19, uchumi na China | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa G7 kujadili juu ya chanjo za COVID-19, uchumi na China

Rais wa Marekani Joe Biden leo atahudhuria mkutano wa kwanza wa kimataifa tangu aingie madarakani ambapo atashiriki kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G7.Uingereza ni mwenyekiti wa zamu.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Jen Psaki  amethibitisha kwamba Rais wa Marekani Joe Biden leo atashiriki kwenye mkutano wa kilele  wa G-7 na kwamba ataweka mkazo juu ya hatua za pamoja za dunia nzima katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, pamoja na utengenezaji na ugavi wa chanjo ya COVID-19  na njia za kufungua uchumi wa dunia ulioathirika vibaya kutokana na janga hilo. Psaki amesema Marekani imeahidi kujiunga na mpango wa COVAX, unaohusika na utengenezaji na ugavi wa chanjo kwa nchi zinazoendelea.

Kushoto: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson Kati: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Kushoto: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson Kati: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Kwenye mkutano huo utakaofanyika kwa njia ya video rais Biden atazungumzia pia changamoto za kimataifa kama zile zinazotokana na China. Katika hotuba yake ya kwanza mara alipochukua hatamu za uongozi Biden alipozungumzia juu sera ya mambo ya nje alisema China ndio mshindani mkubwa wa Marekani.

Nchi za kundi la G7 ni Marekani , Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia, Japan  na Canada na kwa jumla zina utajiri wa takriban dola trilioni 40 sawa na nusu ya uchumi wa ulimwengu mzima.

Soma zaidi:Mkutano wa viongozi wa G7 na Umuhimu wake duniani

Biden pia anatarajiwa kutangaza kuirudisha Marekani kwenye ushirikiano nan chi nyingine msimamo unatofautiana kabisa na sera ya utawala wa Donald Trump aliyeweka sera ya mambo ya nje iliyoifanya Marekani kujitenga na pia kujijiondoa kutoka kwenye makubaliano ya kimataifa na ushirikiano wa ulimwengu katika mambo mengi. Tangu aingie madarakani, Biden amebatilisha hatua nyingi zilizochukuliwa na Trump kama kujiunga tena na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO.

Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wengine pia watajadili hatua thabiti za kushughulikia mgogoro wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani, jambo linalopewa kipaumbele muhimu na utawala wake. Mkutano huo wa kilele wa leo utaongozwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiwa ni mwenyekiti wa zamu wa kundi la nchi za G7 na ambaye ataongoza mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi hilo uliopangwa kufanyika mnamo mwezi Juni mwaka huu wa 2021.

Chanzo: RTRE/DPA